Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, November 29, 2013

Ryan Giggs atimiza miaka 40.Soma historia yake katika soka.


LEO ni siku ya kuzaliwa ya Ryan Giggs ambaye alizaliwa Novemba 29, 1973, hiyo ikiwa na maana kuwa alianza kuliona jua miaka 40 iliyopita, Gazeti la Championi linamtakia kheri mchezaji huyo wa Manchester United, soma stori nzuri inayomuhusu:
Ferguson alivyomsajili kimafia
Kuanzia mwaka 1985, Giggs alikuwa akiichezea timu ya watoto ya Manchester City, nyuma ya pazi kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson alikuwa akimfuatilia kupitia watu wake wa kutafuta vipaji.
Baada ya kujiridhisha kuwa Giggs anaweza kuwa chaguo zuri kwa timu yake, Ferguson alichofanya kwa kuwa ‘dogo’ huyo alikuwa hajafikisha umri wa kusaini mkataba, akaamua kwenda moja kwa moja kwa mama yake mzazi na kumshawishi  juu ya kumchukua mwanaye.
Ferguson akamwambia mama huyo kuwa licha ya kuwa atakuwa mwalimu wa Giggs lakini atakuwa kama mzazi wake, akaahidi kuwa atamuangalia ndani na nje ya uwanja, pamoja na ahadi nyingine nyingi, mama mtu akakubali, Man United ikamnasa Giggs kilaini.
Hivyo, Giggs alitua klabuni hapo baada ya mama yake kumkabidhi mikononi mwa Ferguson na kuanza maisha klabuni hapo kuanzia mwaka 1987 ambapo yupo mpaka leo.
Achapwa makofi na Ferguson
Baada ya kufika United, Giggs akaendelea na maisha kama kawaida katika timu ya watoto, baadaye ndipo akapata marafiki kina David Beckham, Phill Neville, Paul Scholes, Gary Neville na wengine wengi, lakini yeye Giggs ndiye aliyekuwa mkubwa kuliko wote katika rika la vijana hao.

Kuna siku Giggs akiwa tayari ana miaka kadhaa klabuni hapo, akawaita wachezaji wenzake huku akiwa na rafiki yake wa kike nyumbani kwake na kufanya sherehe kubwa, katika sherehe hiyo, wachezaji hao walifungulia muziki kwa sauti kubwa huku wakinywa na kula kwa raha zao.
Kuna mama mmoja ambaye alikuwa jirani yake na Giggs, akawa anasikia kila kitu kinachoendelea, akampigia simu Ferguson na kumuelezea juu ya wanachofanya ‘watoto’ wake, kocha huyo akamshukuru huyo mama, akawasha gari kuelekea nyumbani kwa Giggs.
Alipofika akagonga, kijana mmoja akafungua mlango, ile anamuona mzee huyo, akashtuka sana, kidogo amzuie kuingia ndani, Ferguson akaingia na moja kwa moja akafika mpaka kwa Giggs, akamwambia azime muziki, Giggs akatekeleza hilo.
Baada ya kuzima muziki, Ferguson akamgeukia Giggs na kumnasa makofi palepale mbele ya wenzake na rafiki yake wa kike ambaye baadaye alikuja kuwa mke wa mchezaji huyo.
“Wewe Ryan ndiyo mkubwa hapa, unawaongoza wenzako kufanya upuuzi, huu ndiyo mwisho wa muziki na kila mtu asambae hapa, na kesho ole wake atakayechelewa mazoezini,” hiyo ilikuwa ni kauli ya Ferguson aliyoitoa hapo, bila ubishi vijana hao wote wakasambaa wakiwa vichwa chini.

Maisha ya sasa
Mpaka sasa Giggs ameshacheza mechi 952 na bado ana mkataba mpaka mwisho wa msimu huu kuendelea kuitumikia Man United.
Mapema wiki hii aliulizwa juu ya kufikiria kustaafu, lakini Giggs akasema bado hajafikiria juu ya kustaafu kwa kuwa hiyo inategemea na mwili wake utakavyokuwa wakati muda wa mkataba wake utakapomalizika.
“Nina machaguo mengi, nina biashara kadhaa ninafanya, nina cheti cha ukocha, hivyo naweza kuwa na chaguo moja kati ya hivyo.
“Nafikiria pia kucheza mpaka nitakapofikisha mechi 1,000 lakini hilo litategemea na nitakavyokuwa nikijisikia wakati huo,” anasema kiungo huyo raia wa Wales.

Kuhusu kuyumba kwa Man United
“Nafikiri ni suala la benchi la ufundi na wachezaji, tutakaposhinda au kufungwa tunakuwa ni wote, taratibu muda unavyosonga ndivyo tutavyokuwa imara,” anasema. Akielezea kuhusu umri wake wa sasa, Giggs anasema: “Nimekuwa nikifikiria jinsi ninavyojisikia na siyo kuhusu umri, kuna wakati wachezaji wenzangu wananiambia ninazeeka, nawajibu kuwa umri wangu ni miaka 35 (anacheka).”
Kuonyesha kuwa bado mchango wake unahitajika, kocha wa sasa wa United, David Moyes tayari ameshaanza kuweka wazi nia yake ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja Giggs.

Kama mkataba huo utasainiwa, maana yake ni kuwa ataendelea kuichezea United mpaka atakapofikisha umri wa miaka 41.
Giggs ambaye ana urefu wa futi 5.11, amekuwa hapati nafasi mara kwa mara katika kikosi kinachoanza, badala yake amekuwa akianzia benchi huku akimsaidia Kocha Mkuu David Moyes kwenye benchi la ufundi.
Wakati anachipukia, winga huyo alikuwa na kasi ya kukimbia kiasi kwamba alikuwa tishio kwa mabeki wengi wa timu pinzani, kwa sasa ambacho amekuwa akifanya ni kutulia na mpira kwa kuwa hana kasi kama ambayo aliyokuwa nayo miaka ya zamani.
Jambo jingine ambalo linawashangaza wengi ni kuwa kile kizazi chote ambacho kilimkuta mchezaji huyo kwenye klabu hiyo, wote wameshastaafu lakini yeye bado anacheza.
Upande wa timu ya taifa, Giggs ameichezea timu ya taifa ya Wales mechi 64 na kufunga mabao 12, wakati ambapo timu ya taifa ya Uingereza ameichezea mechi nne na kufunga bao moja.
“Bado anaonekana yupo vizuri, siyo mtu ambaye ukimtazama unadhani kuwa ataacha kucheza hivi karibuni,” anasema Moyes na kuongeza:
 “Tayari ameanza kuelekea kwenye ukocha, unapoona mchezaji anachukua maamuzi hayo maana yake ni kuwa anajua muda wa kucheza umebaki kidogo.”chanzo GPL



No comments:

Post a Comment