I: UTANGULIZI
a) Masuala ya Jumla
Mheshimiwa Spika,
1. Leo
tunahitimisha shughuli za Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge lako
Tukufu. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema
kwa kutufikisha salama siku ya leo.
Mheshimiwa Spika,
2. Mkutano huu ulijumuisha kazi kubwa zifuatazo:
Kwanza: Kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2014/2015;
Pili: Kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2013, [The Written Laws (Miscellaneous Amendments (No. 3) Bill 2013];
Tatu: Kujadili Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Akiba wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu wa Mwaka 2013 [The GEPF Retirement Benefit Bill, 2013]; na
Nne: Kujadili Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (The Constitutional Review Act) sura ya 83.
3. Nitumie
nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika
Kamati ya Mipango hapa Bungeni kwa kujadili kwa kina mapendekezo
yaliyowasilishwa na Serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
mwaka 2014/2015. Napenda kuwahakikishia kuwa, maoni na ushauri kama
yalivyotolewa na Waheshimiwa Wabunge yatazingatiwa na Serikali kila moja
kwa uzito wake wakati wa maandalizi ya Bajeti ya 2014/2015. Vilevile
niwashukuru kwa kujadili na kupitisha Muswada wa Sheria ya Mfuko wa
Akiba wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu.
b) Maswali
Mheshimiwa Spika,
4. Pamoja
na kukamilisha kazi hizo muhimu, pia katika Mkutano huu, jumla ya
maswali 120 ya msingi na 305 ya nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge
yalijibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 6 ya msingi na 6 ya nyongeza
yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
c) Kauli za Mawaziri/Maazimio
Mheshimiwa Spika,
5. Mkutano huu pamoja na kazi za msingi zilizopangwa, Waheshimiwa Wabunge walipata
fursa
ya kujadili Azimio la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu msimamo wake katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(d) Hotuba ya Mheshimiwa Rais,
Mheshimiwa Spika,
6. Katika
Mkutano huu pia, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kumsikiliza
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania akizungumza na Wananchi kupitia Bunge lako Tukufu.
Mtakubaliana nami kwamba hotuba ya Mheshimiwa Rais ilikuwa nzito na
yenye kuonesha umakini, umahiri na busara ambazo ni sifa mojawapo za
Rais wetu kati ya nyingi nzuri alizonazo. Tunachotakiwa ni kutumia
maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kuyafikisha kwa Wananchi katika maeneo
yetu ili nao waweze kuelewa hali halisi ya yanayotokea katika Jumuiya
yetu. Aidha, Hotuba ya Rais imegusa maeneo mengine ambayo sisi Wabunge
tunatakiwa kushirikiana na Wananchi katika kujipanga vizuri namna ya
kukabiliana na matatizo yaliyojitokeza.
II: UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2013/2014
(a) Mwenendo wa Mapato na Matumizi ya Serikali katika Robo ya Kwanza ya Mwaka 2013/2014
Mheshimiwa Spika,
7. Hotuba
yangu kwa leo imejikita zaidi kuelezea utekelezaji wa Mpango wa Bajeti
ya Mwaka 2013/2014 na maeneo machache katika Sekta ya Kilimo na Nishati.
Lakini kabla ya kuelezea mwenendo wa Mapato na Matumizi ya Serikali
katika Robo ya Kwanza ya mwaka 2013/2014, naomba kueleza kwa muhtasari
kuhusu mwenendo wa baadhi ya viashiria muhimu vya uchumi hususan Ukuaji
wa Uchumi na Mfumuko wa Bei. Taarifa za awali zilizotolewa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu zinaonesha kwamba Ukuaji wa Pato la Halisi la Taifa
katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2013, ulikuwa
Asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia 6.9 katika kipindi
kama hicho mwaka 2012. Sekta zilizoonesha kuwa na Viwango vikubwa vya
ukuaji ni pamoja na Sekta ya Mawasiliano na Usafirishaji ambayo imekua
kwa Asilimia 18.4, Sekta ya Fedha Asilimia 14.6 na Sekta ya Ujenzi
Asilimia 8.7.
Mheshimiwa Spika,
8. Kwa
upande wa Mfumuko wa Bei, takwimu zinaonesha kuwa kasi ya upandaji bei
imepungua kutoka Wastani wa Asilimia 13.5 Mwezi Septemba, 2012 hadi
Asilimia 6.1 Mwezi Septemba, 2013. Kushuka kwa Mfumuko wa Bei
kumechangiwa zaidi na upatikanaji wa chakula cha kutosha ndani ya Nchi.
Mwenendo huu mzuri wa viashiria vya uchumi jumla unatupa matumaini
makubwa kwamba jitihada za Serikali za kuimarisha usimamizi wa Uchumi na
kuleta Maendeleo endelevu ya Wananchi wetu zinaanza kuzaa matunda.
Mheshimiwa Spika,
9. Katika
Robo ya Kwanza ya mwaka 2013/2014 kuanzia Mwezi Julai hadi Septemba
2013, Mapato yote yaliyokusanywa na Hazina yalifikia Shilingi
Trilioni3.08; sawa na Asilimia 85.7 ya makadirio ya Shilingi
Trilioni 3.59. Pamoja na mwenendo huo wa ukusanyaji mapato, changamoto
kubwa zinazokabili eneo la Mapato ya Serikali ni kuchelewa kuanza kwa
wakati kwa ukusanyaji wa Mapato katika baadhi ya vyanzo vya mapato.
Changamoto nyingine ni Miundombinu isiyokidhi mahitaji ya usafirishaji
endelevu hasa reli ya kati, bandari, usafiri wa Anga na barabara.
Miundombinu Bora ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa Uchumi na Kukuza
Ajira; na hivyo kuiwezesha Serikali kukusanya mapato zaidi kutokana na
kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi. Serikali inafanyia kazi changamoto
hizo ili kuzipatia ufumbuzi mapema.
Mheshimiwa Spika,
10. Kwa
upande wa matumizi, hadi kufikia mwezi Septemba 2013; matumizi
yalifikia Shilingi Bilioni 3,806.5, sawa na Asilimia 98.5 ya lengo la
kutumia Shilingi Bilioni 3,854.2. Kati ya matumizi hayo, Shilingi
Bilioni 3,058 ni Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni 747.9 ni
Matumizi ya Maendeleo. Katika kipindi hiki, sehemu kubwa ya matumizi ya
Serikali ya Kawaida na Maendeleo imeelekezwa katika maeneo yenye kuleta
ufanisi na tija kubwa kama vile kuboresha miundombinu yabarabara,
ambayo mgao wake ulikuwa Shilingi Bilioni 182.5 za Matumizi ya Kawaida
na Maendeleo, Sekta ya Elimu Shilingi Bilioni 229.2; Sekta ya Nishati,
Shilingi Bilioni 159.9; Sekta ya Kilimo Shilingi Bilioni 119.6 na Sekta
ya MajiShilingi Bilioni 51.3. Vilevile, Serikali
imelipa Mishahara ya Watumishi wa Umma kwa wakati. Changamoto kubwa
iliyopo kwenye matumizi ya Serikali ni kuwepo kwa mahitaji makubwa ya
matumizi yasiyowiana na mapato; jambo ambalo linailazimu Serikali kukopa
kutoka Mabenki ya Ndani. Serikali itaendelea kuoanisha Matumizi na
ukusanyaji wa Mapato, hasa yale ya ndani pamoja na kuzingatia viwango
vya Matumizi vilivyoidhinishwa na Bunge. Aidha, Serikali itaendelea
kuweka msisitizo wa kuelekeza Matumizi kwenye vipaumbele vilivyoainishwa
katika Bajeti ya Serikali ambavyo ni vyanzo muhimu vya kuongeza Mapato,
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini.
III: UTEKELEZAJI WA MFUMO MPYA WA TEKELEZA KWA MATOKEO MAKUBWA SASA (BIG RESULTS NOW - BRN)
(a) Muundo wa Mfumo
Mheshimiwa Spika,
11. Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa Serikali ilianzisha Mfumo mpya wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa au Big Results Now (BRN) ili
kuongeza ufanisi katika usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya
utekelezaji wa Mipango yetu ya Maendeleo, hususan, Mpango wa Maendeleo
wa Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016). Hatua hii ilichukuliwa baada
ya kuona namna Mfumo kama huo ulivyoziwezesha Nchi kadhaa, na hasa Nchi
ya Malaysia, kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kiuchumi na kijamii katika kipindi kifupi. Kwa ukumbusho tu, Mfumo huo unatekelezwa katika Maeneo Sita ya Matokeo muhimu Kitaifa (National Key Results Areas) katika awamu yake ya kwanza, ambayo ni Nishati ya Umeme; Uchukuzi; Kilimo; Elimu; Maji na Ukusanyaji wa Mapato;
Mheshimiwa Spika,
12. Katika
Hotuba yangu ya kuahirisha Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge, tarehe 6
Septemba 2013, nilitoa taarifa ya awali kuhusu utekelezaji wa Mfumo huu
Mpya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, 2013. Katika
taarifa hiyo, nilieleza kuwa tumepiga hatua za
kuridhisha katika uundaji wa Mfumo wa kuleta matokeo ya haraka, ikiwa
ni pamoja na kuanzisha na kuteua Uongozi wa juu wa Taasisi Maalum yaani "President’s Delivery Bureau (PDB)” inayomsaidia
Mheshimiwa Rais kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Miradi na Programu
zilizoainishwa. Hivi sasa zoezi la kuajiri Watumishi wa Taasisi ya "President’s Delivery Bureau” na Vitengo vya Wizara vya Ufuatiliaji yaani Ministerial Delivery Units (MDUs)
watakaochukua nafasi za Watumishi walioazimwa kutoka kwenye Wizara na
Taasisi mbalimbali za Serikali, Sekta Binafsi, na Asasi Zisizo za
Kiserikali ambao walikuwepo katika hatua zake za maandalizi limeanza.
Ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru wote waliotumika katika chombo
hiki tangu kilipoundwa kwa uzalendo na weledi waliouonesha katika
kipindi hiki cha mwanzo na cha mpito;
Mheshimiwa Spika,
13. Napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba hadi sasa vitengo vya ufuatiliaji
katika Wizara zote sita (6) zinazosimamia utekelezaji chini ya Mfumo huu
mpya vimeanzishwa na vinaandaa Taarifa za utekelezaji za kila wiki na
kila mwezi, na kuziwasilisha kwenye Chombo cha President’s Delivery Bureau.
Aidha, Kamati Maalum za kusimamia utekelezaji zinazoongozwa na Mawaziri
husika zinakutana kila mwezi kujadili mwenendo wa utekelezaji na
kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji.
Baraza la Kusimamia Mageuzi na Utekelezaji (Transformation and Delivery Council –
(TDC)) limeundwa na lilikutana tarehe 11 Oktoba, 2013. Katika Kikao
hicho, Baraza lilipokea na kujadili muhtasari wa Taarifa ya utekelezaji
wa Mfumo mpya wa Kusimamia, Kufuatilia na Kutathmini Miradi ya
Kipaumbele katika Maeneo Sita ya Matokeo ya Kitaifa. Baraza liliridhika na hatua za awali za utekelezaji na lilitoa mwongozo stahiki wa hatua za kuchukuliwa pale ilipohitajika. Baraza
litaendelea kukutana mara kwa mara ili kutathmini na kutoa mwelekeo wa
utekelezaji wa Mikakati iliyowekwa ya Mfumo huu mpya;
(b) Utekelezaji wa Mikakati katika Maeneo Makuu Sita ya Matokeo Kitaifa;
Mheshimiwa Spika,
14. Utekelezaji
wa mikakati katika maeneo makuu sita ya matokeo kitaifa ulianza mara
baada ya uchambuzi wa maabara kukamilika. Mafanikio ya kuridhisha
yamepatikana katika kila moja ya maeneo yale sita, hasa ikizingatiwa
kwamba Mfumo huu ni mageuzi makubwa sana katika utendaji Serikalini.
Katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu wa fedha, kuanzia
mwezi Julai hadi Septemba, 2013; baadhi ya matokeo yaliyopatikana ni
pamoja na yafuatayo:
(a) Katika
Sekta ya Kilimo, Serikali inatekeleza miradi 26 ya umwagiliaji kwa
Wakulima wadogo na pia imekarabati maghala 26 ya mpunga kati
ya 39yanayotumiwa na wakulima katika maeneo yaliyopewa kipaumbele hasa
katika eneo la SAGCOT.
(b) Katika
Sekta ya Nishati ya Umeme, jumla ya Wateja wapya 27,494wameunganishwa
na kupatiwa umeme, ikiwa ni Asilimia 18.3 ya lengo la kuunganisha wateja
wapya 150,000 hadi mwisho wa mwaka 2013/2014. Aidha, vipande vya Bomba
la Gesi 20,491 vinavyotosheleza
ujenzi wa Kilomita 243.8 za Bomba la Gesi tayari vimewasili Nchini, na
uchomeleaji wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam
umekamilika kwa Kilomita 124.3. Vilevile, Kilomita 447 za njia ya Bomba la Gesi zimesafishwa;
(c) Katika
Sekta ya Elimu, Shule za msingi 5,916 zilipatiwa mitihani ya marejeo na
mazoezi, sawa na Asilimia 100 ya lengo la mwaka. Aidha, Mafunzo Kazini
kuhusu ufundishaji yametolewa kwa Walimu katika Shule 1,325sawa na
Asilimia 65 ya lengo la Shule 2,048 kwa mwaka huu wa fedha;
(d) Kwa upande wa huduma za maji, wananchi wapatao 752,000 waishio Vijijini wamepatiwa huduma ya maji. Mafanikio haya yanafanya
idadi ya Wananchi waishio Vijijini ambao wanapata majisafi na salama
kufikia takribani Milioni 15.9. Kasi hii ya upanuzi wa huduma za Maji
Vijijini imewezekana baada ya Wizara ya Maji kugatua
madaraka ya usimamizi wa miradi husika kwa Sekretarieti za Mikoa na
Halmashauri za Wilaya, jambo ambalo limewafanya Watendaji kuwajibika na
kuharakisha utendaji wao wa kazi. Aidha,
hatua zilizochukuliwa zimeiwezesha Wizara ya Maji kuongeza ufanisi
katika masuala ya ununuzi wa huduma, ikiwemo ujenzi na vifaa vyake,
kutoka wastani wa siku 265 za hapo awali hadi siku 90 za sasa.
Mheshimiwa Spika,
15. Mafanikio
haya na mengine mengi ambayo sikuyataja hapa yameonyesha kuwa
tukidhamiria, tunaweza kubadilisha kabisa matokeo ya juhudi zetu na
kuifikia dhamira yetu ya kuwa ni Taifa la Kipato cha Kati ifikapo mwaka
2025;
Mheshimiwa Spika,
16. Kufuatia
mafunzo yaliyotolewa mapema mwezi Juni, 2013 kwa Watendaji wa Wizara
husika, Wakuu wa Mikoa wote, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
zote Nchini, mnamo Mwezi Septemba 2013 nilikutana na Wakuu wa Mikoa na
Makatibu Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara ili kujadili kwa kina
Taarifa za utekelezaji wa Miradi ya kipaumbele chini ya Mfumo huu.
Aidha, katika Vikao hivyo, nimezielekeza Wizara, Mikoa na Halmashauri
zote Nchini kufanya yafuatayo:-
(a) Kuchambua
miradi iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha ambayo ipo nje
ya Mfumo wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” kwa kutambua manufaa
yanayotarajiwa baada ya kukamilika na mahitaji halisi;
(b) Kuipanga miradi hiyo kwa kipaumbele ili kuweka mkazo katika miradi itakayokamilika haraka na kuwa na manufaa makubwa kwa Wananchi; na,
(c) Kuweka utaratibu wa Kimfumo na Kitaasisi wa kufuatilia utekelezaji wa miradi yakipaumbele.
Mheshimiwa Spika,
17. Ninafurahi
kutoa taarifa kuwa Wizara na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa zimeupokea mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa kwa hamasa
kubwa. Ili kuhakikisha azma yao ya kutekeleza majukumu yao katika Mfumo
huu kikamilifu, iliamuliwa kuwa Viundwe Vitengo vya kusimamia
utekelezaji katika Ngazi ya Mkoa (Regional Delivery Units (RDUs),
sambamba na vile Vitengo vya ufuatiliaji vya Wizara ili utekelezaji
katika Maeneo Makuu ya Matokeo Kitaifa ufanyike kwa ufanisi na umakini
stahiki. Hatua hii inazingatia umuhimu wa kuhakikisha kuwa maeneo kama
Elimu na Maji ambayo Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zina mchango
mkubwa katika utekelezaji yanapata msukumo wa kutosha. Kazi hii
imeshaanza, na taarifa zilizowasilishwa ni za kutia moyo sana.
Mheshishimiwa Spika,
18. Kwa
kuzingatia mafanikio ya awali yaliyopatikana, Serikali imetoa maelekezo
kwa Wizara, Idara na Taasisi ambazo bado hazijaingia katika Mfumo wa
Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa zisisubiri hadi zitakapoingia rasmi
bali zianze kujipanga na kutekeleza mipango, miradi na program zao kwa
kutumia mbinu ambazo zinatumika katika Mfumo huo pamoja na Rasilimali
fedha na Wataalam waliopo. Msisitizo ni kwamba Wizara zote na Mikoa
ijipange upya na kuongeza ubunifu na kufanya vizuri zaidi katika
kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kwamba Taifa
letu linafikia malengo ya maendeleo tuliyojiwekea katika Dira ya
Maendeleo ya Taifa 2025. Aidha, napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa
Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuimarisha usimamizi wa
Watendaji wao kwa kuzingatia taratibu za uwajibikaji zilizowekwa chini
ya mfumo huu mpya ili kuleta ufanisi na tija ya utendaji Serikalini
pamoja na kupata matokeo makubwa tarajiwa ya Kukuza Uchumi na kuondoa
umaskini;
IV: MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO YA TAIFA WA MWAKA 2014/2015
Mheshimiwa Spika,
19. Mwanzoni mwa Mkutano huu wa Bunge Serikali iliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo 2014/2015. Napenda
kutumia fursa hii tena kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na
michango yao mizuri ambayo itatuwezesha kuboresha Mpango na Bajeti ya
Mwaka ujao wa Fedha 2014/2015. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Stephen
Wasira (Mb.) pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wa Kisekta waliotoa maelezo
fasaha ya ufafanuzi wa Hoja zilizojitokeza wakati wa Mjadala wa
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo. Kwa kuzingatia michango mizuri na
yenye tija iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Mawaziri
wakati wa kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka
2014/2015, nami naomba uniruhusu kusisitiza mambo machache kama
ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika,
20. Kama Waheshimiwa Wabunge watakavyokumbuka katika
majadiliano yaliyokuwa yanaendelea, moja ya jambo ambalo Waheshimiwa
Wabunge wamelizungumzia kwa kina, ni juu ya wingi wa vipaumbele vya
Taifa. Aidha, imeonekana pia kuwa miradi ya maendeleo ni mingi sana
kiasi kinachosababisha miradi hiyo kutotekelezeka kutokana na ufinyu wa
rasilimali fedha. Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa
Vipaumbele vilivyopendekezwa na Serikali vinategemeana na vinalenga
kutanzua vikwazo vikuu vya kiuchumi Nchini ili kufungua fursa za ukuaji
wa uchumi wa Taifa na kuharakisha maendeleo na ustawi wa Wananchi wa
Tanzania. Pendekezo la Serikali ni kuwa njia bora si kupunguza
vipaumbele hivi sasa, bali ni kupanga vizuri mtiririko wa utekelezaji wa
miradi ndani ya kila kipengele ili kuongeza jitihada za kuongeza
Mapato, na kusimamia nidhamu ya matumizi.
Mheshimiwa Spika,
21. Kwa
kuwa Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016) ni
wa kwanza unaojenga msingi wa mipango mingine ya maendeleo ya miaka
mitano itakayoandaliwa, ni dhahiri kuwa kasi ya utekelezaji wake
itarahisisha utengenezaji wa mipango mingine na kupunguza vipaumbele vya
msingi katika mipango ijayo. Hivyo, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge
washirikiane kwa karibu na Serikali kuhakikisha kuwa miradi iliyopangwa
katika ngazi zote inatekelezwa kwa ufanisi ili Mpango huu wa mwanzo
utekelezeke kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika,
22. Mjadala
na Hoja nyingine zilijielekeza katika changamoto za upatikanaji wa
Ajira kwa Vijana Nchini. Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka
2012, Asilimia 34.7 ya nguvu kazi ya Tanzania ni Vijana wa umri wa kati
ya miaka 15 - 35. Kundi hili la Vijana ndilo lenye kiwango kikubwa cha
ukosefu wa ajira cha Asilimia13.4 hapa Nchini. Pamoja na kuwa Vijana
hawa wamekuwa wakipata kazi hususan katika Sekta za Ujenzi, Kilimo na
Hoteli, ajira zao nyingi zimekuwa za muda.
23. Katika
kukabiliana na changamoto hii, Serikali imeandaa Programu ya Ajira kwa
Vijana itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Malengo ni
kupatikana fursa za ajira 840,000 kwa kuwezesha jumla ya
Miradi 10,000 ya Wahitimu wa Elimu ya Juu wapatao 30,000 kutoka Vyuo
mbalimbali ambao watatoa ajira za moja kwa moja kwa wahitimu
wengine 270,000 na ajira zisizo za moja kwa moja540,000. Programu hii
itajengea Vijana uwezo katika stadi za kazi; ujasiriamali; na kuwapatia
Vijana mitaji, nyenzo na vifaa vya kufanyia kazi; na kuwapatia Vijana
maeneo ya uzalishaji na biashara. Serikali inatarajia kuelekeza fedha
zaidi katika kipindi husika ili kuwezesha utekelezaji wa Programu hiyo.
Aidha, naipongeza Sekta Binafsi kwa mchango wao mkubwa katika kukuza
uchumi wa Nchi na kuongeza ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Spika,
24. Kilimo
ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika Mpango wa mwaka 2014/2015. Hili
ndilo eneo kubwa kwa maana ya kuongeza fursa za ajira na kipato kwa
Wananchi wanaoishi Vijijini, kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa namna
ambayo ni shirikishi ili kupunguza umaskini. Hivyo, ili kujibu
matatizo ya msingi ya umasikini wa kipato Mpango wa Maendeleo 2014/2015
utatoa kipaumbele katika mambo muhimu yafuatayo:
(i) Utafiti wa kilimo cha mazao, hususan katika uzalishaji wa mbegu bora, mifugo na uvuvi;
(ii) Kuimarisha huduma za ugani kwa kilimo, mifugo na uvuvi na kuimarisha upatikanaji na matumizi ya mbolea kwa ajili ya kilimo;
(iii) Kuimarisha Ushirika wa Wakulima na Wafugaji;
(iv) Kuongeza
fursa za mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ikiwa ni pamoja na
kukamilisha uanzishwaji wa Benki ya Kilimo mwezi Januari 2014;
(v) Kuwezesha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo, na mifugo;
(vi) Kujenga na kukarabati skimu za umwagiliaji;
(vii) Upatikanaji wa ardhi kwa kilimo na mifugo kwa kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi; na
(viii) Kuendeleza shughuli za kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi;
Mheshimiwa Spika,
25. Mpango wa Maendeleo huandaliwa katika ngazi zote Tano za Utawala kulingana na majukumu ya Serikali ambazo ni:
Moja: Vijiji na Mitaa;
Pili: Kata;
Tatu: Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri);
Nne: Mikoa; na
Tano: Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali.
Mamlaka
husika katika ngazi zote zinatakiwa kuandaa Mipango yao kwa kuzingatia
maeneo ya vipaumbele kama yalivyoainishwa katika Mapendekezo ya Mpango
wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015. Mipango lazima ilenge katika maeneo
yenye kuleta matokeo makubwa na ya haraka hususan katika kuchochea
maendeleo ya maeneo mengine na Programu nyingine katika ukuaji wa uchumi
na kupunguza umaskini.
Katika
kila ngazi, Wadau wengine kama vile Sekta Binafsi, Asasi Zisizo za
Kiserikali, Mashirika ya Dini na Washirika wa Maendeleo washirikishwe
kikamilifu. Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali
ziandae Mpango na kuuwasilisha Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Wiki ya
Nne ya mwezi Januari, Mwaka 2014.
Katika
ngazi za Mikoa na Wilaya, uandaaji uanze katika ngazi ya Kijiji na
Mtaa, Kata, Halmashauri na hatimaye kwenye Mkoa. Mpango uliopitishwa na
Mkoa uwasilishwe Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa na Wizara ya Fedha, Wiki ya Nne ya Mwezi Januari, 2014. Mpango wa
Maendeleo wa Taifa utajadiliwa na Bunge kuanzia Mwezi Aprili hadi Juni,
2014 na utekelezaji wake utaanza Mwezi Julai 2014 hadi Juni 2015;
Mheshimiwa Spika,
26. Mapendekezo
ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2014/2015 ndiyo yatatumika katika
utayarishaji wa Mipango ya Maendeleo ya Wizara, Idara za Serikali
zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali, Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa ya mwaka ujao wa fedha 2014/2015. Hivyo, nawaomba
Waheshimiwa Wabunge kutumia taarifa zilizotolewa hapa Bungeni kutoa
ufafanuzi kwenye Vikao vya Baraza la Madiwani katika Halmashauri zao
wakati wa kujadili Mipango yao. Aidha, napenda kutumia fursa hii
kuzihimiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuainisha vipaumbele
vinavyolenga katika maeneo yenye kuleta matokeo makubwa na ya haraka ya
Kiuchumi na Kijamii; na pia yenye kuchochea maendeleo ya maeneo mengine.
Vilevile, vipaumbele vya Halmashauri vilenge kufungulia fursa za ajira,
kuongeza mapato ya ndani na kuvutia uwekezaji wa Sekta Binafsi katika
maeneo yao.
V: SEKTA YA KILIMO
a) Hali ya chakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
27. Kwa
ujumla hali ya upatikanaji wa Chakula Nchini hadi kufikia Mwezi Oktoba
2013 ni ya kuridhisha kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa
2012/2013 ambapo mazao yake yanaendelea kuingia sokoni kutoka maeneo
mbalimbali hapa Nchini. Tathmini ya awali iliyofanyika mwezi
Julai/Agosti, 2013 inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika
Msimu wa kilimo wa 2012/2013 utafikia Tani 14,383,845 za chakula
zikiwemo Tani 7,613,221 za mazao ya nafaka na Tani 6,770,624 za mazao
yasiyo ya nafaka. Kiasi hicho cha chakula kilichozalishwa ni ongezeko
la Tani 2,234,726 za chakula, ikilinganishwa na mahitaji ya chakula kwa
mwaka 2013/2014 ya Tani 12,149,120. Kiwango hicho
kinajumuisha Tani 354,015za mahindi na Tani 466,821 za mchele. Hivyo
napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla kuwa
tutakuwa na chakula cha kutosha Nchini kwa Asilimia 118.
Mheshimiwa Spika,
28. Vilevile,
tathmini hiyo inaonesha kuwa, pamoja na kuwepo kwa chakula cha kutosha
na cha ziada, Halmashauri 61 katika Mikoa ya Manyara, Shinyanga, Simiyu,
Arusha, Dodoma, Lindi, Tanga, Singida, Mara, Morogoro, Kilimanjaro,
Mwanza, Pwani, Mtwara, Kigoma na Tabora zinatarajiwa kuwa na uhaba wa
chakula.
29. Natoa
wito kwa Halmashauri zinazohusika katika Mikoa hiyo kufuatilia kwa
karibu utaratibu wa kupata chakula kinachotolewa kutoka maeneo yenye
ziada na kuhakikisha kuwa kinafika mapema kwenye maeneo yao kabla
Wananchi wa maeneo hayo hawajaanza kulalamika.
(b) Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
30. Kutokana
na hali ya upatikanaji wa chakula kuwa nzuri, Bei za wastani za vyakula
hasa mahindi na mchele katika Soko Nchini zimeendelea kushuka. Kwa
mfano, bei ya mahindi ilishuka kutoka Shilingi 774.30 kwa kilo mwezi
Februari, 2013 hadi Shilingi 535.40 kwa Kilo mwezi Septemba 2013. Kwa
upande wa mchele, bei kwa kilo moja imeshuka
kutoka Shilingi 1,825.45 mwezi Februari, 2013 hadi
kufikia Shilingi 1,206.70 mwezi Septemba 2013, na bei ya mchele imeshuka
zaidi hadi kufikia Shilingi 1,146.70 katika mwezi Oktoba, 2013.
(c) Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa
Mheshimiwa Spika,
31. Serikali
kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula imepanga kununuaTani
250,000 za nafaka katika msimu wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 23
Oktoba, 2013, Wakala alikuwa amekwishanunua kiasi cha Tani 218,412 za
nafaka sawa na Asilimia 87.37 ya lengo lililowekwa ambapo Tani
217,919 kati ya hizo ni za Mahindi na Tani 493 ni za mtama. Aidha, hadi
kufikia tarehe 23 Oktoba 2013, maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula yalikuwa na jumla ya Tani 232, 921 za nafaka, kati ya hizo Tani
232,419 ni za mahindi na Tani 493,103 ni za mtama. Kiasi hiki cha nafaka kinajumuisha albaki ya Tani 25,452 za mahindi kutoka msimu uliopita wa 2012/2013.
Mheshimiwa Spika,
32. Serikali
inaendelea na tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe katika
Halmashauri 61 zilizoainishwa kuwa na hali tete ya chakula kwa lengo la
kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula ili kutafuta ufumbuzi wa
kudumu wa tatizo hili. Nitumie fursa hii kwa mara nyingine tena
kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwahimiza Wakulima hasa walioko
katika maeneo yenye chakula cha ziada kuhifadhi Chakula cha kutosha kwa
mahitaji ya Kaya zao. Aidha, Wakala wa Taifa na Hifadhi ya Chakula
wajipange vizuri kuhamisha Chakula kutoka maeneo yenye ziada na kupeleka
kwenye maeneo yaliyoainishwa kuwa na hali tete mara taarifa ya upungufu
itakapotolewa.
Mheshimiwa Spika,
33. Pamoja
na juhudi za Serikali za kuhakikisha kwamba kuna chakula cha kutosha,
natambua Changamoto zilizopo katika ununuzi wa Chakula kupitia Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Natambua kuwepo kwa madeni yanayotukabili
kwenye ununuzi wa nafaka kwa ajili ya Wakala yaani NRFA. Hata hivyo,
Mikoa inayohusika na madeni hayo ni Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga,
Ruvuma, Rukwa na Tanga. Serikali itahakikisha deni hilo hilo linalipwa
ndani ya mwaka huu wa fedha 2013/2014.
(d) Mpango wa Pembejeo za Ruzuku
Mheshimiwa Spika,
34. Kama
nilivyoeleza katika Mkutano wa 12 wa Bunge, katika msimu wa 2013/2014
Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 112.564 kwa ajili ya ruzuku
ya mbolea, na pembejeo. Aidha, nilielezea kuhusu utaratibu mpya wa kutoa
ruzuku utakaohusisha uwiano wa Asilimia 80 kwa Vocha na Asilimia 20 mikopo. Ili
kuhakikisha Mfumo huu mpya unatekelezwa kikamilifu na kuleta matokeo
yaliyotarajiwa, Serikali imetoa mafunzo ya utoaji pembejeo kwa njia ya
mikopo kwa Washauri wa Kilimo wa Mikoa, Maafisa Ushirika wa Mikoa na
Wilaya na Maafisa Kilimo wa Wilaya kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza
ikihusisha Mikoa ya Shinyanga, Geita na Manyara; na Awamu ya Pili
inahusu Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Iringa. Aidha, uchambuzi wa
takwimu za Vyama vya Ushirika na Vikundi vya Wakulima watakaokopeshwa
pembejeo za Kilimo mwaka 2013/2014 umefanyika katika Mikoa ya Iringa,
Ruvuma, Shinyanga, Njombe, Mbeya, Geita na Manyara. Takwimu zinaonesha
kuna SACCOS 214, AMCOS 163 na Vikundi vingine 51 vyenye
Wakulima 88,290 watakopeshwa pembejeo za Kilimo. Natoa Wito kwa Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuendeleza mafunzo haya kwa Mikoa
iliyobaki.
(e) Hali ya Usambazaji wa Vocha za Pembejeo
Mheshimiwa Spika,
35. Kuhusu
hali ya Usambazaji wa Vocha za Pembejeo katika Msimu wa 2013/2014
napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, jumla ya Vocha2,796,300 kwa
ajili ya Kaya 932,100 zikiwemo Vocha 932,100 za mbolea ya
kupandia, 932,100 za mbolea ya kukuzia, Vocha 441,100 za mbegu za
mahindi chotara; Vocha 432,000 za mahindi ya OPV na Vocha 60,000 za
mbegu za mpunga zilisambazwa katika Mikoa yote hapa Nchini. Nitoe wito
kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya kwa kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani
na Viongozi wengine kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata na wanatumia
Vocha hizi kupata pembejeo kama ilivyokusudiwa. Aidha, tushirikiane
kuhakikisha kuwa wale watakaokwenda kinyume na utaratibu huu wa
usambazaji wa Vocha hizo wanashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria.
(f) Changamoto za Mbolea ya Minjingu
Mheshimiwa Spika,
36. Juhudi
za Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa Pembejeo za ruzuku ziko
dhahiri. Hata hivyo, imebainika kwamba katika mahitaji ya mbolea, kilio
kikubwa cha Wakulima ni kupatiwa mbolea kwa wakati. Aidha, wapo
Wananchi wanaolalamikia mbolea ya Minjingu Mazao ambayo ni kweli hapo
awali ilikuwa na matatizo. Lakini sasa, mbolea hii imeboreshwa kwa
kiwango kikubwa kwa kuongezewa virutubisho.
Mheshimiwa Spika,
37. Mbolea
ya Minjingu ya awali ilikuwa na virutubisho vya udongo viwili tu vya
Kalisiumu na Fosfeti. Mbolea ya Minjingu Mazao imeboreshwa kwa kuongezwa
virutubisho vinne zaidi na kufanya virutubisho hivyo kuwa sita yaani Kalisiumu, Fosfeti, Naitrojeni, Salfa, Boroni na Zinki.
38. Kwa
msingi huo, Mbolea ya Minjingu mazao inaweza kutumika katika aina
mbalimbali za udongo tofauti na ilivyokuwa awali. Aidha, Mbolea ya
Minjingu Mazao ni ya chengachenga (granulated) tofauti na ya awali ambayo ilikuwa katika mfumo wa unga (dust)
ambapo pengine matumizi yake hayakuwa rafiki kwa mkulima. Baada ya
kuboreshwa, kwa sasa Mbolea hii ya Minjingu inatumika kwa mazao mengi
hususan mahindi, mpunga na alizeti katika sehemu mbalimbali na aina
mbalimbali za udongo.
Mheshimiwa Spika
39. Mkulima
anahitaji kutumia mifuko miwili ya mbolea ya Minjingu Mazao ya
kilo50 kila mmoja kwa wakati mmoja ikilinganishwa na mfuko mmoja wa
kilo 50 wa mbolea ya DAP. Hata hivyo, ukilinganisha na mbolea ya DAP,
mkulima anayetumia Minjingu Mazao anawezesha shamba lake kupata
virutubisho zaidi. Kwa hiyo, Mbolea ya Minjingu Mazao ni nafuu
ikilinganishwa na Mbolea ya DAP.
40. Bei
ya mbolea ya Minjingu Mazao kwa mfuko mmoja ni Shilingi 32,500/=hivyo
kwa mifuko miwili ni Shilingi 65,000 katika Wilaya zote Nchini
ikilinganishwa na bei ya wastani ya Shilingi 75,000/= ya mfuko mmoja wa
DAP. Aidha, kwa aina zote mbili za mbolea zinapotumika kupandia, lazima
mkulima aweke mbolea nyingine ya kukuzia ambayo ina virutubisho vingi
vya Naitrogeni kama CAN au UREA.
41. Majaribio
ya kutumia Mbolea ya Minjingu yalianza mwaka 1977 kuendelea hadi mwaka
2006 ikiwa katika hali ya unga. Mwaka 2007 Mbolea hiyo iliboreshwa kwa
kuiweka katika hali ya chenga chenga (granulation) ingawa
virutubisho havikuboreshwa. Mbolea hiyo iliendelea kutumika katika hali
hiyo hadi mwaka 2009. Hivyo, mwaka 2010 Mbolea hiyo iliboreshwa kwa
kuongezea virutubisho ambavyo baada ya utafiti wa kuihakiki (validation) iliingizwa Sokoni mwaka 2012.
42. Kwa
sasa, Mbolea ya Minjingu Mazao inatumika katika Mikoa ya Iringa,
Ruvuma, Rukwa, Mbeya, Njombe, Katavi, Kigoma na Morogoro. Aidha, kuna
mikoa mingine ambako mbolea hii imepelekwa pamoja na mbolea nyingine kwa
ajili ya Wakulima wenyewe kufanya maamuzi ya kuchagua.
Mheshimiwa Spika
43. Matumizi
ya Mbolea ya Minjingu Mazao katika mwaka 2012/2013 yamewezesha
kuongezeka kwa uzalishaji wa mahindi, mpunga na alizeti kwa ekari
hususan katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Changamoto kubwa ni elimu
juu ya matumizi sahihi ya Mbolea hiyo kwenye baadhi ya maeneo.
44. Katika
kutatua changamoto hii, Wizara inashirikiana na Mmiliki wa Kiwanda cha
Mbolea cha Minjingu kuendesha mashamba darasa katika Wilaya mbalimbali
Nchini. Vilevile, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo, inaendelea kufanya utafiti katika maeneno mbalimbali
ya Nchi ili kuboresha matumizi sahihi ya Mbolea hiyo katika aina
mbalimbali za udongo (site specific validation trials).
45. Changamoto
zinazohusiana na Mbolea ya Minjingu katika Wilaya ya Mbozi zitaangaliwa
kwa namna yake. Kitendo hicho ni cha udanganyifu kwani Mbolea ya aina
nyingine ni bei kubwa ikilinganishwa na ya Minjingu Mazao. Kutokana na
kitendo hicho kuwa kinyume na Sheria ya Mbolea ya 2009, Mamlaka ya
Udhibiti wa Mbolea kwa kushirikiana na Wakaguzi wa mbolea wa Wilaya ya
Mbozi ilimkamata Wakala husika na kumchukulia hatua za kisheria. Naagiza
Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuchunguza mbolea inayopelekwa katika
maeneo yao isije ikachakachuliwa.
Mheshimiwa Spika,
46. Kwa
kuzingatia Changamoto zilizojitokeza katika matumizi ya mbolea ya
Minjingu katika maeneo mbalimbali Nchini Serikali itaendelea kuzitafutia
ufumbuzi kwa kuchukua hatua zifuatazo:
(a) Kutoa
elimu kwa Wakulima kuhusu namna bora ya kutumia Mbolea ya Minjingu
Mazao kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam
kuhusu aina ya udongo na mazao yanayofaa kwa mbolea hiyo. Vilevile,
kuwaelimisha Wananchi kuhusu ubora wa Mbolea ya Minjingu Mazao
ikilinganishwa na Mbolea za aina nyingine hasa kutokana na virutubisho
vilivyoongezwa katika mbolea.
(b) Mamlaka
ya Udhibiti wa Mbolea imeagizwa kufuatilia na kufanya uchunguzi wa
madai ya Wakulima kuhusu changamoto za matumizi ya mbolea ya Minjingu
Mazao hasa katika Wilaya ya Mbozi na sehemu nyingine zenye matatizo ya
matumizi ya mbolea hiyo Nchini.
(c) Naomba
kuiagiza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuendelea kushirikiana
na Wadau kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali Nchini. Kutokana na
utafiti huo itoe ushauri na mwongozo kwa Wakulima wote Nchini kuhusu
njia sahihi za kutumia Mbolea ya Minjingu Mazao katika aina mbalimbali
za udongo na mazao yanayofaa kulimwa. Lengo ni kuongeza tija katika
uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa eneo. Kwa Wilaya ya Mbozi Wizara itoe
mwongozo kuhusu nini kifanyike kwa sasa wakati hatua za utafiti na
uchunguzi wa matumizi sahihi ya Mbolea hiyo zinaendelea.
(g) Uzalishaji na Ununuzi wa Mazao ya Biashara
Mheshimiwa Spika,
47. Katika
miaka ya hivi karibuni kumekuwa na Changamoto mbalimbali za uzalishaji
na ununuzi wa baadhi ya mazao ya biashara hapa Nchini ikiwemo Kilimo cha
zao la Pamba, Korosho, Tumbaku na Kahawa. Kwa kuzingatia ufinyu wa
muda, leo naomba mniruhusu nizungumzie kidogo kuhusu kilimo cha mazao
mawili ya Pamba na Korosho.
(h) Uzalishaji na Ununuzi wa Zao la Pamba
Mheshimiwa Spika,
48. Serikali
inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa Wakulima wa Pamba
wanazalisha kwa tija kwa kutumia mbegu bora, utumiaji wa pembejeo
(Viuadudu na Mbegu), kutoa huduma za ugani kupitia Maafisa wa Kilimo
katika Halmashauri za Wilaya na pia kuhamasisha Kilimo cha pamba kwa
kushirikiana kwa karibu na Wadau mbalimbali ikiwemo Sekta Binafsi.
49. Katika
kilimo hiki cha Pamba, Zana za kilimo zinazotumika kwa sasa ni majembe
ya kukokotwa na wanyama kazi kwa ajili ya kulima nah ii ni dhahiri
haiwezi kuongeza tija. Ttahakikisha tunatumia Zana za Kisasa.
(i) Mkakati wa Wizara kupata masoko ya uhakika ya pamba
50. Serikali
pia inaendelea kuhakikisha kwamba pamba inaongezwa thamani hapa Nchini
kwa kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya nyuzi na nguo.
Uwekezaji mpya unafanyika kwa kujenga kiwanda cha nyuzi na nguo cha
Dahong Mkoani Shinyanga na pia Mradi mkubwa wa kuzalisha pamba,
kuchambua, kutengeneza nyuzi, kutengeneza vitambaa na nguo unaotarajiwa
kutekelezwa na Kampuni ya Kijapani (NITORI) katika Wilaya ya Handeni.
Kwa sasa mradi huo uko katika hatua ya umilikishwaji wa Ardhi.
51. Vilevile,
Serikali imeanzisha mafunzo ya Uhandisi na Ubunifu katika Viwanda vya
Nyuzi na Nguo. Pia tumeanzisha kozi ya ubunifu wa mitindo katika mitaala
ya VETA na Mafunzo ya Shahada ya uzamili katika “Textile” katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Lengo ni kuhakikisha kuwa kuna watalaamu
wa kutosha katika mchakato wa kuongeza thamani ya pamba.
(j) Tofauti za ubora wa mbegu za pamba manyoya na De – linted
Mheshimiwa Spika,
52. Sina
shaka Watanzania wameshasikia kuwa kwa sasa tunazo aina mbili za mbegu
za Pamba zinazotumika hapa Nchini. Tunayo mbegu yetu ya asili ya Pamba
Manyoya na Mbegu mpya na ya kisasa ya Pamba isiyo na manyoya
(De-linted). Aina hizi zinatofautiana sana kwa ubora na bei. Mbegu ya
manyoa ina uotaji wa chini ya Asilimia 50 wakati ile ya De –linted ni
zaidi ya Asilimia 90. Mbegu ya manyoya hutumika nyingi kwa eneo (kilo 25
kwa Ekari), wakati De – linted ni kilo 6tu kwa Ekari, sawa na
Shilingi 7,200 kwa Ekari kwa bei ya Shilingi 1,200 kwa kilo. Mbegu ya
manyoya ina tija ndogo (inazalisha kati ya kilo 250 na 300 kwa Ekari)
ikilinganishwa ya mbegu ya De-linted inayozalisha Kilo 450 – 1200 kwa
Ekari. Mbegu ya manyoya ina uwiano mdogo wa pamba nyuzi (Asilimia 33)
ikilinganishwa na mbegu De-linted ambayo uwiano wake ni Asilimia 36.
(k) Jitihada za Wizara kupunguza bei ya mbegu bora
Mheshimiwa Spika,
53. Ili
kuwawezesha Wakulima kutumia mbegu bora (de-linted) Serikali imetoa
ruzuku ya Shilingi Billioni 4.8 ili kufanya mbegu hiyo ipatikane kwa
Shilingi 600 kwa kilo kwa mkulima badala ya Shilingi 1,200 kwa kilo
iliyotumika mwaka 2012/2013.
54. Serikali
pia inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutoa elimu kwa wakulima wa
pamba kuhusu mbegu bora. Kwa mfano, Viongozi wa maeneo yanayolima pamba
(Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na baadhi ya Madiwani) wamepelekwa
katika kiwanda cha kuchakata mbegu bora za Pamba cha Kampuni ya Quton
ili kupata maelezo na kujionea hali ya utendaji wa mbegu bora katika
kilimo.
55. Kupitia programu ya kuendeleza zao la pamba wakulima wawezeshaji (Lead Farmers)
3000 wa vikundi vya Kilimo cha Mkataba wanaendelea kupewa mafunzo ya
kilimo bora na matumizi ya mbegu bora ili watumike kupeleka elimu hii
kwa wakulima wenzao.
Mheshimiwa Spika,
56. Katika
msimu huu wa Kilimo wa 2013/14, Serikali imejipanga kusimamia
utekelezaji wa Kilimo cha Mkataba kwa lengo la kuleta ufanisi katika
Kilimo cha Pamba Nchini. Hatua hii inahusisha pia kutoa elimu ya
kutosha na kushirikisha kwa karibu Wadau katika kuzipatia ufumbuzi
changamoto zilizopo kwenye utaratibu mzima wa kilimo hicho ambacho kina
manufaa makubwa iwapo kitaeleweka na kutekelezwa vyema kwa misingi ya
haki miongoni wa wadau. Baadhi ya manufaa hayo ni:
(i) Uhakika wa upatikanaji wa pembejeo kwa mkulima kwa mkopo.
(ii) Kuongeza tija kutokana na kupata pembejeo na huduma za ugani.
(iii) Kuongeza
ubora wa pamba kutokana na matumizi makubwa ya pembejeo na huduma za
ugani pamoja na vikundi kutumika kama Mawakala wa kununua Pamba ya
wanachama wake hivyo kusimamia ubora
(iv) Uhakika wa soko la pamba ya mkulima
(v) Kupunguza wizi kupitia mizani ya mawakala
(vi) Wakulima kupata teknolojia kupitia uwekezaji
(vii) Kujenga na kuimarisha mfumo wa Ushirika kupitia vikundi vya wakulima.
(l) Elimu ya kilimo cha mkataba kwa wakulima
Mheshimiwa Spika,
57. Kupitia
programu ya kuendeleza zao la pamba, wakulima Wawezeshaji zaidi
ya 3,000 wamekwisha pokea mafunzo ya kilimo cha Mkataba wanao tumika
kupeleka elimu hii kwa vikundi vya wakulima. Wagani wa Halmashauri
wapatao 560wameshapata mafunzo haya. Chini ya Mpango huu kila mgani
anaweza kuhudumia vikundi hadi 20.
58. Napenda kuwaagiza
Viongozi na Wataalamu wa Kilimo waendelee kutoa elimu ya matumizi na
faida ya mbegu bora za De-linted au mbegu zisizokuwa na manyoya kwa
Wakulima wa Pamba Nchini. Aidha, mashamba darasa yatumike ipasavyo
kuonesha tija inayotokana na aina hiyo ya mbegu za Pamba
inapolinganishwa na mbegu zenye manyoya. Vilevile, Viongozi na
Wataalamu wa Kilimo waendelee kuwakumbusha Wakulima wa Pamba na
Watanzania kuwa utaratibu mpya wa Kilimo cha Mkataba una manufaa mengi
na makubwa. Tuendelee kuwashawishi Wakulima kujiunga na Kilimo cha
Mkataba bila kuwashurutisha isipokuwa tuwape elimu hasa kupitia mashamba
darasa. Wale watakaoshawishika kuingia katika utaratibu huu wasaidiwe
kwa kila hali ili wanufaike na kilimo hicho huku wakisaidia kutoa elimu
kwa Wakulima wengine ili wajiunge na aina hii ya kilimo. Ni matumaini
yangu ndani ya muda mfupi Wakulima watafahamu faida ya kilimo cha
mkataba.
(m) Zao la Korosho
Mheshimiwa Spika,
59. Kuhusu
Zao la Korosho, azma ya Serikali ni kuimarisha Viwanda vya Korosho na
kufufua vile vilivyopobinafsishwa ili viweze kusaidia kukuza Soko kwa
wakulima wa Korosho. Ili kutekeleza azma hiyo, Serikali imefanya
tathmini na kubaini kuwa Wawekezaji wengi katika Viwanda vya Korosho
vilivyobinafsishwa wameshindwa kutekeleza Mikataba ya Ubinafsishaji wa
viwanda hivyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ukosefu wa fedha za
uendeshaji, ukosefu wa nishati ya uhakika na Viwanda kutumia teknolojia
zilizopitwa na wakati. Ili kukabiliana na hali hiyo, Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika kwa kushirikiana na Shirika Hodhi la Mali za
Mashirika ya Umma (CHC) pamoja na Wadau wengine inaandaa mapendekezo ya
hatua za kuchukua dhidi ya Wawekezaji walioshindwa kuendeleza viwanda
hivyo. Dhamira ya Serikali ni kwamba Mwekezaji ambaye ameshindwa
kuendeleza kiwanda alichonunua kwa kuzingatia Makubaliano ya ununuzi na
Serikali, mali hiyo irudishwe Serikalini na ifanyiwe tathmini na
itangazwe upya ili kupata Wawekezaji mahiri na wenye nia thabiti ya
kuendeleza Viwanda husika.
Mheshimiwa Spika,
60. Sambamba
na hatua hiyo, Bodi ya Korosho Tanzania imeandaa Mpango wa Ubanguaji wa
miaka mitatu kuanzia mwaka 2012/2013 ambao umelenga kuwasaidia
wabanguaji wadogo na wa kati kuendesha shughuli za ubanguaji kwa ufanisi
kwa kuwapatia mafunzo, vifaa vya kubangulia, na kuwatafutia masoko ya
ndani, masoko ya kanda na masoko ya nje;
61. Hatua
iliyofikiwa kwa sasa ni kwamba, Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la
Korosho kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania umetenga fedha kwa
ajili ya kujenga viwanda vitatu katika Mikoa ya Ruvuma, Mtwara, na Pwani
kwa ajili ya kuwawezesha Wabanguaji wadogo na wa kati kumalizia baadhi
ya hatua za ubanguaji katika viwanda hivyo kwa ajili ya kukidhi matakwa
ya masoko makubwa ya korosho duniani.
Mheshimiwa Spika,
62. Ili
kuboresha kilimo cha Korosho, katika mwaka 2013/2014, Serikali
itaendelea kutoa ruzuku ya madawa kutoa huduma za ugani na kuhamasisha
wakulima wahudumie mikorosho na kupuliza madawa mapema.
Mheshimiwa Spika,
63. Kuhusu
ununuzi wa Korosho, katika msimu huu wa 2013/2014 ununuzi wa Korosho
utaendelea kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi za mazao Ghalani. Ukusanyaji
wa Korosho kutoka kwa wakulima umeanza katika maeneo mbalimbali Nchini.
Kwa mfano, katika Mkoa wa Mtwara, mnada wa kwanza wa Korosho ulianza
tarehe 25 Oktoba, 2013 ambapo ulihusisha Vyama vya Msingi vya Mkoa wa
Mtwara. Korosho zote zilizokuwa zimekusanywa na kutangazwa katika kila
mnada zilinunuliwa. Bei ya Korosho katika Mnada wa kwanza ilikuwa kati
ya Shilingi 1,402/= na 1,520/= kwa kilo ikilinganishwa na bei dira ya
Shilingi 1,000/= kwa kilo. Mnada uliofuatia bei ziliongezeka na kuwa
kati ya Shilingi 1,481/= na 1,570/= kwa kilo.
Mheshimiwa Spika,
64. Kwa
upande wa Mkoa wa Lindi, Vyama vya Msingi vilivyobaki chini ya ILULU
vilifanya Mnada wa kwanza tarehe 2 Novemba, 2013 ambapo jumla ya
Tani783.593 ziliuzwa. Vyama vingine 51 vya kutoka Wilaya ya Ruangwa,
Nachingwea na Liwale ambavyo vilijiondoa kutoka usimamizi wa Chama Kikuu
cha ILULU vitafanya mnada baada ya taratibu za kupata Kamati
itakayowasimamia zitakapokamilika. Vyama hivyo vimeomba kufanyiwa Minada
yake katika Wilaya ya Nachingwea ambako ndiko walikoweka Ofisi yao.
