Kutokana
na taarifa zilizotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya hesabu za
Serikali kuwa vyama vya siasa ambavyo vinapata ruzuku kutoka serikalini
havijawasilisha taarifa yake ya mapato na matumizi kwa ajili ya
kufanyiwa ukaguzi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa
kipindi cha miaka minne mfululizo, yaani kuanzia mwaka 2009/2010-
2012/2013.
CHADEMA tunapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo juu ya taarifa hizo;
i. Kuwa taarifa hizo sio sahihi na hazina ukweli kuhusiana na CHADEMA
labda kwa vyama vingine, hii ni kutokana na ukweli kuwa
tulishawasilisha taarifa zetu za fedha kwa msajili wa vyama vya siasa na
zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha 2010/2011, 2011/2012 na hili
linathibitishwa na barua ya msajili wa vyama vya siasa yenye Kumb.Na.
CDA.112/123/01a/37, ya tarehe 04 september 2012. Iliyopelekwa kwa
makatibu wakuu wa vyama vyote vya siasa (nakala imeambatanishwa).
Aidha, hesabu za mwaka wa fedha zilizokaguliwa za 2009/2010,
tuliziwasilisha kwa Msajili wa vyama vya siasa kwa barua yenye Kumb.Na.
C/HQ/ADM/MSJ/04/71 ya tarehe 27 Octoba, 2011. (Nakala ya barua
imeambatanishwa).
ii. Kuhusu taarifa ya fedha iliyokaguliwa kwa mwaka huu wa
fedha 2012/2013, bado haijawasilishwa kwenye ofisi za msajili wa vyama
kutokana na barua ya msajili wa vyama vya siasa ya Novemba 26, 2012
yenye Kumb.Na.DA.112/123/16A/97 ambayo ilikuwa na maelekezo kuhusu
ukaguzi wa mahesabu ya vyama vya siasa, iliyokuwa inajibu barua
tuliyomwandikia tukitaka kupata ufafanuzi kuhusu ukaguzi wa hesabu za
chama kutakiwa kufanywa na CAG na alitujibu kuwa “tumefanya mawasiliano
na Mkaguzi na Mdhibiti wa Mahesabu ya Serikali (CAG) kwa ufafanuzi wa
jambo hili na tutawafahamisha ipasavyo kuhusu malipo/gharama mliyotakiwa
kulipa katika ukaguzi wa Mahesabu hayo”; mpaka leo hatujawahi kupata
ufafanuzi huo pamoja na ukweli kuwa tumeshafunga hesabu zetu za mwaka
kama chama (barua imeambatanishwa).
iii. Kuhusu taarifa ya fedha kutoka nje ya nchi, CHADEMA tumekuwa
tukiwasilisha taarifa zetu kila mara tunapopata fedha kwa ajili ya
mafunzo na programu nyingine mbalimbali za chama kama ambavyo msajili
alituandikia barua tarehe 19 Agosti 2013 yenye Kumb.
Na.DA.112/123/16a/10 iliyokuwa ni taarifa ya mapato yatokanayo na
michango au misaada toka nje ya nchi, alisema “tunashukuru kwa taarifa
hii ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya vyama vya siasa”
(imeambatanishwa barua husika).
iv. Kuhusu Taarifa za gharama za uchaguzi kwa mwaka 2010 ,
tuliwasilisha taarifa hiyo na Msajili alikiri kuwa ni vyama viwili tu
ndiyo vilikidhi utekelezaji wa sheria ya gharama za uchaguzi kwa ukaguzi
wa marejesho, hii inathibitishwa na barua ya Msajili yenye Kumb.Na.
CDB.173/205/01/23 ya tarehe 16 April, 2012. (Nakala imeambatanishwa).
Tunapenda kuwahakikishia watanzania kuwa CHADEMA ndiyo ambayo tulidai
CAG awe na mamlaka ya kukagua fedha za vyama vya siasa ili taarifa zake
ziwekwe hadharani na tutaendelea kutoa ushirikiano kama ambavyo
tumekuwa tukifanya siku zote, kuhakikisha sheria hii inatekelezwa
ipasavyo kuhakikisha uwazi kwenye mapato na matumizi ya vyama vya siasa.
Aidha, kama ambavyo siku zote tumesimamia na kusisitiza, tunamtaka
CAG akague fedha zote za vyama na sio ruzuku tu kama ambavyo kamati ya
Bunge inataka iwe.
Imetolewa leo Alhamis, Oktoba 17, 2013;
……………………….
Antony C. Komu
Katibu wa Baraza la Wadhamini.
No comments:
Post a Comment