Pages

Monday, November 4, 2013

MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA NCHI ZA KIARABU WAKUTANA CAIRO



Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za kiarabu jana wamefanya mkutano wa dharura kujadili suala la Syria katika makao makuu ya Umoja wa Nchi za Kiarabu mjini Cairo, Misri. 

Mawaziri hao wameyataka makundi ya upinzani ya Syria kuitikia juhudi za pande mbalimbali za kuhimiza kufanyika kwa mkutano wa pili wa Geneva kuhusu suala la Syria, na kupeleka ujumbe wake kwenye mkutano wa Geneva haraka iwezekanavyo. 


Kiongozi wa kundi muhimu la upinzani la Syria lililoko nje ya nchi hiyo National Coalition of Syrian Revolutionary and Opposition Forces Bw. Ahmed Jarba alihudhuria mkutano huo. 


Katika mkutano huo, mawaziri hao walijadili maendeleo ya hali nchini Syria na juhudi za jumuiya ya kimataifa na nchi za kiarabu katika kuhimiza kufanyika kwa mkutano wa pili wa Geneva. 


Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo inasisitiza kuwa, nchi za kiarabu zinaunga mkono kundi la National Coalition of Syrian Revolutionary and Opposition Forces, ambalo linaitaka jumuiya ya kimataifa iunge mkono kufanyika kwa mkutano wa pili wa Geneva na utekelezaji wa mpango wa kutatua mgogoro wa Syria kwa amani.

No comments:

Post a Comment