Mheshimiwa Spika,
65. Kwa
upande wa Wilaya ya Tunduru, bado haijapata mkopo mpaka sasa na juhudi
za kufuatilia zinaendelea. Taarifa kutoka Benki ya NMB inaonyesha kuwa
kuna uwezekano mkubwa wa Vyama vya Msingi vya TAMCU kupata mkopo msimu
huu kwani deni ambalo TAMCU walikuwa wanadaiwa na Benki hiyo ya NMB
limelipwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika,
66. Kwa
upande wa Mkoa wa Pwani, uwezekano wa Vyama vilivyo chini ya Chama
Kikuu cha Coast Region Cooperative Union (CORECU) kupata Mkopo ni mdogo
kutokana na kudaiwa fedha nyingi zaidi ya Shilingi Bilioni 7 za msimu wa
mwaka 2010/2011. Serikali imefanya Ukaguzi Maalum katika Vyama hivyo na
kubaini kwamba madeni hayo kwa kiwango kikubwa yamesababishwa na
ubadhirifu wa Viongozi na Watendaji wa Vyama hivyo. Hivyo, kupitia Ofisi
ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika hatua za kisheria zimechukuliwa ikiwa
ni pamoja na kuwataka wahusika wa ubadhirifu huo kufidia hasara hiyo.
Kwa upande mwingine, Wahusika wamekata rufaa, lakini Mamlaka yenye
dhamana imezitupilia mbali rufaa hizo zote 434, na kuwataka Wahusika
walipe kiasi cha fedha kinachodaiwa na Vyama vyao. Kutokana na hali
hiyo, Wakulima wa Mkoa wa Pwani wanashauriwa kupeleka mavuno ya Korosho
katika maghala yaliyoteuliwa. Minada ya Korosho itafanyika katika
maghala hayo na wakulima watalipwa mara moja baada ya minada kufanyika.
Mheshimiwa Spika,
67. Kutokana
na jitihada za Serikali zinazoendelea natoa wito kwa Bodi ya Korosho na
Wakuu wa Mikoa husika kuendelea kusimamia kikamilifu taratibu wa
ununuzi wa Korosho ili kuhakikisha kwamba Wakulima wanauza Korosho zao
walizovuna na kulipwa malipo yao halali kwa wakati.
(n) Hali ya mwenendo wa Mvua za vuli mwaka 2013 na athari kwa mazao ya vuli
Mheshimiwa Spika,
68. Taarifa
ya utabiri wa mwelekeo wa hali ya hewa hususan mvua katika kipindi cha
Oktoba hadi Disemba 2013 iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini
inaonesha kuwa mvua za vuli zinatarajiwa kuwa chini ya wastani katika
Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kaskazini mwa Morogoro,
Kilimanjaro, Arusha, Manyara na baadhi ya maeneo katika mikoa ya Mwanza,
Simiyu, Shinyanga Kagera, Geita na Mara. Pamoja na kwamba mvua za msimu
wa vuli zimechelewa kuanza katika maeneo mengi ambayo yalitarajiwa
kupata mvua za vuli, mvua hizi hazitarajiwi kuwa na mtawanyiko wa
kuridhisha.
(o) Athari za mvua za vuli zinazonyesha chini ya Wastani
Mheshimiwa Spika,
69. Kutokana
na utabiri huo wa Hali ya Hewa, tathmini ya awali iliyofanyika katika
maeneo yaliyotarajiwa kupata mvua za vuli inaonesha kuwa:
i. Hali ya mazao hasa katika Nyanda za juu Kaskazini na ukanda wa Pwani Kaskazini si ya kuridhisha,
ii. Mategemeo
ya mavuno ya vuli ni kidogo isipokuwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda
wa Ziwa Viktoria hususan katika Mikoa ya Kagera na Geita ambayo
yamepata mvua za wastani hadi chini ya wastani,
iii. Mchango
wa mavuno ya vuli ambao ni kati ya Asilimia 28-30 ya Chakula
kinachozalishwa katika maeneo yanayopata mvua hizo au
Asilimia 18 Kitaifa hauwezi kufikiwa katika hali hii ya mvua.
iv. Hali hii inaashiria kuwa kutakuwepo na upungufu wa Chakula katika maeneo hayo niliyotaja hapo juu.
Mheshimiwa Spika,
70. Kutokana
na hali hii, natoa wito kwa Wakulima katika maeneo haya kuzingatia
ushauri wa kupanda mazao yanayostahimili ukame na yanayokomaa kwa muda
mfupi. Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika Halmashauri husika wasimamie
suala hili kwa ukamilifu; ili kuepusha upungufu wa Chakula unaotarajiwa.
VI: NISHATI
(a) Kuongezeka kwa upatikanaji wa Nishati Vijijni (Miradi ya REA) na hali iliyofikiwa
Mheshimiwa Spika,
71. Wakati
wa Kuhitimisha Mkutano wa 12 wa Bunge nilieleza Mikakati ya Serikali
katika kueneza umeme Vijijini na matarajio ya baadaye. Napenda kulieleza
Bunge lako Tukufu kwamba tumeweza kupiga hatua katika baadhi ya maeneo
katika kuelekea kwenye malengo tuliyojiwekea. Tayari Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) ulitangaza zabuni mwezi Desemba 2012 kwa ajili ya
kuwapata Wakandarasi wa kupeleka umeme Vijijini na kujenga vituo vya
kupoozea umeme. Baada ya tathmini kufanyika, zabuni 15 za kupeleka umeme
Vijijini zilipata Wakandarasi. Mikoa ambayo ilipata Wakandarasi
katika awamu hiyo ni pamoja na Arusha, Dodoma, Iringa, Katavi,
Kilimanjaro, Mara, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu,
Singida na Tabora. Aidha Wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa
vituo vya kupozea umeme vya msongo wa Kilovoti 11 na 33 vya Ngara,
Kibondo, Kasulu, Kigoma, Tunduru na Mbinga walipatikana. Kwa sasa
Wakala unaendelea na kulipa malipo ya awali (advance payments) na Wakandarasi wanaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanza kazi. Miradi hii yenye thamani ya Shilingi Bilioni 430.82 inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2015.
Mheshimiwa Spika,
72. Mwezi
Mei, 2013 zabuni nyingine 10 ya Miradi yenye thamani ya
ShilingiBilioni 450 zilitangazwa kwa ajili yakuwapata Wakandarasi wa
kupeleka umeme Vijijini katika Mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma,
Lindi, Manyara, Mbeya, Morogoro, Pwani, Rukwa na Tanga. Kwa sasa
tathmini ya zabuni hizo inaendelea. Inatarajiwa kwamba Wakandarasi
kutokana na Tathmini hiyo watajulikana ifikapo tarehe 15 Novemba, 2013.
(b) Suala la Fidia, Sera; na Miongozo ya usambazaji Umeme Vijijini:
Mheshimiwa Spika
73. Ili
kuharakisha maendeleo ya upatikanaji wa Nishati Vijijini, suala la
Wananchi kuchangia nguvu kazi na kutoa njia na maeneo ya kupitisha nyaya
za umeme bila fidia pale inapowezekana limekuwa likisititizwa na
Serikali kutokana na ufinyu wa bajeti. Upo ukweli kwamba, Miradi mingi
imechelewa kutekelezwa kutokana na Wananchi kudai fidia ya miti na mazao
ya msimu yanayokutwa kwenye njia ya umeme. Kwa mfano miradi ya Awamu
ya Kwanza katika Mkoa wa Pwani imechelewa kuanza na kukamilishwa
kutokana na Wananchi kudai fidia ilipwe kwanza ndio ujenzi uendelee.
Pia, kwa sasa ujenzi umesimama katika maeneo ya Bungu-Nyamisati na
Kisiwa cha Mafia kutokana na Wananchi kudai fidia kwanza.
Mheshimiwa Spika,
74. Ni
kweli kwamba kulingana na Sheria zilizopo kama katika njia ya kupitisha
umeme yapo mazao yanayostahili kulipwa fidia. Hata hivyo kutokana na
bajeti finyu Wakala wa Nishati Vijijni unashindwa kutoa fidia
inayohitajika na kuona ni bora wale wanaojitolea maeneo yao wapelekewe
umeme haraka kuliko kusubiri bajeti kwa ajili ya fidia. Serikali inatoa
rai kwa Viongozi na Wananchi kuona umuhimu wa kujitolea maeneo yao ili
waweze kupata huduma hii muhimu mapema. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge
tushirikiane katika kuwahamasisha Wananchi katika maeneo yetu kuhusu
umuhimu wa kupata umeme mapema kwa maendeleo ya maeneo yetu.
(c) Utekelezaji wa Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam
Mheshimiwa Spika,
75. Shughuli za ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam zinaendelea vizuri. Mpaka
sasa usafishaji wa njia ya kulaza bomba unaendelea na tayari
Kilometa 484.17 kati ya Kilometa 517 zimekamilika. Aidha jumla ya
mabomba 20,491 yanayotosheleza kulazwa umbali wa
Kilometa 243.8yamekwishawasili Nchini. Kazi ya kuchimba mtaro, kuyapanga
mabomba katika mstari mmoja kwenye mkuza na kuyaunganisha pamoja kwa
kuchomelea inaendelea na hadi sasa Kilometa 124.3 zimeshaunganishwa.
Kazi zinazoendelea ni ujenzi wa kambi, nyumba za wafanyakazi katika
maeneo ya Songo Songo na Madimba, pamoja na maandalizi ya ujenzi wa
mitambo ya kusafirishia Gesi Asilia. Tutaendelea kutoa taarifa ya hatua
iliyofikiwa ya utekelezaji wa Mradi huu muhimu kwa Taifa letu.
76. Aidha,
katika kuhakikisha kwamba miradi hii inatekelezwa na kuleta manufaa
katika Nchi yetu, ninayo furaha kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa,
Serikali ilipitisha Sera ya Gesi Asilia tangu tarehe 10 Oktoba 2013,
Utaratibu wa kuichapisha sera hiyo katika lugha ya Kiswahili na
Kiingereza unaendelea. Vilevile Serikali kupitia Wizara ya Nishati na
Madini imeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Utekelezaji wa Sera ya
Gesi na imeanza kutayarisha Rasimu ya Sheria ya Gesi. Ni matumaini
yangu kwamba vitu vyote hivi vikikamilika Sekta ya Gesi Asilia
itaimarika.
VII: MIFUGO
(a) Operesheni Ondoa Mifugo Katika Maeneo Mbalimbali Nchini
Mheshimiwa Spika,
77. Kwa
muda mrefu sasa maeneo mbalimbali hapa Nchini yamekuwa yakikumbwa na
migogoro inayotokana na matumizi ya Ardhi hususan kwa Wafugaji wanaohama
kutoka maeneo yaliyokatazwa kisheria kwenda eneo lingine pasipo na
maandalizi ya kutosha ya kuwapokea. Utafiti unaonesha kuwa, migogoro ya ardhi hapa Nchini ina sura nne:
Moja: Migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji,
Pili: Migogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji,
Tatu: Migogoro kati ya Wananchi na Serikali, na
Nne: Migogoro kati ya Mamlaka moja na Mamlaka nyingine ndani ya Serikali inayotokana na migongano ya kimaslahi.
Mheshimiwa Spika,
78. Kuna
ukweli kwamba, kuongezeka kwa idadi ya Watu na kuongezeka kwa matumizi
ya ardhi kutaendelea kuongeza kasi na vipaumbele katika kugawa maeneo
yaliyoko wazi. Hali hii imeanza kuonekana katika
maeneo ya Wafugaji ambayo yameendelea kupungua siku hadi siku. Aidha,
shughuli za kilimo, maendeleo ya makazi, na matumizi mengine ikiwa ni
pamoja na kuongezeka kwa Vijiji kunakotokana na ongezeko la idadi ya
watu kumeendelea kupunguza eneo la malisho.
Mheshimiwa Spika,
79. Kuna
ukweli pia kwamba, mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa mifugo
katika maeneo ya Nchi kwa ajili ya kutafuta malisho na maji kumeendelea
kuchangia migogoro mingi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Kati ya mwaka 2005 na sasa, tumeshuhudia uhamiaji wa mifugo kutoka
mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa kwenda katika Mikoa ya Kusini na
Mashariki mwa Nchi. Uhamiaji huo licha ya kusababisha migogoro kati ya
watumiaji wengine pia imesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kwenye
maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi za Taifa. Baadhi ya maeneo hayo ni
pamoja na hifadhi za Wanyama pori za Burigi, Maswa na Meatu, Bonde la
Usangu na Bonde la Kilombero.
Mheshimiwa Spika,
80. Ni
matumaini yangu kwamba, maadam suala hili limepewa umuhimu na Bunge
lako Tukufu na hivyo kuunda Kamati ya kufuatilia migogoro hii, ni
dhahiri tutapata ufumbuzi wa kudumu katika tatizo hili. Niwaombe
Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla wanaotoka katika
maeneo yenye migogoro inayotokana na Wafugaji na Wakulima kutoa
ushirikiano katika kutoa taarifa muhimu kwa Kamati iliyoundwa ili
kulisaidia Taifa katika kutatua migogoro hii.
VIII: HALI YA ULINZI NA USALAMA NCHINI.
Mheshimiwa Spika,
81. Kwa
ujumla hali ya Ulinzi na Usalama Nchini imeendelea kuwa shwari,
isipokuwa katika maeneo machache ambako kulijitokeza vitendo
vinavyoashiria kuwepo kwa vikundi vya uhalifu na ujambazi. Serikali
kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kujipanga kukabiliana na matishio
mbalimbali ya kiusalama ikiwemo ugaidi. Tukio lililotokea Nchini Kenya
hivi karibuni na matukio ya kukamatwa kwa Vijana 12 kule Mtwara na lile
lililotokea Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga ambapo zaidi ya
watuhumiwa 46 wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali yanaashiria
kwamba ugaidi hauna mipaka unaweza kutokea katika Nchi yoyote.
Mheshimiwa Spika
82. Katika kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaendelea kudumu Nchini, Serikali imejipanga katika maeneo hayo kama ifuatavyo:
(i) Kuhakikisha
Vikao vya Kamati za Ulinzi na Usalama vya Mitaa, Vijiji na Vitongoji
vinafanyika mara kwa mara kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Serikali za
Mitaa katika kila Kata/Shehia kwa kuwashirikisha madiwani ili kujadili
na kubaini kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi.
(ii) Kufufua
mpango wa Daftari la Wakazi na Wageni katika kila Mtaa/Kitongoji kwa
Tanzania Bara na Zanzibar ili kila Kiongozi wa Mtaa, Kijiji na Kitongoji
ajue Watu wanaoishi katika himaya yake. Zoezi hili litasaidia kuepuka
tatizo la wageni wasiojulikana au wahamiaji haramu. Aidha kamati za
Ulinzi na Usalama za Serikali za Mitaa na Vijiji zinahimizwa kutekeleza
mkakati wa Halmashauri wa kuzuia uhalifu kwa kuimarisha vikundi vya
ulinzi shirikishi/ulinzi jirani, kwa kuzingatia Sheria ya Serikali za
Mitaa na Sheria Ndogo zilizotungwa ili kuimarisha usalama katika
Halmashauri husika.
(iii) Kuhimiza
wafanyabiashara wasaidiane na vikundi vya ulinzi shirikishi/ulinzi
jirani vilivyo kwenye maeneo jirani na biashara zao kama sehemu ya
kuimarisha usalama wa maeneo yao ya biashara. Pia, kwa wafanyabishara
wenye biashara kubwa zenye mikusanyiko ya Watu wengi wanaagizwa kufunga
“CCTV Camera” na kuziunganisha kimtandao na “Control Room” ya Polisi ili kutoa msaada wa kuzuia na kutanzua mapema uhalifu wowote utakaojitokeza.
(iv) Kuendelea
kuunda Zonal Task Force za Jeshi la Polisi katika kila Tarafa/Jimbo ili
kukusanya taarifa za uhalifu na kufanya operesheni za kuzuia uhalifu
katika kila Kata au Shehia zilizo ndani ya Tarafa husika. Kwa kufanya hiovyo tutaokoa maisha ya watu wengi.
(v) Kuendelea
kutoa elimu kwa jamii kuhusu mbinu mbalimbali za kuzuia na kupambana na
uhalifu kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari, mihadhara, mikutano,
maonesho na usambazaji wa machapisho na vipeperushi.
Mheshimiwa Spika,
83. Jukumu
la kuhakikisha Ulinzi na Usalama katika Nchi yetu ni letu sote. Kila
Mwananchi popote alipo anawajibika kushiriki kwa vitendo kwa kubaini
vitendo vyovyote vya uhalifu katika sehemu za kazi, biashara na maeneo
tunamoishi. Wito wangu kwa Waheshimiwa Wabunge wote, ni kuwaomba
tuwahimize Wananchi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha Nchi yetu
inadumu katika hali ya Amani na Utulivu.
IX: HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
84. Kwa
kuhitimisha, naomba nitumie nafasi hii ya mwisho kuwashukuru wote
waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa
Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Niwashukuru
Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza vikao vya Bunge lako
Tukufu. Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri na
kwa michango mbalimbali wakati wa Mkutano huu. Namshukuru Katibu wa
Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na
Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya
Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru
pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa
taarifa za majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia
Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri waliofanya ya
kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge,Viongozi mbalimbali,
Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.
Mheshimiwa Spika,
85. Nimalizie
kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi
na katika majimbo yenu. Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa hoja
kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 3 Desemba, 2013 saa
3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 14 kwenye Ukumbi huu hapa
Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
86. Naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment