Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, September 7, 2013

UMEWAHI KUONA MAZISHI YA KIRASTAFARI?KAMA BADO TAZAMA HAPA

Mayasa Mariwata na Denis Mtima

MAZISHI ya rasta mmoja maarufu kwa jina la Rasta Gido aliyekuwa dereva wa bodaboda yameonekana kushika nafasi ya juu katika rekodi ya marehemui wote waliozikwa Ifakara, Morogoro miaka ya karibuni.

Rasta Gido alipata ajali mbaya ya kugongwa na gari aina ya Fuso, Julai 28, mwaka huu eneo la Ifakara Kibaoni.

Aliaga dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mtakatifu Francisca ya mjini Ifakara.

Akizungumza na waandishi wetu juzi, jijini Dar baada ya kurejea kutoka kwenye msiba huo, mjomba wa marehemu aitwaye Avi Simba alisema msiba huo uliongozwa kwa imani ya kirasta bila kuhusisha mchungaji wala shehe huku waombolezaji wakivalia kofia za kirasta zenye rangi za kijani, nyekundu, njano na nyeusi hali iliyozidisha kuyafanya mazishi hayo kuwa ya aina yake.

Mbali na kofia hizo, jeneza la marehemu lilipakwa rangi hizo za kirasta zilizotajwa hapo juu, hivyo kulifanya eneo lote la msiba kutawaliwa na taratibu za kirasta.

“Mimi na ndugu zangu wote tulikaa chini na kukubaliana kuwa marehemu azikwe kwa imani ya kirasta bila kufuata taratibu za dini yoyote ile,” alisema mjomba huyo wa marehemu.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya wananchi waliohudhuria msiba huo walijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na utaratibu wa mazishi uliowekwa na ndugu na jamaa wa marehemu ambao ni jamii ya rasta tofauti na taratibu za dini yake aliyokulia Rasta Gido ya Romani Katoliki.

Hali iliyoongeza mazishi hayo kuwa ya aina yake ni Wazungu waliofika msibani hapo sanjari na mwongozaji wa mazishi hayo, Rasta Side ambaye ni mchumba wa mmoja wa Wazungu hao.

Mbali na hayo yote, kwenye mazishi, hakukutumika machepe na majembe kufukia kaburi la marehemu huyo badala yake ilitumika mikono kufanya kazi hiyo mwanzo hadi mwisho.

Kutokana na msiba huo, madereva wa bodaboda wa eneo la Kibaoni waliamua kusitisha shughuli zao ili kuungana na mwenzao katika safari yake ya mwisho.

Madereva hao walimlaani vikali dereva wa Fuso aliyemgonga Rasta Gido wakidai kuwa hakuwa makini barabarani na kusababisha ajali hiyo mbaya.

Nayo familia ya marehemu ilijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na jukumu zito la malezi alilowaachia rasta huyo kwani ameacha watoto watatu, Rose, Neema na Stanislaus ambao wote bado wanahitaji msaada.

Marehemu Rasta Gido alizikwa kwenye makaburi ya familia ya Kibaoni, Ifakara mkoani Morogoro.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Ameni.

No comments:

Post a Comment