Kijana Ramadhani Rajabu akionesha sehemu ambazo amenyofoka nyama kwa kemikali hizo.
Kijana Ramadhani Rajabu akionesha sehemu ambazo amenyofoka nyama kwa kemikali hizo.
Kijana Said Omari akionesha sehemu za vidole vyake vilivyoathirika kwa kemikali hizo
Na Mashaka Mhando,Handeni
VIJANA 12 wa kijiji cha Manga kilichopo kata ya Mkata wilayani hapa, wameanza kunyofoka nyama kutokana na madai ya kubeba magunia yenye kemikali baada ya lori lililokuwa limebeba mzigo huo, kupinduka katika eneo la dajani la kitongoji cha Tengwe kijijini.
Vijana hao wamepata athari hizo baada ya kupewa kibarua cha muda mfupi wa kubeba maguni yaliyokuwa na uzito wa kilo 25 kuyafaulisha kwenye gari jingine na kulipwa ujira wa sh. 95,000 ambazo waligawana sh. 11,500 kila mmoja baada ya kumaliza kazi hiyo.
Ofisa Tarafa ya Mazingara Bw Hashim Msagati alisema kuwa tukio hilo limetokea Julai 26 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni katika eneo hilo baada ya lori lenye namba za usajili T 787 CBT lililokuwa na tela lenye namba T 101 BTB kupinduka kisha watu waliokuwa kwenye gari hilo, kuwapa kazi vijana hao kubeba mizigo hiyo.
Alisema lori linadaiwa kumilikiwa na kiwanda cha soda cha Bonite kilichopo mjini Moshi, lilipata ajali hiyo iliyothibitishwa na polisi wa kituo cha Mkata, lilikuwa likitokea Jijini Dar es salaam kwenda mkoani Kilimanjaro, likiwa limebeba mifuko yenye kemikali hizo.
Wakizungumza na gazeti hili, wakiwa nyumbani kwao katika kijiji hicho cha Manga, mmoja ya waathirika hao Bw. Said Omari alisema walipata kazi hiyo kutoka kwa mtu mmoja aliyekuwa na asili ya Kihindi kupakia mifuko hiyo bila kuelezwa kwamba kilichomo ndani yake ni madawa makali.
Aliwataja wenzake waliokuwa pamoja ni Omari Bahorela, Khatib Juma, kassim Bakari, Hamis Chilo, Ramadhani Rajab, Ramadhani Mbelwa na Omari Mbuji kutoka katika mji wa Manga na Lazaro Jackson, Aweso Mussa, Mkombozi Mussa na Mohamedi Shabani waliotokea kitongoji cha Tengwe.
Alisema baada ya kufika kwenye eneo hilo, walianza kubeba mizigo hiyo na kuipakia kwenye gari jingine lakini ghafla mwezao mmoja Kasimu alianza kuanguka chini akawa hawezi kusimama baada ya madawa hayo kuanza kumuunguza miguuni na kwenye shingo hatua ambayo walianza kuogopa kuendelea na zoezi hilo.
"Mwenzetu alipokuwa ameanguka chini akawa hawezi kuinuka huku akilia miguu kumchoma kwa ndani na huku akishindwa kuinuka pale chini, tulianza kuogopa tukamwagia maji tukazidisha maumivu, tulikataa kuendelea na zoezi lile lakini yule Mhindi akasema hapana endeleeni mifuko iliyobaki, vinginevyo hatatulipa," alisema Bw Said.
Alisema hata hivyo, waliendelea kubeba na walipomaliza wakalipwa fedha hiyo ingawa walikuwa wamekubaliana ujira wa sh. 100,000 wakapewa sh. 95,000, lakini mwenzao yule hakuweza kutembea hadi wakambeba pamoja na Mhindi huyo kumrudisha nyumbani kwao kisha wakaondoka kuendelea na safari.
Bw Said alisema kesho yake walianza kunyofoka nyama kila mmoja aliyebeba mizigo hiyo na ngozi kuwa nyeupe huku wakipata maumivu kwenye uti wa mgongo na maeneo mengine ya miili yao hatua ambayo wanashindwa kupata matibabu sahihi kutokana na kukosa fedha.
Akizungumzia zaidi tukio hilo Bw. Msagati alisema kuwa wamepeleka taarifa hizo kwa viongozi wa wilaya ili waweze kuchukua hatua ya kuwatafuta waliohusika kwa ajili ya kuwasaidia matibabu vijana hao na kusafisha eneo lililopata ajali hiyo amba[po wanahofu kwamba endapo mvua itanyesha, inaweza kusombwa na kuingia katika visima vya maji na kuleta madhara makubwa kwa jamii.
Mkuu wa wilaya ya Handeni, Bw Muhingo Rweyemamu alisema atafika katika kijiji hicho kuwatembelea vijana hao kisha kuona eneo lililopata ajali kabla ya kuchukua hatua nyingine.
No comments:
Post a Comment