Wakati wafuasi wa Tawi la Mwandiga, Kigoma
wakifanya maandamano kupinga kitendo hicho, wenzao wa Mbeya wameunga
mkono hatua hiyo.
Kigoma
Baadhi ya wanachama wa Mwandiga walichoma moto
kadi, bendera na fulana za chama hicho kupinga uamuzi wa kuvuliwa
uongozi kwa Zitto.
Wanadaiwa kufanya vurugu hizo baada ya maandamano
ya umbali wa kilomita tisa kutoka Mwandiga hadi Kigoma. Pia wanadaiwa
kubomoa ukuta unaotumika kubandika matangazo.
Wakizungumza katika eneo la Kituo cha Mabasi
Mwandiga, wanachama hao walisema Chadema kimekuwa na desturi ya kufukuza
viongozi wanaopigania haki na kupambana na ufisadi nchini hatua ambayo
walisema ni sawa na kudhoofisha jitihada za kupambana na uovu nchini.
Akisoma tamko lao, mmoja wa wanachama wa tawi
hilo, Rucha Bakari alisema wanachama wa Kigoma wamepokea kwa masikitiko
uamuzi wa chama kumvua madaraka Zitto na kusema jambo hilo linaua
harakati za Chadema kuingia Ikulu mwaka 2015.
“Chama kimemdhalilisha kiongozi wetu Zitto Kabwe.
Viongozi wa Chadema wamezidi kuonyesha ubabe na umangimeza dhidi ya
viongozi wanaopigania haki za kidemokrasia ndani ya chama na rasilimali
za chama,” inasema sehemu mojawapo ya tamko hilo na kuongeza:
“Walianza kwa kumfukuza Dk Aman Kabourou, David
Kafulila, Shaibu Akwilombe, Habibu Mchange, Juliana Shonza na Mtella
Mwampamba na sasa wamehamishia ukatili huo kwa mwanademokrasia, Jemedari
wa vita dhidi ya ufisadi, Zitto. Ili chama kiwe na amani tunataka
ufanyike mwafaka wa kitaifa ndani ya chama, vinginevyo tutachukua uamuzi
mgumu.”
Mmoja wa viongozi wa Baraza la Wanawake Chadema
(Bawacha), Jimbo la Kigoma Kaskazini, Stumai Omari alisema anapinga
uamuzi wa chama dhidi ya adhabu aliyopewa Zitto. Hata hivyo, alisema
bado ataendelea kuwa mwanachama wa Chadema.
Tawi la Mwandiga ndiko alipozaliwa Zitto na kisiasa ndipo ilipo ngome kuu ya Chadema katika Jimbo la Kigoma Kaskazini.
No comments:
Post a Comment