Pages

Sunday, November 3, 2013

museveni aishangaa tanzania

president-yoweri-museveni-of-uganda1 3fbf9
RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni ametetea mazungumzo ya kile kinachoitwa ushirika wa hiari unaohusisha nchi tatu za Uganda, Rwanda na Kenya, huku akiishangaa Tanzania kuhusu madai yake ya kutengwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Museveni alidhihirisha mshangao wake huo jana mjini hapa, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo yaliyowahusisha Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Katika kikao hicho, Museveni alidai majadiliano hayo ni sahihi kwa kuwa nchi hizo zinachojadili ni miradi ya miundombinu kwa ajili ya ukanda wa kaskazini.
Museveni alidai Tanzania itahusishwa wakati majadiliano yatakapohamia ukanda wa kusini, ambako ndiko lilipo taifa hilo lenye eneo kubwa zaidi miongoni mwa wanachama wa EAC.
Kauli kama ya Museveni pia ilitolewa na Rais Kenyatta wakati akizungumza na Wakenya waishio nchini Rwanda, akipuuza hofu iliyojengeka kuwa jumuiya hiyo inaelekea kuvunjika.
Rais Kenyatta alisema utekelezaji wa miundombinu ya kimaendeleo unaohusisha nchi hizo pamoja na Sudani Kusini, hauhujumu mtangamano wa jumuiya hiyo.
"Tumedhamiria katika malengo yetu ya mtangamano wa eneo hili na kulifanya listawi. Kwa sasa tunatarajia kaka na dada zetu wa Sudan Kusini kuungana nasi muda si mrefu na kuifanya EAC istawi na kuwa na nguvu zaidi," alisema.
Aliendelea kueleza kwamba, tofauti na kinachoelezwa na 'maadui' wa mtangamano wa EAC, wanachama wote wa jumuiya hiyo bado wamedhamiria kuungana.
"Kutokana na wasiwasi wa majirani zetu, niliamua kuchukua hatua zilizofanikisha kupunguza siku za kusafirisha bidhaa kutoka Mombasa kwenda Kigali kutoka siku 22 hadi nane," alisema.
Aidha alisema Serikali yake imeondoa vikwazo vyote vya usafirishaji mizigo na anatarajia mizigo itasafirishwa kwa kasi na urahisi zaidi katika nchi zote jirani.
Hata hivyo, viongozi hao walikwepa kuzungumzia suala nyeti zaidi ambalo nchi hizo katika mikutano miwili ya nyuma ziligawana majukumu ikiwamo kushughulikia suala la katiba ya shirikisho la kisiasa, viza moja, ushuru wa forodha na mengineyo ambayo yamo ndani ya mipango ya EAC.
Hivi karibuni, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta alieleza msimamo wa Serikali ya Tanzania kutokana na kitendo cha nchi hizo kujiundia utatu wa hiari ndani ya EAC.
Akijibu moja ya maswali ya wabunge mjini Dodoma hivi karibuni kuhusu mwelekeo huo unaotishia mustakabali wa jumuiya hiyo, Sitta alisema Serikali imeamua kutohudhuria mikutano yenye ajenda ambazo nchi hizo tatu zimeshaweka msimamo wa peke yao.
Sitta ambaye awali aliwahi kuonya kwamba kinachofanywa na nchi hizo ni kinyume na makubaliano na mkataba wa EAC, alienda mbali akisema Serikali imeshaanza mazungumzo na Burundi pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ili kuanzisha ushirikiano wao.
Aidha alifafanua kauli ya hivi karibuni ya waziri mwenzake wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, kwamba Tanzania inasubiri talaka, akisema yenyewe ndiyo yenye uwezo wa kutoa talaka kwa jumuiya hiyo kwa kuwa inamiliki asilimia 52 ya eneo lote, huku nchi zilizobakia zikigawana asilimia 48 iliyobakia.
"Hawa wenzetu wanafanya utoto wa kutuzunguka, sisi tunatumia hekima ya Mzee Mwinyi aliyesema 'mwongo, mwongoze.' Kama wao wana hila zozote juu yetu, siku si nyingi tutazibaini, kama ni ndoa ya kwenye jumuiya basi sisi ndiyo tutakuwa tumeoa. Hivyo tutatoa talaka sisi," alisema.
Hata hivyo, Rais Museveni alipoulizwa na mmoja wa wanahabari wakati wa mkutano wake mjini Kigali, alidai kuwa hana taarifa ya malalamiko yanayotolewa na Tanzania kuhusu utatu wa nchi zao.
"Hadi nitakapopata barua rasmi kutoka Serikali ya Tanzania ndipo nitakapoamini, vinginevyo nahesabu kile ninachoshuhudia katika vyombo vya habari ni uongo," alisema.
Hata hivyo, wanadiplomasia wa Tanzania wamekuwa wakieleza wasiwasi wao kuhusu kuachwa katika mipango ya jumuiya hiyo, wakisema haikualikwa kushiriki na wanatarajia kulifikisha suala hilo katika kikao cha wakuu wa EAC kitakachofanyika mjini Kampala, Uganda mwishoni mwa Novemba mwaka huu. Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment