Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu mtandao wa kijamii wa nchini Kenya ulioituhumu Serikali ya Tanzania.
(Picha na Hassan Silayo)
Na Fatma Salum
SERIKALI
ya Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu tuhuma mbalimbali dhidi yake
zilizotolewa na mtandao wa kijamii wa nchini Kenya ujulikanao kama www.standardmedia.co.ke
unaosadikika kuendeshwa na kampuni ya gazeti la The Standard la nchini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Serikali na
Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene , alisema mtandao huo
umeripoti kuwa Serikali ya Tanzania
imekataa kuiuzia Kenya gesi asili ya Songosongo jambo ambalo halina ukweli kwa kuwa gesi inayozalishwa hivi sasa bado haijafikia
kiasi cha kuweza kuuzwa nje ya nchi.
Mtandao huo pia umeripoti kuwa Serikali ya
Tanzania ilikataa viwanja vyake vya ndege vya kimataifa kutumiwa na ndege
zilizopaswa kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyata wakati wa
ajali ya moto iliyotokea kwenye uwanja huo hivi karibuni.
Mwambene alifafanua kuwa tuhuma hizo ni za
uongo kwani mara baada ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyata kuwaka moto, ndege
zilizotakiwa kutua uwanjani hapo ziliruhusiwa kutua kwenye viwanja vya ndege
vya Tanzania vya Julius Nyerere International Airport (JNIA) na Kilimanjaro International
Airport (KIA).
“Sio kweli hata kidogo kwamba Tanzania
ilikataa ndege za Kenya zisitue kwenye viwanja vyake kwa sababu uwanja wa Jomo
Kenyata ulipoungua ndege nyingi zilizopaswa kutua katika uwanja ule zilitua
kwenye viwanja vyetu na hii pia ilitokana na ukweli kwamba Tanzania na Kenya
zinachangia ndege nyingi za nje ya nchi.” Alisema Mwambene.
Aidha
Mwambene alikanusha tuhuma nyingine iliyodai kuwa mwaka 2010 Tanzania ilikataa
kuiuzia Kenya chakula badala yake ikaiuzia nchi ya Uganda taarifa ambazo si za
kweli kwa kuwa mwaka huo nchi nyingi za Afrika zilikumbwa na baa la njaa
ikiwemo Tanzania yenyewe.
Hivyo Tanzania ililazimika kusitisha utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara
kuuza chakula nje ya nchi na hakukuwa na taarifa yoyote ya kuuzwa chakula
nchini Uganda.
Kutokana na upotoshaji huo Mwambene alisema
Serikali ya Tanzania imeutaka mtandao huo kuomba radhi na isipofanya hivyo
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Katika hatua nyingine Mwambene alifafanua
kuwa zoezi linaloendelea nchini la kuwataka
wahamiaji haramu wanaoishi hapa kinyume cha utaratibu kuondoka kwa hiari haliwahusu
wakimbizi waliopo nchini kisheria.
Pia zoezi hilo linawalenga wahamiaji haramu
wote kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Congo DRC, Zambia na Uganda na hakuna
serikali ya nchi yoyote kati ya hizo iliyolalamika kuhusu hatua hiyo.
“Mpaka sasa zoezi linaenda vizuri hakuna
taarifa yoyote ya malalamiko kutoka Zambia, DRC, Burundi, Rwanda wala Uganda na
tayari Rwanda imetuma taarifa rasmi kuishukuru serikali ya Tanzania kwa
kuendesha vema zoezi hilo. Kinachoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari ni
upotoshaji unaolenga maslahi binafsi.”
Akizungumzia usalama wa Watanzania nchini
Rwanda, Mwambene alisema hakuna taarifa ya
Mtanzania yeyote kunyanyaswa nchini
humo na uhusiano wa kidiplomasia
kati ya Rwanda na Tanzania haujakatika.
No comments:
Post a Comment