Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine
Massawe alisema jana kwenye eneo la tukio kuwa, polisi waliwakabili
watu hao kwa bunduki baada ya kuonyesha nia ya kutaka kuwadhuru askari
walipokuwa kazini.
Massawe alisema tukio hilo limetokea wakati polisi
walipokwenda Kijiji cha Kimamba kuwakamata washukiwa wa mauaji ya
mgambo Salum Mgonje, wiki iliyopita.
Mgambo huyo aliuawa na wananchi ambao wengi ni
wafanyabiashara waliokuwa wakipinga kutozwa ushuru wa mazao. Kutokana
na mauaji hayo askari hao walifanya operesheni maalumu kusaka washukiwa
wa mauaji yaliyotekelezwa Kijiji cha Lulago, Kata ya Lwande, wilayani
hapa.
Katika vurugu hizo, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha
Songe, Edward Lusekelo alijeruhiwa kwa risasi. Mpaka sasa, wanavijiji 44
wa kata za Lwande na Negero wakiwamo wanawake na watoto wanashikiliwa
na polisi. Akitoa maelezo ya mkasa huo wa Ijumaa iliyopita, Mkuu wa Mkoa
wa Tanga, Chiku Galawa alisema hali kwenye vijiji hivyo imetulia.
Galawa aliwataja wanavijiji waliouawa katika
mapambano hayo kuwa, ni Hamis Ramadhan mkazi wa Kijiji cha Negero na
mfanyabiashara wa madini na ambaye hajatambuliwa ingawa ilielezwa kuwa
alikuwa Imamu wa Msikiti na Mwalimu wa Madrasa katika msikiti uliopo
Kitongoji cha Madina, Kijiji cha Kimamba, Kata ya Negero.
Gallawa alisema katika operesheni hiyo askari na
wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tanga, walikwenda vijiji
mbalimbali na kukuta watu wengi wamekimbilia msituni kujificha vurugu.
“Katika operesheni hii, tulikwenda msituni na
tukabaini vitongoji ambavyo walikuwa wakiishi Waislamu hawa wenye siasa
kali, ambao kutokana na taarifa za kijijini walikuwa washukiwa wa vurugu
zilizotokea na kusababisha mauaji ya mgambo na kujeruhiwa kwa Mkuu wa
Kituo cha Polisi cha Songe,” alisema.
Alitaja vitongoji ambavyo walivibaini kuwa ni
Lulago, Kata ya Lwande na kingine cha Madina, Kijiji cha Kimambo, Kata
ya Negero, ambako wamekamata bunduki nne aina ya magobore, bastola
mbili zilizotongenezwa kienyeji, mapanga 18, shoka mbili , visu 10,
madaftari yaliyokuwa yakitumika kufundishia madrasa na vitabu vya dini
ya Kiislamu.
Gallawa alisema baadhi yao wakiwamo wanawake na
watoto, wamechukuliwa ili kuhifadhiwa hadi hasira za wanavijiji
itakapopungua kwa kuwa wamekataliwa kupokewa na ndugu zao kutokana na
kile kilichoelezwa kuwa, walikuwa wakiendesha dini kwa siasa na
kusababisha mateso kwa wanavijiji wasio wafuasi wa itikadi hiyo.
“Ifahamike hawa tunaowashikilia hakuna
atakayeonewa wala kubambikwa makosa, ila kinachofanyika ni kuwachuja
wahusikana,” alisema.CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment