Pages

Wednesday, October 16, 2013

HATIMAYE BABA ALIYETELEKEZA WATOTO AKAMATWA.


Watoto  Agustino Steven (8) na Rebeka Steven(7) wakifanya usafi katika nyumba wanayoishi 
Hapa ndipo wanapopikia chakula wakati wa usiku  kwakweli ni hali ya hatari sana
Mwandishi wa Mbeya yetu Joseph Mwaisango akiwa na watoto hao alipowatembelea nyumbani mara baada ya kuwakosa shuleni mwandishi wetu alipowauliza kwanini hamjaenda shule leo? wakamjibu tulijua leo ni sikukuu ndiyo maana hatujaenda shule,
Hapa wakinawa kutokana na hali ya uchafu waliokuwanayo baada ya kumaliza kufanya usafi nyumba yao
Wakiwa na waalimu wao
Hapa mwandishi wetu Joseph Mwaisango akiwarudisha nyumbani watoto hao mara baada ya maongezi mafupi na waalimu wao

JESHI la Polisi Mkoani Mbeya linamshikilia Steven Julias mkazi wa Jakaranda kata ya Iyela Jijini Mbeya akituhumiwa kutelekeza familia kwa miezi mitano bila huduma za msingi ikiwemo chakula na sare za shule.

Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kumethibitishwa na mwenyekiti wa dawati la Jinsia Mkoa wa Mbeya, Mary Gumbo ambaye alisema walimkamata Oktoba 11, mwaka huu eneo la nyumbani kwake alikokuwa amewatelekeza watoto hao.

Aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa anafanya maandalizi ya kuwatorosha watoto hao ili kukwepa mkono wa sheria dhidi yake baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa anatafutwa kukabili kesi iliyombele yake.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo alisema hivi sasa uchunguzi unafanyika ili kesi iweze kufunguliwa na hatimaye kufikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake ili vitendo vya unyanyasaji dhidi ya watoto vikomeshwe.

Wakati huo huo maisha wanayoishi kwa sasa watoto hao  Agustino Steven (8) na Rebeka Steven(7) ambao ni wanafunzi wa darasa la kwanza  shule ya msingi Mapambano iliyopo Kata ya Iyela Jijini Mbeya maisha ya kujipikia bila huduma za msingi wasamaria wema wameombwa msaada wao wa hali na mali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti watoto hao wamesema hivi sasa wanaishi kwa misaada kutoka kwa walimu na baadhi ya watu ambao huwapa unga na maharage na wao hulazimika kutafuta fedha za kununulia mahitaji mengine kama mafuta ya kula na taa.

Wametaja baadhi ya mahitaji yao muhimu kwa sasa kuwa ni pamoja na Sare za shule kutokana na kuchakaa kwa sare wanazotumia ikiwemo Madaftari, kalamu,Masweta, Viatu, mafuta ya kupikia, mafuta ya kupaka, sabuni, chumvi, mkaa, Unga, Mchele na maharage.

Aidha imeshauriwa kuwa kutokana na mazingira wanayoishi watoto hao kutokuwa mazuri kwa utunzaji wa vyakula ambapo nyumba wanayoishi kutokuwa na mlango vitu hivyo vihifadhiwe Ofisini Kwa Mwalim Mkuu kama vitapatikana.

Kwa yeyote atakayekuwa ameguswa na hali ya watoto hao awasiliane na Mbeya yetu kupitia namba 0754374408
 au Bomba fm redio kupitia 0754 490752.

Na Mbeya yetu

No comments:

Post a Comment