Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bw.Philipo Mulugo,akifafanuliwa
jambo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya
Ufundi(NACTE)Dkt.Primus Nkwera(kulia)kabla ya kufungua mkutano wa kwanza
Kitaifa wa wakuu wa vyuo vya ufundi,Serikali na wadau wengine wa elimu
ya ufundi,Mkutano huo wa siku tatu unafanyika katika ukumbi wa mikutano
wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu, Arusha
NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Philipo Mulugo, amesema kuanzia mwaka wa masomo 2014/15 vyuo
vyote vya ufundi nchini vinaendesha mafunzo ya kozi zenye ithibati tu
ili kuondoa usumbufu kwa wahitimu.
Aidha ametangaza rasmi kuanza kwa
mtaala wa Stashahada ya Elimu ya Msingi ambao utaanza kutekelezwa kwa
vyuo vilivyo na sifa kuanzia mwaka wa masomo wa 2014/15.
Akifungua mkutano wa kitaifa wa
wakuu wa vyuo vya ufundi nchini ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu
ya Ufundi (NACTE) na kufanyika jijini hapa, atalazimika kutumia polisi
kukagua na kuvifunga vyuo ambavyo wamiliki wake wanashindwa kutekeleza
masharti ya vyuo vyao kupata ithibati.
“Siku hizi kumeibuka wimbi kubwa la vyuo holela vinavyoendeshwa pasipokuzingatia vigezo vilivyowekwa na NACTE.
“Jamii yetu imeendelea kuhujumiwa
na watu wanaojitafutia fedha kwa njia za mkato na hasa wanaojitangaza
kutoa Elimu ya Ufundi tena kwa ada ndogo,” alisema.
Aliwaasa wazazi na walezi kabla ya
kuwapeleka watoto wao kujiunga na vyuo vya ufundi wahoji mambo muhimu
ikiwa ni pamoja na usajili wa vyuo hivyo, taaluma za wakufunzi wake ili
wawe na uhakika na taalum inayotolewa kwa watoto wao.
Aliliagiza Baraza hilo, “ikiwa
katika kutekeleza agizo langu mtakutana na kikwazo cho chote basi ofisi
yangu ambayo ni mamlaka ya rufaa kwa mujibu wa sheria yenu itatoa
ushirikiano kuhakikisha tatizo la kozi zisizotambuliwa linadhibitiwa kwa
nguvu zote.”
Alisema kabla ya kuanzishwa NACTE,
serikali haikuwa na chombo mahsusi cha kuratibu elimu na mafunzo ya
ufundi hali ambayo ilisababisha kila mwenye chuo kujiwekea vigezo na
viwango vyake vya taaluma na hivyo kusababisha nchi kuwa na vyuo ambavyo
vinatoa tuzo ambazo vigezo vyake havilingani.
“Kila mwenye chuo alikuwa
akitayarisha mtaala wake wa mafunzo kama alivyoona inafaa, na hivyo,
kusababisha utofauti wa viwango vya tuzo zinazotolewa baina ya chuo
kimoja na kingine,” alisema.
Alisema katika mfumo wa soko huria
na kutokana na kiu ya Watanzania kupata elimu ya ufundi, ilikuwa ni
rahisi kudanganywa na kupewa elimu duni na pia ilikuwa vigumu kwa
serikali kuweka mikakati ya kuendeleza Elimu ya Ufundi ili kukidhi
mahitaji ya maendeleo ya nchi na watu wake.
Katibu Mtendaji wa NACTE, Dk.
Primus Nkwera, alivitaka vyuo na taasisi za elimu za ufundi nchini
zinazotoa mafunzo bila kusajiliwa pamoja na wale wote wenye nia ya
kuanzisha vyuo vipya kuhakikisha vyuo vyao vinapata usajili kutoka
Baraza hilo kwa mujibu wa sheria.
“Baraza linapenda kuwasisitizia
wadau wote ikiwemo wazazi, wanafunzi na umma kwa uiumla kujiunga na vyuo
vilivyosajiliwa na Baraza na si vinginevyo,” alisema.
Alisema matarajio ya soko la ajira
ni kuona vyuo vinatoa wahitimu wenye ujuzi na maarifa yanayokidhi
viwangao vya utendaji kazi katika taaluma husika.
Mwenyekiti wa NACTE Mhandisi
Steven Malote, alisema baraza hilo limeweka mfumo wa tuzo za kitaifa za
Elimu ya Ufundi ambazo zimeunganishwa na Tuzo za Kitaifa za Ufundi Stadi
(NVA), ili kuwa na ngazi kumi za Mfumo wa Kitaifa wa Elimu ya Ufundi na
Ufundi Stadi (TVET).
Pia alisema imewaka kanuni za usajili na ithibati pamoja na masharti ya vyuo/taasisi kuanzisha kozi za shahada.
No comments:
Post a Comment