Tanzania
imesema itatoa msimamo wake wiki hii kuhusu mkutano wakuu wa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ngazi ya marais,
uliotarajiwa kufanyika jana kujadili masuala yanayohusu maslahi ya nchi
zilizoko katika ukanda huo bila kushirikishwa.
Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta,mjini hapa jana kuwa
mkutano huo ulitarajiwa kufanyika nchini Rwanda juzi na kwamba
ungehusisha marais wa nchi za Rwanda, Paul Kagame; Rais wa Uganda,
Yoweri Museveni; Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais wa Burundi,
Pierre Nkurunziza.
Alisema
hayo alipokuwa akijibu swali la NIPASHE lililotaka kauli ya serikali
kuhusu uamuzi wa nchi hizo kuendeleza tabia yao ya kuitenga Tanzania
katika mikutano yao.
"Mkutano
wa Rwanda unafanyika leo ngazi ya marais. Tunasubiri kupata maazimio.
Tanzania itatoa msimamo wiki hii," alisema Waziri Sitta bila kutaka
kuingia kwa undani kuhusiana na suala hilo.
Mkutano
huo ni wa tatu kufanyika bila kuishirikisha Tanzania. Mara mbili
mfululizo, marais wa nchi hizo walikutana na kujadili mchakato wa
kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo, huku wakiitenga Tanzania.
Marais
Kenyata, Museveni na Kagame alikutana mara zote hizo bila kumualika Rais
Jakaya Kikwete.Kwenye vikao viwili vilivyofanyika nchini Uganda na
Kenya, viongozi hao walikubaliana kutekeleza kwa haraka miradi ya ujenzi
wa reli itakayounganisha nchi hizo na bomba la mafuta litakalojengwa
kuanzia Sudan Kusini hadi Mombasa na lingine kutoka Kenya hadi Rwanda.
Pia nchi
hizo zilitangaza kuanzia Januari Mosi, raia wao watembeleane bila kuwa
na hati za kusafiria, pia kuwa na viza moja kwa watalii.
Mkutano
wa Kenya ulioambatana na ufunguzi wa gati katika bandari ya Mombasa,
nchi za Burundi na Sudani Kusini zilialikwa na kuwakilishwa na mawaziri
wao waandamizi, lakini Tanzania haikualikwa.
Vile
vile, vyombo vya habari viliwakariri baadhi ya mawaziri wa nchi hizo
waliopewa jukumu la kusimamia makubaliano hayo, wakiyaeleza kuwa ni ya
jumuiya nzima na endapo Tanzania ikipenda kuingia itakaribishwa.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Tanzania ilionyesha wasiwasi wake juu
ya mwenendo wa nchi hizo.
Ilipinga
dalili zinazoonekana kwa nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kutumia jina
la EAC kuomba fedha au kugharimia miradi inayopaswa kuwa ya jumuiya.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Abdullah Juma Saadalla.
Alisema malalamiko hayo yalishawasilishwa pia katika kikao cha Baraza la Mawaziri wa EAC, kilichofanyika jijini Arusha.
Dk.
Saadalla alisema serikali imemtaka Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard
Sezibera, kutoa maelezo juu ya gharama ya miradi kadhaa inayoaminika
kuwa sehemu ya jumuiya hiyo. Pia alisema hatua zilizochukuliwa na nchi
hizo kwa kukubali kuanzisha utaratibu wa matumizi ya viza moja na
vitambulisho vya pamoja, ni mfano wa ubabe usiokidhi matakwa ya
kidemokrasia.
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema hivi
karibuni kuwa Tanzania ikibaini kuwapo haja ya kujitoa EAC itafuata
utaratibu kwa kulifikisha suala hilo bungeni ili wabunge waliamue.CHANZO NIPASHE
No comments:
Post a Comment