Muswada
wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013 uliokuwa ujadiliwe katika
mkutano wa 12 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma, umeondolewa na sasa
utajadiliwa Bunge lijalo.
Habari za
uhakika zilizopatikana jana, zilisema kwamba kuahirishwa huko
kumetokana na wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge
wanaotoka Zanzibar kupinga vikali kura ya maoni kupigwa visiwani humo
kwa kuwa tayari huko kuna sheria hiyo.
Muswada
huo ulikuwa ujadiliwe na wabunge katika kikao cha Bunge kinachoendelea
ukitanguliwa na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya mabadiliko
ya Katiba wa mwaka 2013.
hdg
"Ukisoma
huu Muswada unasema kura hiyo itapigwa Tanzania Bara na Zanzibar sasa
sheria hii ina apply vipi (inatumikaje) Zanzibar wakati kule tuna sheria
yetu tayari?" alihoji Mbunge mmoja wa Zanzibar.
Kaimu
Katibu wa Bunge, John Joel alipoulizwa jana, alithibitisha kuondolewa
kwa muswada huo wa kura ya maoni kusema na utakaojadiliwa ni ule wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pekee.
"Bunge
litaahirishwa Ijumaa (keshokutwa) na ni kweli huo Muswada wa Kura ya
Maoni umeondolewa kwa sababu bado uko kwenye ngazi ya kamati," alisema
Joel.
Alipoulizwa
sababu za kuondolewa kwa muswada ambao ulishaingizwa kwenye ratiba ya
Bunge, alitaka swali hilo aulizwe Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Waziri Lukuvi alithibitisha kuondolewa kwa muswada huo na kusema utajadiliwa katika Mkutano wa Bunge wa Oktoba.
"Ni kweli
muswada huu hautajadiliwa na Bunge hili bado kuna mashauriano
yanaendelea kati ya SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," alisema.
Kwa
upande wake, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu
Lissu alisema wabunge wa Zanzibar ndiyo waliokwamisha muswada huo
kutokana na mgongano wa sheria.
"Wao
wanasema masuala ya kura ya maoni siyo ya Muungano kwa sababu wao tayari
wana sheria yao ya kura ya maoni. Sasa wanahoji inakuwaje sheria hii
itumike tena hadi Zanzibar? Huu ni mgongano," alisema.
Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema tangu
mwanzo aliliona suala hilo na kuitahadharisha Kamati ya Bunge kwamba
mapendekezo hayo yana upungufu.Muswada pekee uliobaki wa Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba unatarajiwa kuwasilishwa leo huku
ukitarajiwa kuibua mjadala mzito kutokana na misimamo ya baadhi ya
wabunge.
Muswada huo unawasilishwa wakati CCM kikiwa kimeweka msimamo wa kupinga baadhi ya mambo katika Rasimu ya Katiba.
Yanayotarajiwa kuzua mjadala
Waziri wa
Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amekiri kupokea mapendekezo kutoka
kwa wabunge na hasa kwenye Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba
akisema wametaka kuangaliwa upya kwa kipengele cha Kamati ya Uteuzi ya
viongozi wa Bunge la Katiba. Alisema sasa wataweka sifa za mwombaji wa
nafasi hizo na wasiokuwa nazo hawatagombea.
Muswada
wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba unataka wawakilishi kutoka makundi ya
jamii kuwa 166 katika Bunge la Katiba, lakini wabunge wanataka idadi iwe
200.
Mbunge wa
Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisema uzoefu katika nchi
nyingine unaonyesha kuwa mabunge ya Katiba hushirikisha watu wengi ili
kupata uwakilishi mpana tofauti na mapendekezo yaliyotolewa.
Mkosamali
ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala, alisema ni vyema sheria ikasema wajumbe wa Bunge hilo watatoka
katika taasisi zipi.
Kifungu
kingine ni kile kinachohusu Kamati ya Uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu
wake ambao kwa mujibu wa muswada itaundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri
na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (AG) na yule wa SMZ, Waziri wa Katiba na
Sheria Tanzania Bara na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar na
Kiongozi Rasmi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Mkosamali
alisema muswada huo wa Mabadiliko ya Katiba unasema mwenyekiti wa muda
atakuwa Spika wa Bunge lakini akataka: "Mwenyekiti wa muda atokane na
Chama cha Majaji wastaafu maana wao hawafungamani na upande wowote."
:CHANZO MWANANCHI.
:CHANZO MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment