SIKU chache baada ya Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya
(CCM), kudaiwa kutoweka nchini kukwepa mkono wa sheria dhidi ya tuhuma
za kutishia kumuua binti anayedaiwa kumbaka, vigogo wa polisi wanadaiwa
kuhusika kumsaidia kutimkia nje,
Habari ambazo gazeti hili limezipata, zinaeleza kuwa siku mbunge huyo
akikamilisha taratibu za kusafiri, ndiyo siku ambayo Jeshi la Polisi
Mkoa wa Kinondoni lilikuwa limekamilisha kufungua jalada la tuhuma zake
na liliweka mtego wa kumnasa.
“Wakati Polisi Kinondoni wakiweka mtego wa kumnasa, baadhi ya polisi
walimjulisha na hata kumsaidia kuhakikisha anasafiri nje ya nchi,”
alisema mmoja wa maofisa wa juu wa polisi nchini.
Hata hivyo, kuna utata na kauli zinazopingana kuhusu mbunge huyo.
Taarifa nyingine zinasema kuwa mbunge huyo ambaye amepata kuwa waziri,
anadaiwa kusafiri kwenda nchini Sweden kwa masuala ya kikazi, na kwamba
atakuwepo huko kwa muda usiopungua mwezi mmoja.
Chanzo kingine kimedokeza kuwa mbunge huyo alidai ametumwa kazi na
kigogo mmoja serikalini na atakuwepo nchini humo miezi miwili hadi
mitatu.
Hata hivyo, haijajulikana kazi anayokwenda kuifanya Kapuya ingawa kuna
taarifa safari hiyo imelenga kutuliza upepo mbaya wa kuandamwa na tuhuma
za ubakaji ambazo zipo polisi hivi sasa.
Tayari Profesa Kapuya alishafunguliwa jalada namba OB/RB/21124/13 katika Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam juzi.
Hata hivyo Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa linamsaka mbunge huyo ndani na nje ya nchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alikaririwa juzi
kuwa watamtafuta Kapuya nchi yoyote atakayokwenda iwapo tuhuma dhidi
yake zitathibitika.
Alisema mtandao wa polisi ni mkubwa, hivyo si rahisi kwa mtuhumiwa
yeyote kuukwepa mkono wa sheria endapo itahitajika kufikishwa kwenye
vyombo vya sheria.
“Sisi tunashirikiana na polisi wa nchi mbalimbali duniani, ndiyo maana
inakuwa rahisi kwa mtuhumiwa aliyetoroka nchi fulani kukamatwa nyingine
na kurejeshwa kwao.
“Nataka niwaondoe hofu wale wote wanaodhani polisi haiwezi kumkamata mtu
akikimbia nchini, tuna mkono mrefu sana, na hatufanyi kazi kinyume na
taratibu zetu,” alisema.
Kamanda Wambura pia alikiri polisi kufungua jalada la Kapuya, huku
akiweka wazi kuwa kinachofanyika hivi sasa ni uchunguzi wa tuhuma zake.
Alisema miongoni mwa maeneo wanayoyafanyia uchunguzi ni kubaini kama
ujumbe ulio katika simu ya binti anayedai kubakwa na kutishiwa maisha
unatoka katika simu ya mbunge huyo.
“Tumefungua jalada, lipo kwa ajili ya uchunguzi na tukibaini kuwa ni
nani anahusika na tuhuma hizo tutamsaka na kumkamata popote alipo,”
alisema Wambura.
Gazeti hili limekuwa likiandika namba ya simu ya Prof. Kapuya ambayo
huwa anaitumia kutuma ujumbe wa vitisho kwa binti huyo, ingawa kuna
vyombo vingine vya habari viliamua kuandika kwa mtazamo tofauti na
kumtuhumu dada wa binti aliyebakwa kuwa ni mtu mzima na kuwa ana
uhusiano na Kapuya, na wana watoto.
Simu hiyo namba 0784993930 inayodaiwa kumilikiwa na Profesa Kapuya,
mbali ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno ya kutishia kuua, pia ndiyo
inayodaiwa kutumika kutuma pesa kwa njia ya mtandao kwenda kwa binti
huyo.
Tangu gazeti hili lianze kuandika tuhuma hizi nzito, kumekuwapo na
kusuasua kwa mtuhumiwa huyo kutiwa hatiani na Jeshi la Polisi.
Harakati za kufungua jalada dhidi ya Kapuya zilizoanza wiki iliyopita
ziliendelea hadi juzi ambapo polisi walitumia zaidi ya saa 12 kumhoji
binti huyo anayedaiwa kubakwa ili kupata ukweli wa sakata hilo.
Akiwa polisi, binti huyo alikutana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi
ya Oysterbay (OCD) na OC-CID wake na kutoa maelezo ya awali kabla ya
viongozi hao kumruhusu ayaweke malalamiko yake katika maandishi kwa
ajili ya kufunguliwa mashitaka.
CHANZO tanzania daima
No comments:
Post a Comment