Pamoja na kwamba imepungua kidogo, bado kasumba ya kwamba hip hop ni
uhuni imeendelea kuwa na makazi kwenye akili za Watanzania wengi. Hata
kwa wazazi wengi, vijana wanaofanya hip hop wameendelea kuonekana kama
wahuni na wavuta bangi.
Japokuwa ni kweli kwamba maisha ya baadhi ya wana hip hop,yamekuwa
yakiipa nguvu zaidi kasumba hii, wapo rappers smart ambao kwa matendo
yao, maisha yao, elimu zao na mafanikio yao, akili walizonazo na namna
wanavyojua kujenga hoja, wameishinda nguvu kasumba hii.
Hawa ni miongoni mwa rappers hao.
Joseph Mbilinyi aka Sugu
Kutoka kwenye hip hop hadi bungeni. Sugu aliwaacha midomo wazi watu
wengi baada ya mwaka 2010 kushinda kiti cha ubunge wa Mbeya Mjini kwa
tiketi ya CHADEMA. Wakati wa kampeni, hata wapinzani wake walikuwa
wakitumia propaganda ya kumwelezea mbunge huyo kama mhuni, japo wananchi
wa Mbeya hilo hawakulijali. Tangu aingie bungeni, Sugu amekuwa mmoja wa
watetezi wazuri wa wananchi wa Tanzania na ni mtu mwenye hoja, na
mwanasiasa mzuri.
Profesa Jay
Profesa Jay
Unaweza kuwa umeshahau, lakini nyimbo za Profesa Jay, hususan, nyimbo
tatu zilizofuatana kimaudhui (trilogy) Ndio Mzee, Kikao cha Dharura na
Nang’atuka zilikuwa na ‘impact’ kubwa kisiasa nchini. Zilieleza hali
halisi ya jinsi wanasiasa walivyo na ahadi tamu wakati wa kampeni ambazo
hushindwa kuzitekeleza waingiapo madarakani. Unaanza vipi kuziita
nyimbo hizi ni za uhuni?
AY
Kutoka kuwa rapper hadi kuwa ‘business mogul’. Mwaka jana AY
aliishawishi kampuni ya Airtel Afrika kumteua kuwa balozi wake,
akiungana na wasanii wengine akiwemo Papa Wemba. Kama rap ingekuwa ni
uhuni siamini kama, kampuni kubwa kama hiyo ingempa heshima hiyo kubwa.
Leo hii AY, akiwa CEO wa Unity Entertainment, amekuwa akifanya
biashara na makampuni makubwa nchini na kukaa mezani na watu wenye
maamuzi katika makampuni hayo. “Tulianza tukiwa hatuna deal kabisa
ingawa tumefungua ofisi, leo hii tunahandle accounts za makampuni,” AY
aliiambia Bongo5 hivi karibuni kuhusiana na mafanikio ya kampuni yake.
Fid
Niliwahi kumuelezea Fareed kwenye makala yake mwenyewe (Makala: ‘Siri ya Mchezo’ ya kwanini Fid Q ni ‘Hip Hop Genius’)
ambapo sehemu ya yale niliyoandika yalisema: Wakati mwingine mawazo na
kile anachokiandika Fid Q, kinaweza kumfanya mtu anayechukua Phd ajihisi
mwanafunzi tu mbele yake. Pengine ni kwasababu, rapper huyu wa Mwanza
anapenda sana kusoma vitabu. Kutokana na ukweli kuwa, Watanzania wengi
hatuna utamaduni wa usomaji vitabu kujiongezea maarifa, ni ngumu
kuyafananisha mawazo yake na ya rapper mwingine yeyote Tanzania, hata
aliyesoma kiasi gani.”
Nick wa Pili
Hakupata nafasi ya kuwa mmoja wa wasemaji kwenye semina za fursa za
Clouds FM bure. Elimu yake na uwezo wa kupambanua mambo kisomi ndio
uliwavutia waratibu wa semina hizo na kumpa nafasi. Kwa wale
waliohudhuria semina hizo, wanajua upeo mkubwa wa rapper huyu wa Weusi.
Akiwa na shahada yake ya pili kibindoni, Nick wa Pili amedhamiria
kufanya makubwa.
“Nafikiria kufanya projects, nafikiria kuwa na media house ya kwangu,
nafikiria kuwa na NGO, na nafikiria kujiajiri kupitia muziki pia,” Nick
aliiambia Bongo5 hivi karibuni.
Mwana FA
Kutoka kuwa rapper hadi kuwa mwajiriwa benki, kuacha na kuwa
mjasiriahiphop. Hamis Mwinjuma ana shahada zake mbili kibindoni za
masuala ya biashara na amekuwa akionesha nia ya kutaka kuendelea na
kitabu zaidi. Akiwa na Vodacom na CCBRT, mwaka huu pia alizunguka kwenye
mikoa kadhaa nchini kwenye kampeni ya Fistula na alikuwa msemaji. Kama
hip hop ingekuwa uhuni, sidhani kama Vodacom wangempa heshima hiyo.
Roma Mkatoliki
Mashairi ya Roma hayapishani sana na makala za mwandishi kama Said
Kubeneya wa gazeti la Mwana Halisi. Tofauti ni moja tu kuwa ujumbe wa
Roma huwasilishwa kwa njia ya muziki. Tangu ameanza, nyimbo zake nyingi
zimekuwa zikigusa maisha na matatizo ya wananchi wa Tanzania na pia
kukemea maovu ya mafisadi na viongozi wabovu. Sidhani kama mtetezi kama
huyu anaweza kuitwa mhuni…
Kala Jeremiah
Kutoka Mwanza kwenye mitumba, hadi kuwa balozi wa Pepsi. Nyimbo
nyingi za Kala zimekuwa zikigusa maisha halisi ya Mtanzania na ndio
maana alifanikiwa kuwashawishi watu wa Pepsi. Kuanzia Wimbo wa Taifa,
Ningekuwa Rais, Dear God, Jaribu Kujiuliza na zingine.
“Ni hatua kubwa na jinsi gani sasa muziki wetu wa Hiphop unaeleweka
vizuri. Kama hip hop inaweza kushawishi makampuni kama hayo kuwekeza
nadhani inaeleweka,” Kala aliiambia Bongo5 baada ya kupewa ubalozi wa
Pepsi.
Source: Bongo5
No comments:
Post a Comment