Pages

Sunday, November 3, 2013

ZIto arudi na siri ya mabilioni ya uswisi


zkabwe1 2a089*Apanga kuanika aliyobaini Ulaya, ashtushwa na fedha zilizofichwa visiwa vya Uingereza
*Asema ni zaidi ya zile za Uswisi, ayageukia makampuni asema nayo yamo, aonya yakiachwa

MIEZI 12 tangu serikali iazimie kuunda timu maalumu kuchunguza sakata la vigogo wanaodaiwa kuficha fedha haramu nje ya nchi, hususani katika mabenki ya Uswisi, upepo wa suala hilo sasa unaweza kubadilika wakati wowote, baada ya muasisi wa hoja hiyo, Zitto Kabwe, kupanga kuibua mazito aliyodai kubaini katika uchunguzi wake Ulaya.

Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alirejea nchini jana akitokea katika nchi za Ulaya, baada ya kumaliza kazi ya kuongoza jopo la wataalamu kutoka Shirika la Kimataifa la Mtandao wa Ulaya wa Madeni na Maendeleo (Eurodad), kufanya uchunguzi kuhusu masuala ya uwazi katika kodi.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya mtandao akiwa nchini Ufaransa siku tatu zilizopita, Zitto alisema; "Huu uchunguzi ni mkubwa. Ni jambo kubwa sana. Nikimaliza kazi nitafanya press conference (mkutano na waandishi wa habari) ili kila Mtanzania aweze kujua, uchunguzi wa suala hilo ni mkubwa, hivyo kila Mtanzania anatakiwa kujua kinachoendelea," alisema Zitto kwa kifupi.
Gazeti hili lilipotaka kujua ni mambo gani hasa ameyabaini ambayo yanaigusa Tanzania moja kwa moja, likiwemo suala la idadi ya vigogo wanaotajwa kuficha fedha chafu nje ya nchi, Zitto bado alisisitiza azma yake ya kukutana na waandishi wa habari, huku akitoa angalizo kuwa inatupasa kuwa makini.
Nikimaliza kazi nitafanya 'press conference' siku ambayo nitatangaza ili kila Mtanzania aweze kujua, ninarudi Novemba 2. Uchunguzi ni mkubwa sana na lazima tuwe makini sana," alisema.
Alisema akiwa huko alikutana na watu waliokuwa wanafanya kazi kwenye mabenki ya Uswisi na Mauritius, ambao alisema kuwa wana taarifa nyeti sana.
Zitto, ambaye wakati anawasiliana na gazeti hili alikuwa mjini London, nchini Uingereza, alisema akiwa hapo alikutana na mchunguzi mwingine kwa ajili ya akaunti za visiwa vya Jersey, Isle of man, Guarnsey, Cayman na kisiwa cha British Virgin, ambako imebainika kuna fedha nyingi zaidi kuliko zile za Uswisi.
Alibainisha kuwa fedha za watu binafsi ni chache kuliko makampuni makubwa yanavyokwepa kodi nchini.
Watu binafsi ni rahisi kuwashughulikia na kurejesha fedha zilizopatikana kwa wizi, rushwa na biashara ya madawa ya kulevya. Kazi kubwa ipo kwa makampuni ya kimataifa ambayo yanakwepa kodi zaidi ya dola 546 milioni kila mwaka," alisema Zitto.
Katika kushughulikia suala hilo la utoroshwaji wa mabilioni ya fedha nchini, Zitto alisema kuwa ni vyema makampuni nayo yasisahauliwe.
Akili za watu wengi sasa ni kwa watu binafsi, lakini tusipokuwa makini tutayaacha makampuni yakiendelea kunyonya rasilimali zetu na kutolipa kodi," alisisitiza Zitto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kwa upande wa kampuni za madini, alisema tangu mwaka 2001 mpaka 2011 zimeuza nje ya nchi madini ya dola 11.3 bilioni, lakini wamelipa kodi dola 440 milioni, ambayo ni chini ya asilimia nne ya mauzo yao yote.
Kwa mujibu wa maelezo yake, idadi hiyo ni mbali na makampuni ya simu na sekta nyingine ambapo ametilia shaka serikali kupoteza fedha nyingi kwa mtindo huo.
Inaelezwa kuwa takwimu za mtiririko wa fedha haramu zinazofichwa nje zikitokea Afrika ni mara mbili ya kiasi cha fedha za msaada zinazotolewa kwa bara hili.
Shirika la Kimataifa la Fedha la Global Financial Integrity, linakadiria kuwa kiasi cha dola trilioni 1.4 zilihamishwa kutoka Afrika katika kipindi cha miongo mitatu (1970 mpaka 2009).
Katika kipindi hicho, mikopo ya Afrika ilikuwa chini kuliko fedha haramu zinazohamishwa.
Inakadiriwa kuwa kila mwaka, Afrika inaingia hasara ya dola bilioni 50 katika ukwepaji wa kodi.
Hatua hiyo ilisababisha Nicholous Shaxson kuandika katika kitabu chake "Treasure Islands" kwamba; huwezi kuelewa umaskini barani Afrika pasipo kujua jukumu la Kodi ya Bandari.
Utafiti huo pia unaonyesha kuwa katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, fedha zilizofichwa nje ya nchi ni Dola za Marekani 7,967.4 milioni (sawa na Sh 12.7 trilioni).
Zitto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kwa muda mrefu amekuwa akipigia kelele suala hilo ambapo Novemba 9 mwaka jana, katika mkutano wa Bunge aliwasilisha hoja binafsi ya kulitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza serikali hatua dhidi ya raia wa Tanzania walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.
Hata hivyo, Bunge liliazimia serikali ifanye uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo na kuwasilisha ripoti yake katika mkutano wa Bunge wa Aprili mwaka huu, jambo ambalo haijaweza kulitekeleza mpaka sasa.
Gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel, kujua ilikoishia ripoti hiyo ya uchunguzi unaofanywa na serikali. Alisema Spika wa Bunge, Anne Makinda, katika kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge kilichofanyika kabla ya kuanza kwa shughuli za Bunge linaloendelea sasa mjini Dodoma, aliikumbusha serikali kuhusu kuleta ripoti hiyo.
"Spika katika kikao cha Kamati aliagiza serikali ilete taarifa, hivyo siwezi kujua, lakini kama ni taarifa tu ya serikali muda huo utapatikana," alisema Joel.
Alipoulizwa iwapo pia Zitto anaweza kuwasilisha taarifa yake ya Eurodad katika Bunge hili, alisema haitawezekana, kutokana na utaratibu wa Bunge kuwa mwisho wa kuwasiliswa hoja ni siku moja kabla ya kuanza kwa Bunge.
"Sidhani, kwa utaratibu wetu hoja zinatakiwa ziwasilishwe siku moja kabla ya kuanza, labda kama ataleta na atakabidhi kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya Bunge lijalo," alisema Joel.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, ambaye mara kadhaa amekaririwa akisema kuwa ripoti kuhusu mabilioni ya fedha ipo tayari, alipotafutwa mara kadhaa na gazeti hili kujua lini itafikishwa bungeni, ameonekana kutopenda kuweka wazi suala hilo.
Zitto aliteuliwa mwezi uliopita kuongoza jopo la wataalamu kutoka Eurodad, ambao ni Mtandao wa Mashirika yasiyo ya kiserikali yapatayo 48 kutoka nchi 19 za Ulaya, ambayo yanajihusisha na masuala ya kufutia madeni nchi zilizoendelea, misaada yenye maana na kodi za haki, kufanya uchunguzi kuhusu masuala ya uwazi katika kodi.
Mashirika hayo yamekuwa kwenye kampeni ya kupinga utoroshwaji wa fedha kupitia ukwepaji kodi unaofanywa na mashirika ya kimataifa kwa nchi zinazoendelea.
Uchunguzi huo uliofanywa katika nchi za Ulaya, ulianza Oktoba 20 na ulitarajiwa kukamilika Novemba 5, mwaka huu kwa kuandika ripoti yake. Cjanzo: Rai

No comments:

Post a Comment