Pages

Thursday, October 10, 2013

Polisi wamnasa jambazi anayejiita ‘Rais wa Nyololo’

 
JESHI la Polisi mkoani Iringa limemtia mbaroni mkazi wa Nyololo Wilaya ya Mufindi, Gwelino Mtonyole maarufu kama ‘Rais wa Nyololo’ kwa tuhuma za kufanya unyang’anyi wa kutumia silaha na utekaji wa lori la mafuta.
Mtonyole anatuhumiwa kushiriki kuliteka lori aina ya Scania lililokuwa likisafirisha mafuta aina ya dizeli kutoka Dar es Salaam kwenda Ndola, Zambia mali ya kampuni ya E. Awadh. Co. Ltd.
Mtuhumiwa huyo na wenzake waliliteka gari hilo baada ya dereva kuteremka kwa lengo la kuangalia hitilafu zilizokuwa zikijitokeza na kusababisha kufuka moshi katika injini.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ramadhani Mungi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo maeneo ya Igumbilo, Septemba mwaka huu katika barabara ya Iringa - Dar es Salaam.
Alisema kuwa watu wanane walimvamia dereva na utingo wake na kisha kumfunga kamba miguuni, kitambaa usoni na kumweka vitambaa mdomoni kisha kumtelekeza katika pagale.
Mungi alisema harakati za kumsaka kiongozi huyo wa shughuli za utekaji wa magari mkoani Iringa, zilifanikiwa baada ya gari hilo kukutwa likiwa limetelekezwa Makambako huku mapipa 15 ya mafuta aina ya dizeli yakikutwa nyumbani kwake.
Mungi alisema Jeshi la Polisi linawasaka watu saba wanaodhaniwa kuwamo katika mtandao huo ili kudhibiti tabia za utekaji wa magari na kwamba tukio hilo ni la pili kutokea katika kipindi cha mwezi mmoja.
Alisema kuwa dereva wa lori hilo lenye namba za usajili T 945 CAS na tela lake lenye namba T 215 CFQ alijulikana kwa jina la Hassan Mapili (38).
Kamanda alifafanua kuwa mtuhumiwa huyo wakati anakamatwa nyumbani kwake Nyololo, alikutwa na zaidi ya lita 4,000 za mafuta ya dizeli zikiwa zimehifadhiwa katika madumu makubwa.
Alisema lori hilo hadi linapatikana Makambako, mkoani Njombe lilikuwa limebakia na lita 6,000 kati ya 36,000 za mafuta yaliyokuwa yamebebwa.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment