Pages

Saturday, August 24, 2013

RIPOTI:::NDEGE YA RAISI YAHUSISHWA NA KUBEBA MIHOGO NA MKAA

Ngege maalumu ya Rais Tanzania pia hutumika kubeba viongozi wa Serikali 
Kwa ufupi
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaeleza kuwa, tuhuma hizo zilitolewa na wabunge hao wakati wa kikao chao na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mwezi uliopita.
Wabunge wa CCM Zanzibar wameibua zengwe jipya dhidi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kwamba anatumia ndege ya Rais kubebea mkaa, mihogo na ndizi kutoka Pemba kwenda Unguja.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaeleza kuwa, tuhuma hizo zilitolewa na wabunge hao wakati wa kikao chao na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mwezi uliopita.

Kitendo hicho kinachodaiwa kufanyika mwezi uliopita kimeonekena kuwakera baadhi ya viongozi wa Serikali wakiwamo wabunge wa CCM Zanzibar, ambao wakati wa kikao hicho na Rais Dk Shein mwezi uliopita mjini Zanzibar, walilizungumza kwa uchungu na kuomba Rais amuonye Maalim Seif kwa kuigeuza ndege ya Rais kuwa ya mizigo.
Anayedaiwa kuibua hoja hiyo ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM), Sadifa Juma Khamis, ambaye alisema kuwa kitendo hicho cha Makamu wa Kwanza wa Rais kutumia ndege hiyo kubebea mkaa, mihogo na mikungu ya ndizi kinadhalilisha Ofisi ya Rais.
Katibu wa Wabunge wa CCM Zanzibar, Mbunge wa Magomeni, Mohammed Chombo alipoulizwa na gazeti hili kuhusiana na suala hilo alikiri wabunge hao kulifikisha suala hilo kwa Rais Shein.
“Tulimweleza Rais matatizo mengi likiwamo na hilo la Makamu wa Kwanza wa Rais kutumia ndege ya Serikali kubebea mihogo na mkaa,” alisema.
Alisema kuwa Rais aliwaambia kuwa ameyapokea malalamiko hayo na kwamba atayafanyia kazi.
Chombo alisema kuwa kwa sasa wanamsubiri Rais Shein awaite kuwapa majibu ya matatizo yao.
Baadhi ya wabunge wa CCM Zanzibar ambao walizungumza na gazeti hili, walisema kuwa kitendo hicho ni matumizi mabaya ya mali za umma kwa sababu kuna vyombo vingi vya usafiri vinavyoweza kutumika kusafirishia mizigo hiyo.
Ofisa mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake kutoka Mamlaka ya Ndege za Serikali, akizungumzia utaratibu wa viongozi wa Serikali kutumia ndege hizo, alisema viongozi wa juu wa Serikali ya Muungano na Zanzibar hukodi ndege zao.
Alisema hajawahi kuona ndege kubebea mkaa, hata ndege ya jeshi hajawahi kuona ikibeba mkaa.
Hata hivyo, Katibu wa Wabunge wa CUF, Mohammed Habibu Mnyaa, alisema madai hayo ya wabunge wa CCM ni siasa chafu dhidi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na kwamba wao wanaamini hawezi kufanya jambo hilo.
Alisema Maalim Seif anaheshimika na ni mzoefu katika utawala hawezi kufanya jambo hilo, wakati kuna meli ambazo zinaweza kutumika kusafirishia bidhaa hizo kutoka Pemba kama akitaka.
“Hizi ni siasa chafu za wabunge wa CCM dhidi ya Maalim Seif, sisi tunaamini hawezi kufanya jambo hilo hata kidogo,” alisema Mnyaa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Fereji alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, alisema hana taarifa na madai hayo.
“Sina taarifa na yoyote, ndiyo kwanza nayasikia kutoka kwako,” alisema.
Kaimu Katibu Mkuu wa CUF Taifa, Julius Mtatiro alipoulizwa jana kuhusiana na suala hilo alisema kuwa Maalim Seif yuko nje ya nchi, hata hivyo msimamo wa chama hicho ni kwamba madai hayo ya wabunge wa CCM siyo ya kweli.
Alisema kuwa wamesikia kikao cha Wabunge wa CCM na Rais Shein, kwamba wanachokidai kinaonyesha wazi kuwa wamekosa cha kuwafanyia wananchi wao.
Mtatiro alisema hii siyo mara ya kwanza kwa viongozi wa CCM kumtungia tuhuma Maalim Seif, kwani waliwahi kudai kuwa ni mwasisi wa Kikundi cha Kiislamu cha Uamsho jambo ambalo siyo la kweli.
“Pia viongozi haohao wa CCM waliwahi kumtupia tuhuma nyingi ambazo baadaye zinakuja kuonekana siyo za kweli,” alisema.
Alisema hata kama Maalim Seif angetumia hiyo ndege kubebea zawadi kwani kuna ubaya gani, mbona hata viongozi wa CCM hufanya hivyo?
“Kuna ubaya gani, viongozi wa kitaifa kubebea zawadi, mbona hata viongozi wa CCM wakiwa katika ziara wakipewa zawadi hubeba kwenye ndege?”
Huu ni msukosuko mwingine katika serikali ya umoja wa kitaifa. Hivi karibuni Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, iliingia kwenye msukosuko baada ya viongozi wake kutofautiana kuhusu muundo wa Muungano. Maalim Seif aliwahi kunukuliwa akisema anataka serikali ya mkataba, kauli ambayo ilipingwa na viongozi wengine hususan kutoka CCM.
Wakati makamu huyo wa kwanza akisema hivyo, Rais Shein alisikika akisema anataka muundo wa sasa wa serikali mbili. Hata hivyo, wiki iliyopita Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema kuwa mwarobani wa Muungano ni kuwa na serikali tatu.
CHANZO MWANANCHI

No comments:

Post a Comment