Pages

Wednesday, August 21, 2013

UJUMBE WA MSANII FEROUZ KWA WASANII WAKUBWA, PIA AFUNGUKA KUHUSU ISHU YA YEYE KUA KIMYA


ferouz
AMECHEKI kwa umakini na amekubali kweli chipukizi wa siku hizi wanawakimbiza wakongwe kinoma. Lakini msanii wa Bongo Fleva, Ferouz Mrisho, amewataka wakongwe hao wasikatishwe tamaa na chipukizi, badala yake wajipange kutawala chati.
Ferouz ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wa ‘Ndege Mtini’ aliouimba kwa mahadhi ya mnanda, anasema wakongwe hao wanapaswa kujipanga vyema kuweza kuukabili ushindani wa muziki uliopo hivi sasa.
“Kuna njia nyingi zinazoweza kutusaidia wakongwe turudi kwenye chati kama zamani, mimi nimekaa chini na kufikiria na hatimaye nimeamua kubadilisha staili ya uimbaji,” anasema.
“Nimelazimika kufanya hivi ili niweze kwenda na soko la mashabiki. Msanii lazima uendane na wakati, ujue ni kipi utakachoimba na ukiimbeje ili kuwakamata mashabiki.
“Staili ninayoimba sasa inanilipa kiukweli, ninapata shoo nyingi tu, mashabiki wananikubali japo wapo baadhi yao ambao wananiponda kwa hatua hii.
“Staili hii ninayoimba inaonyesha jinsi gani nilivyokuwa nina kipaji cha ziada kilichojificha.”
Atoboa siri ya ukimya wake
Ferouz anasema ukimya wake umetokana na kundi lake la Daz Nundaz kusambaratika licha ya ukweli kuwa tangu zamani alishakuwa akifanya kazi kivyake pia.
“Kundi lililoposambaratika nikaamua kukaa chini na kujipanga upya, kweli kuna kazi nilikuwa nikizifanya pembeni. Lakini suala la kundi lilinilazimisha kutafakari mambo kwa umakini na ndiyo maana nilitulia kwanza,” anasema.
Anaongeza: “Pia kuna suala la mkataba pale Bongo Records, ulikuwa umemalizika. Kama mnakumbuka asilimia kubwa ya nyimbo zangu kama ule wa ‘Starehe’ nilizirekodi pale. Kwa sasa ninarekodi sehemu nyingine.
“Unajua muziki unahitaji umakini mkubwa, ni tofauti na jinsi watu wanavyofikiria.”
Ferouz anaamini kuwa bado yupo katika chati za juu kimuziki Afrika Mashariki na anatarajia kupanda zaidi kutokana na mabadiliko ya uimbaji aliyoyafanya.
“Mnanda umeniimarishia makali, wimbo wangu wa ‘Ndege Mtini’ sasa unatumika hata katika simu, unanitengenezea kipato kizuri tu,” anasema.
 ferouz
Bado aiota albamu ya Safari
Anasema hawezi kusahau mafanikio ya albamu ya Safari iliyompa umaarufu mkubwa kuliko kazi alizofanya na kundi la Daz Nundaz.
“Albamu ile ilinipa mashabiki hasa kupitia wimbo ‘Starehe’, unajua wimbo ule nilitokea kuupenda hata kabla sijaurekodi na nilipofanya hivyo ndiyo ikawa balaa kwa mashabiki, yaani waliupenda hadi kunipa jina la ‘Ferouz Starehe’, ile ni alama ya ubora wangu,” anasema.
Amkubali Belle 9
Kuna wasanii wengi wenye kazi nzuri nyingi tu. Lakini anakiri kuvutiwa na umahiri wa Belle 9 wa Morogoro.
“Mwanzoni nilipoanza kuzifahamu kazi zake nilidhani hayupo makini, lakini muda ulivyozidi kwenda nikaanza kumwelewa na kumkubali. Huyu jamaa anajua kazi,” anakiri.
Katika anga la Afrika Mashariki anazikubali kazi za Jose Chameleon wa Uganda akisema hachuji kiusanii kutokana na kufahamu anachokifanya.
Kwenye soka pia yumo
Si mchezaji wa soka la ushindani kwenye timu kubwa, lakini anasema hutumia pia muda wake katika mchezo huo.
Mbali ya kucheza kwenye timu za mtaani, anasema yeye ni shabiki mkubwa wa Simba ya Dar es Salaam na kwa Ulaya hauwezi kumwambia kitu juu ya Manchester United ya Ligi Kuu England.
“Naupenda sana mpira wa miguu, nadhani kama si muziki na biashara ninazozifanya, soka ingeweza kuchukua nafasi kubwa,” anasema anayejiandaa kuachia kazi mpya kadhaa katika siku za karibuni.
“Sitazitaja kazi hizo, lakini mashabiki wajiandae kwa ‘sapraiz’ kali za ladha tofauti. Nina uhakika hawatachoka kuzisikiliza,” anasema.
Huyo ndiye Ferouz aliyewahi kutamba na nyimbo za ‘Boss’, ‘Nipe Tano’, ‘Starehe’, ‘Wema Umemponza’, ‘Jirushe’ pamoja na nyinginezo kadhaa.CHANZO FRESH 120MEDIA

No comments:

Post a Comment