JESHI la Polisi mkoani Iringa limemtia mbaroni
mkazi wa Nyololo Wilaya ya Mufindi, Gwelino Mtonyole maarufu kama ‘Rais wa
Nyololo’ kwa tuhuma za kufanya unyang’anyi wa kutumia silaha na utekaji wa lori
la mafuta.
Mtonyole anatuhumiwa kushiriki kuliteka lori aina
ya Scania lililokuwa likisafirisha mafuta aina ya dizeli kutoka Dar es Salaam
kwenda Ndola, Zambia mali ya kampuni ya E. Awadh. Co. Ltd.
Mtuhumiwa huyo na wenzake waliliteka gari hilo
baada ya dereva kuteremka kwa lengo la kuangalia hitilafu zilizokuwa
zikijitokeza na kusababisha kufuka moshi katika injini.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ramadhani Mungi
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo maeneo ya Igumbilo, Septemba mwaka
huu katika barabara ya Iringa - Dar es Salaam.
Alisema kuwa watu wanane walimvamia dereva na
utingo wake na kisha kumfunga kamba miguuni, kitambaa usoni na kumweka vitambaa
mdomoni kisha kumtelekeza katika pagale.
Mungi alisema harakati za kumsaka kiongozi huyo wa
shughuli za utekaji wa magari mkoani Iringa, zilifanikiwa baada ya gari hilo
kukutwa likiwa limetelekezwa Makambako huku mapipa 15 ya mafuta aina ya dizeli
yakikutwa nyumbani kwake.
Mungi alisema Jeshi la Polisi linawasaka watu saba
wanaodhaniwa kuwamo katika mtandao huo ili kudhibiti tabia za utekaji wa magari
na kwamba tukio hilo ni la pili kutokea katika kipindi cha mwezi mmoja.
Alisema kuwa dereva wa lori hilo lenye namba za
usajili T 945 CAS na tela lake lenye namba T 215 CFQ alijulikana kwa jina la
Hassan Mapili (38).
Kamanda alifafanua kuwa mtuhumiwa huyo wakati
anakamatwa nyumbani kwake Nyololo, alikutwa na zaidi ya lita 4,000 za mafuta ya
dizeli zikiwa zimehifadhiwa katika madumu makubwa.
Alisema lori hilo hadi linapatikana Makambako,
mkoani Njombe lilikuwa limebakia na lita 6,000 kati ya 36,000 za mafuta
yaliyokuwa yamebebwa.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment