TAARIFA KWA UMMA
KUKOMA KUWA KIONGOZI KWA MWENYEKITI WA WILAYA YA MONDULI MCHUNGAJI AMANI SILANGA MOLLEL
Kwa niaba ya baraza la uongozi la mkoa wa Arusha, napenda kuujulisha
umma wote kwa ujumla kuwa mwenyekiti wa wilaya ya monduli Mchungaji
Amani Silanga Mollel amekoma/amesimamishwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA
wilaya ya monduli kuanzia tarehe 29 Novemba 2013 kufuatia tuhuma nzito
za uvunjifu wa kanuni za maadili ya chama.
Hatua hii imefikiwa baada ya kuthibitika na yeyé mwenyewe kukiri mbele
ya kikao cha kamati tendaji ya wilaya ya monduli kilichoketi tarehe 29
Novemba 2913 saa NNE asubuhi kuwa alitoa tamko batili akitumia wadhifa
wa mwenyekiti wa wilaya bila ridhaa ya kamati tendaji na huku
akidanganya kuwa ni tamko kwa niaba ya wilaya ya Monduli.
Katika tamko lake ametoa tuhuma dhidi ya wajumbe wa kamati kuu na
viongozi wakuu wa kitaifa kwa maamuzi halali ya kikao cha kamati kuu
huku akijua kuwa anavunja kanuni za chama kwa mujibu wa katiba ya chama
toleo la mwaka 2006 ya Kanuni za uendeshaji kazi za chama, sura ya KUMI,
ibara ya 10 (X) “Kiongozi asitoe tuhuma zozote juu ya viongozi
wenzake pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi
zilizoelezwa kwenye kanuni za chama”.
Sambamba na hilo, Mchungaji Amani Silanga ametoa tuhuma za uzushi, uongo
na upotoshaji na kutaka kuaminisha jamii kuwa chadema ina makundi ya
CHADEMA Asili na CHADEMA Family kitu ambacho ni upotoshaji mkubwa na wa
hatari kwa ustawi na umoja wa chama na kinyume na kanuni za uendeshaji
kazi za chama, sura ya KUMI, ibara ya 10 (VII), “Kiongozi anatakiwa
kuwa mkweli na muwazi wakati wote hususani katika vikao halali na
aachane na vikundi vya majungu, wadanganyifu (Rumour Mongers). Ni mwiko
kwa kiongozi kujihusisha na upotoshaji wa maamuzi wa vikao halali”.
Kamati tendaji ya wilaya ilipomtaka aonyeshe CHADEMA asili ni kina nani
na CHADEMA family ni kina nani alishindwa kutoa maelezo yoyote ya maana
na kufikia hatua ya kutaka kuvuruga kikao kwa kuleta vijana wahuni
wapatao 17 ndani ya kikao ambao wengi walijulikana kuwa sio WANACHADEMA.
Katika utambulisho wake wa majigambo Mchungaji Amani SIlanga kwa kiburi
na kejeli amejitambulisha na kukiri kuwa yeye yupo kambi ya Zito Kabwe
na hakuna wa kumfanya kitu maana ni mjumbe wa baraza kuu la chama.
Maneno yake yalidhihirisha kuwa Mchungaji Amani Silanga anashiriki
mpango wa kuunda makundi yasiyo na tija ndani ya chama na hivyo kuwa
kinyume na sura hiyo hiyo ya kumi ya kanuni za uendeshaji kazi za chama
ibara ya 10 (IX), “Kiongozi asijihusishe au kushiriki na vikundi au
vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au
wanachama wake”.
AZIMIO LA BARAZA LA UONGOZI LA MKOA WA ARUSHA:
Baraza la uongozi la mkoa lililoketi tarehe 29 Novemba 2013, limepokea
mapendekezo ya kamati tendaji ya wilaya na kuzingatia hofu kubwa
iliyoainishwa na kamati tendaji kufuatia matendo mengi yanayotia shaka
ya uadilifu na uwezo wa kiuongozi wa Mchungaji Amani Silanga na hivyo
baraza la uongozi la mkoa limeridhia kuwa amevunja kanuni za maadili ya
chama sura ya KUMI ibara ya (VII) hadi (XII) na hivyo kupelekea ukomo wa
yeye kuwa Mwenyekiti wa wilaya kuanzia tarehe 29 Novemba 2013. Baraza
la mkoa likiwa mamlaka ya nidhamu kwa mujibu wa katiba ibara ya 6.3.6
(a) (iv) limemjulisha tuhuma zake na hatua hii stahiki iliyochukuliwa.
Kwa vile Mchungaji Amani Silanga alikiri kosa hili mbele ya kamati
tendaji ya wilaya bila kulijutia au kuomba msamaha, baraza la mkoa
limechukua hatua hii stahiki kwa maslahi ya chama na kuwa uchunguzi
zaidi utafanyika ili kufikia maamuzi makubwa zaidi ya tuhuma nyingi kwa
mujibu wa kanuni za hatua za kinidhamu.
Baraza la uongozi la mkoa wa Arusha, linatoa onyo kwa wote ambao wapo
katika mtandao huu mchafu, ama watoke wenyewe mapema maana
hawatavumiliwa kamwe. Baraza la uongozi wa mkoa liliona kuwa Mchungaji
Silanga amepotoka na hivyo yeyé kuendelea kuwepo ndani ya chama wakati
wa uchunguzi wa tuhuma hizi nzito dhidi yake ni hatari zaidi kwa ustawi
wa chama na hivyo baraza likaridhia kwa kuzingatia tafsiri ya katiba ya
chama ibara ya 6.3.4 (c) wa yeyé kukoma uongozi na hivyo akae nje kwa
muda na waliopotoka wenzake.
Amani Golugwa
Katibu wa CHADEMA – Mkoa wa Arusha.
(Kwa niaba ya Baraza la Uongozi la Mkoa wa Arusha)
Tarehe 30 Novemba 2013
No comments:
Post a Comment