Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Malawi na
Tanzania zimewasilisha ushahidi na majibu ya maswali kuhusu umiliki wa
maeneo kwenye Ziwa Nyasa, kwa jopo la wasuluhishi linaloongozwa na Rais
mstaafu wa Msumbiji Joachim Chissano.
Wasuluhishi hao walizitaka Malawi na Tanzania
kutoa majibu ya maswali manne muhimu, wakati wakiwasilisha ushahidi wao
kuhusu umiliki wa ziwa hilo wenye mgogoro.
Mgogoro huo uliibuka baada ya Serikali ya Malawi
bila kushauriana na Tanzania kutoa leseni kwa kampuni mbili za kigeni,
kutafuta mafuta katika eneo la ziwa ambalo linamilikiwa na Tanzania.
Kwa mujibu wa gazeti la mtandaoni la Malawi la
Nyasa Times, msemaji wa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa
wa Malawi, Quent Kalichero alithibitisha Jumatano wiki hii kwamba nchi
hiyo imewasilisha majibu ya maswali hayo na ushahidi uliohitajika.
“Waziri wetu amewasilisha taarifa maalumu ya
maandishi kwa wasuluhishi na kwa sasa yuko nchini Msumbiji, kwa ajili ya
suala hilo,” alisema Kalichero juzi.
Makabidhiano hayo yalifanyika mjini Maputo,
Msumbiji ikiwa ni siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya
mazungumzo na wasuluhishi, marais wa zamani wa Msumbiji, Joachim
Chissano na wa Botswana, Festus Mogae jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mkutano huo wa Jumatatu mjini
Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa
Tanzania, Bernard Membe aliwaeleza wanahabari kwamba mazungumzo baina ya
Rais Kikwete na wasuluhishi hao yalihusu zaidi ushahidi wa Tanzania
katika suala la umiliki wa Ziwa Nyasa.
Pia alithibitisha kwamba Tanzania ilikuwa tayari
kuwasilisha ushahidi wake kwa sekretarieti ya ofisi ya waliokuwa wakuu
wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) inayoongozwa
na Chissano, Jumatano iliyopita.
Baada ya mkutano huo wa Jumatatu, Membe alieleza
kwamba nchi zote husika, yaani Tanzania na Malawi zinatakiwa kuheshimu
maagizo na kuwasilisha ushahidi huo kwa wakati, na kuwaachia wasuluhishi
kazi ya kupitia na kutekeleza wajibu wao wakiwa wamepewa muda unaofikia
mwaka mmoja kupata suluhu.
Wasuluhishi hao wa Sadc, Chissano na Mogae
waliwasili jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita kwa ajili ya
mazungumzo kuhusu mgogoro huo, kama walivyofanya kwa Malawi Julai mwaka
huu.
Julai mwaka huu, Rais Joyce Banda wa Malawi
alinukuliwa akisema kuwa nchi yake haina nia ya kulegeza kamba katika
mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na Tanzania.
Alitoa msimamo huo baada ya kukutana na Chissano
wa Msumbiji na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini ambao ni wajumbe maalumu wa
Jumuiya ya Sadc katika mgogoro huo.
Alisema kwamba madai ya Tanzania kuwa inamiliki sehemu ya Ziwa
Nyasa, siyo ya kweli na kwamba mpaka uko ufukweni mwa ziwa hilo upande
wa Tanzania.
Rais Banda alidai kuwa nchi yake inafuatilia kwa
karibu upatanishi wa SADC na kwamba isiporidhishwa na uamuzi ya jumuiya
hiyo italiwasilisha suala hilo Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ).
Kabla ya hatua hiyo ya Malawi, Aprili mwaka huu
Serikali ya Tanzania iliitaka nchi hiyo kuacha kutapatapa na kuonya kuwa
kamwe isithubutu kugusa eneo hilo la mpaka.
Akitoa kauli ya Serikali ya Tanzania Membe
alisema: “Nadhani watasikia na kuelewa, Serikali ya Malawi iache
kutapatapa, nchi zote ilikoenda kulalamika kuhusu mgogoro huu, Tanzania
tumekuwa tukielezwa na hata hao wanaotueleza wanaishangaa sana Malawi.”
Kauli hiyo ya Serikali ilifuatia Rais Banda kusema kuwa mgogoro huo sasa
utapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kwa madai kwamba
juhudi za usuluhishi wa kidiplomasia zimeshindikana.
Hata hivyo, uamuzi huo wa Malawi ni kinyume na
makubaliano baina ya nchi hizo mbili yaliyofanyika Novemba 7 mwaka jana,
jijini Dar es Salaam ambapo zilikubaliana kwamba jopo hilo ndiyo sehemu
ya mwisho ya makubaliano.
Katika maelezo yake, Rais Banda alisema nchi yake
imejitoa katika mazungumzo ya usuluhishi kwa madai ya kuhujumiwa na
katibu wa jopo hilo ambaye ni Mtanzania, John Tesha kwa maelezo kuwa
anavujisha taarifa muhimu za Malawi kwa Tanzania kabla ya Tanzania
haijawasilisha taarifa zake kwa jopo hilo. Alisema kuwa tangu kuibuka
kwa mgogoro huo, Malawi imekwenda kulalamika katika nchi za Uingereza,
Marekani, Umoja wa Afrika (AU) na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (Sadc).
Hata hivyo, baadaye Julai mwaka huu, Serikali ya
Malawi ilitangaza kuwa itaendelea na mazungumzo na Tanzania kuhusu mpaka
huku ikieleza kuwa viongozi wa Tanzania hawaelewi mipaka ndiyo maana
wanapigania kuwa wao ni sehemu ya ziwa.
Waziri wa Habari wa Malawi, Moses Kunkuyu
aliliambia Shirika la Utangazaji la Malawi (MBC) kuwa viongozi wote wa
Tanzania wanadhani wanamiliki Ziwa Malawi (Nyasa) lakini watakuja
kubaini baadaye kuwa hawana hata tone la umiliki.
CHANZO MWANANCHI
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment