Pages

Monday, November 4, 2013

HALI YA MJUMBE WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA DOKTA MVUNGI INAENDELEA KUIMARIKA

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR – Mageuzi, JAMES MBATIA amesema, hali ya Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, DK, SENGONDO MVUNGI aliyevamiwa na watu wanaodaiwa kuwa Majambazi nyumbani kwake Kibamba, Dar es salaam, inaendelea kuimarika ingawa bado fahamu zake hazijarejea.
Akifafanua zaidi kuhusiana na hali ya DK. MVUNGI aliyelazwa katika Kitengo cha Taasisi ya Mifupa (MOI), MBATIA amesema kwa sasa Madaktari wa Kitengo hicho wanaendelea na juhudi za kumhudumia kuhakikisha hali yake inaimarika zaidi.
Aidha MBATIA amewaomba Watanzania kuendelea kumwombea DK. MVUNGI, huku akiwashukuru watu mbalimbali waliofika na wanaoendelea kufika Hospitalini hapo kumjulia hali, akiwemo Rais JAKAYA KIKWETE pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali.
Kwa upande wake Msemaji wa MOI, ALMAS JUMAA amesema, pamoja na hali ya DK. MVUNGI kuendelea kuimarika bado wanasubiri taarifa maalumu kutoka kwa Madaktari wanaomhudumia, ili kujua ukubwa wa tatizo baada ya kujeruhiwa vibaya katika tukio la kuvamiwa na kushambuliwa na Watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi.
DK. SENGONDO MVUNGI alijeruhiwa vibaya kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na Watu wanaodhaniwa kuwa Majambazi usiku wa kuamkia jana Nyumbani kwake Kibamba, Manispaa ya Kinondoni, Jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment