Pages

Monday, September 30, 2013

CHANZO CHA AJALI ILIYOKATISHA UHAI WA DADA WA MBOWE CHATAJWA...


Majeruhi wa ajali hiyo, Zedii Mzuke  na mtoto wake wakiwa wamelazwa katika hospitali ya Magunga wilayani Korogwe kwa matibabu.
Familia ya Mwenyekiti Chadema Taifa, Freeman Mbowe, imepata pigo baada ya dada wa mwenyekiti huyo, Grace Mbowe, kufariki katika ajali ya gari.

Ajali hiyo ilitokea jana   katika eneo la Changa Kabuku, barabara ya Segera-Chalinze, ambapo gari lenye namba za usajili T 277 CAT aina ya Toyota Crester Saloon Gx 100, likitokea Tanga kwenda Dar es Salaam, liliacha njia na kupinduka.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, gari hilo lilikuwa limebeba watu watano, akiwemo Grace Mbowe na dereva aliyetambulika kwa jina la Ibrahim Mkindwa. 
Mashuhuda hao walidai chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari, uliosababisha tairi la nyuma upande wa kulia kupasuka. Hali  hiyo ilisababisha dereva kushindwa kumudu kona, hivyo kusababisha kupinduka na kuingia chini ya daraja.
Katibu wa Mbunge Mbowe, Richard Mtui, alithibitisha kutokea kwa msiba huo na kuongeza kuwa Chadema Hai imesitisha mikutano ya hadhara, kusubiri taratibu zingine.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa bado Polisi inaendelea na uchunguzi zaidi.
Massawe alitaja majeruhi watatu waliokuwa abiria katika gari hilo kuwa ni Ridhiwani Bakari (29), Zedii Mzuke (28) na mtoto  Mariam Ridhiwani (3), wote wafanyabiashara wa Msambweni mkoani Tanga.
Alisema miili ya marehemu na majeruhi, walipelekwa katika Hospitali ya Magunga Korogwe mkoani Tanga.
Kifo cha dada yake na Mbowe, kimetokea ikiwa ni siku chache  baada ya kuhama Chadema na kujiunga na  CCM.

No comments:

Post a Comment