Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, November 29, 2013

Baregu aitahadharisha Chadema kuhusu Zitto




“Tuhuma zinazotolewa dhidi ya Zitto na wenzake kwamba wamenunuliwa na chama fulani cha siasa zinahitaji maelezo na vielelezo vya kina ili kuwaaminisha wengi. Nasema hivi kwa sababu historia yao inadhihirisha kuwa wana uchungu na chama chao. Chama kinachoongozwa kwa demokrasia na kinachotarajiwa kushika madaraka ya kuongoza nchi, lazima kionyeshe uwezo mkubwa wa kuvumiliana, kutafakari, kusamehe, kuaminiana na kujenga umoja wenye lengo la kuelekea kusudio lake.” Baregu  
Dar es Salaam. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu amewataka viongozi wa chama hicho kutafakari na kudhibiti madhara yanayoweza kukikumba hasa baada ya hatua yake ya hivi karibuni ya kumvua nyadhifa zote, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na wenzake wawili.
“Bahati nzuri wamevuliwa uongozi siyo uanachama, binafsi nadhani  viongozi wanatakiwa kutafakari na kudhibiti madhara zaidi kwa chama, wakishupaza shingo, lolote litakalotokea watakuwa ni sehemu ya lawama,” Profesa Baregu alisema Dar es Salaam jana.
Zitto, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba walivuliwa uongozi Novemba 22 mwaka huu, kwa tuhuma za kuandaa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013, uliolenga kufanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho kinyume na katiba, sheria na itifaki za chama.
Profesa Baregu alisema pamoja na viongozi hao kuvuliwa madaraka, mema waliyokifanyia chama hicho hayawezi kuyeyuka na kwamba makosa yao yasikuzwe kiasi cha kufuta mazuri yao katika kujenga chama hicho.
“Ni vigumu kuamini kwamba makosa ya Zitto, Dk Kitila na Samson Mwigamba yanaweza kuyeyusha mema waliyokifanyia chama kama barafu inavyoyeyuka juani.”
Profesa Baregu ambaye alikuwapo katika kikao kilichowavua uongozi Zitto na wenzake alisema kinachotakiwa kufanyika sasa ni kujenga uhusiano ndani ya chama na hasa kipindi hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani ambao umeanza Novemba 22 na unatarajiwa kumalizika Juni mwakani.
Alitaka hatua dhidi yao zizingatie Katiba ya chama hicho ili kuhakikisha kuwa hazivurugwi na mamlaka nyingine zilizopo ndani ya Chadema akisema mkutano wa Baraza Kuu unaweza kubadili uamuzi wa Kamati Kuu.
“Kinachotakiwa kufanywa ni kuwatangazia wanachama misingi, taratibu na kanuni za kuzingatia katika harakati zao  ili kuondoa hali ya watu kufanya mambo kwa kificho,” alisema na kuongeza:
“Ni wazi wengi wapo katika kampeni, ichukuliwe kuwa walioshughulikiwa wamebambwa na iwe njia ya kuonyesha ukomavu katika kustahamiliana.”
Alisema asingependa kuona siasa za kulipizana visasi na kusisitiza kwamba hata kama mwanachama ana chuki binafsi na mwenzake, hatakiwi kutumia chuki hiyo kumhukumu.
“Tuhuma zinazotolewa dhidi ya Zitto na wenzake kwamba wamenunuliwa na chama fulani cha siasa zinahitaji maelezo na vielelezo vya kina ili kuwaaminisha wengi. Nasema hivi kwa sababu historia yao inadhihirisha kuwa wana uchungu na chama chao. Chama kinachoongozwa kwa demokrasia na kinachotarajiwa kushika madaraka ya kuongoza nchi, lazima kionyeshe uwezo mkubwa wa kuvumiliana, kutafakari, kusamehe, kuaminiana na kujenga umoja wenye lengo la kuelekea kusudio lake.”CHANZO MWANAINCHI
TUNAOMBA CLICK IYO LINK NA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGI NA UPDATES TOFAUTI TOFAUT

No comments:

Post a Comment