WAKATI nchi ikiendelea kuandamwa na zimwi la kuporomoka kwa majengo,Tanzania Daima Jumapili limebaini udhaifu mkubwa kwenye Bodi ya Makandarasi (CRB).
Uchunguzi wa gazeti hili kwa takribani wikimbili,
umejiridhisha pasipo shaka kwamba CRB imeisajili Kampuni ya Visual
Storm Co. Ltd kwa kutumia nyaraka bandia na imekuwa ikitekeleza miradi
mikubwa bila kuisajili kwenye bodi hiyo kama sheria inavyosema.
Kampuni
hiyo inamilikiwa na Noel Severe (30), mtoto wa mkurugenzi wa zamani wa
wanyamapori, Emmanuel Seveve ambaye wakati fulani aliingia kwenye
mgogoro wa kiuongozi wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo.
Severe
ni mkwe wa waziri mkuu aliyejiuzulu ambaye pia ni mbunge wa Monduli,
Edward Lowassa ambaye amemuoa bintiye aitwaye Dk. Adda Lowassa.
Katika
kile kinachoonyesha kuwepo kwa nguvu ya viongozi nyuma ya pazia, Visual
Storm iliweza kupewa mkataba wa ukarabati wa tawi la Benki ya Biashara
ya Dar es Salaam (DCB) mwaka 2011 ikiwa bado haijasajiliwa na CRB kwa
mujibu wa sheria.
Kwa
mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili linazo, kampuni hiyo ilisajiliwa
kwa Msajili wa Makampuni (Brella) mwaka 2009 kwa No. 71362 na kisha CRB
Februari 23, 2013 kwa No. B5/0674/2/12 daraja la tano.
Gazeti
limebaini kuwa kabla ya usajili CRB, Visual Storm iliingia mkataba na
DCB Oktoba 3, 2011 wa kujenga ukumbi wa mikutano katika tawi la Ukonga
kwa gharama ya sh 56,676,580 kwa muda wa wiki tano.
Hata
hivyo, hadi kufikia Januari 9, 2013 zaidi ya mwaka mmoja, kampuni hiyo
ilikuwa imeshindwa kukamilisha kazi hiyo, hatua iliyomlazimu Mkurugenzi
Mkuu wa DCB, Edmund Mkwawa kuiandikia akiitaarifu kusudio la kutaka
kuvunja mkataba huo.
Nakala
ya barua hiyo pia ilipelekwa kwa msajili wa CRB, Boniface Muhegi,
ambapo Februari 12, 2013, bodi hiyo kupitia kwa kaimu meneja wa Kanda ya
Mashariki, D. J. Karugendo, ilijibu kwa kuiandikia Visual Storm na
kuipa siku saba itoe maelezo ya kushindwa kutimiza mkataba huo.
Alipotafutwa
Mkwawa ili kufafanua ni kwanini benki yake iliingia mkataba na kampuni
ambayo haikuwa imesajiliwa CRB, alisema kuwa suala hilo aulizwe Visual
Storm.
“Tunawasubiri hao CRB tukutane mahakamani, lakini kwanini usiwaulize Visual Storm wakakupa majibu?” alisema.
Hadi
gazeti linafanya uchunguzi huo, CRB inadai kuwa haikuwa na taarifa ya
kasoro hiyo ya Visual Storm kuvunja sheria ya kuingia mkataba wa ujenzi
bila kusajiliwa, licha ya kupata barua ya malalamiko ya DCB.
Katika
kosa hilo, Muhengi anathibitisha kuwa kampuni hiyo inapaswa kuadhibiwa
kwa kutozwa faini pamoja na DCB kwa kutoa zabuni kwa kampuni ambayo
haikuwa na usajili wa Bodi ya Makandarasi.
Kwa
mujibu wa chanzo chetu, kampuni hiyo ililazimika kukimbilia CRB
kujisajili baada ya kushindwa kutimiza mkataba wa DCB kwa wakati, na
hivyo kuhofia kukumbwa na rungu la adhabu baada ya benki hiyo kuanza
kulalamika.
Hata
hivyo, katika kujinasua, kampuni hiyo ilitumia nyaraka na vielelezo
visivyo halali, hatua ambayo Muhegi anasema itasababisha sasa iadhibiwe
kwa kufutiwa usajili wake, na wamiliki wake kuchukuliwa hatua za
kisheria.
Ili
kampuni iweze kusajiliwa CRB, Muhegi anasema ni lazima itimize vigezo
kadhaa kulingana na daraja husika ambapo wamiliki wanatakiwa kuwa na
wataalamu, ofisi na vifaa vya ujenzi.
Kwa
upande wa wataalam, kampuni inapaswa kuwa na mkurugenzi wa ufundi
ambaye amesajiliwa na Bodi ya Mainjinia (ERB) ambaye atakuwa ameajiriwa
na kampuni husika na kuwa mmoja wa wanahisa.
Lakini
katika hatua ya kushangaza, Kampuni ya Visual Storm, awali iliwasilisha
vielelezo vya vyeti vya Loserian Sokonoi ambaye hata hivyo
alitofautiana na mmiliki Severe na kuamua kuondoka na kuajiriwa
serikalini mkoani Shinyanga.
Kampuni
hiyo katika kusaka usajili wa haraka, ilitumia cheti cha Kent Kissima
na kumtambulisha kama mkurugenzi wao wa ufundi ilhali mtu huyo ni
mwajiriwa wa serikali akifanya kazi kama meneja wa Wakala wa Barabara
(Tanroads) makao makuu.
Awali
katika majibu yao, CRB walijikanganya wakidai mkurugenzi wa ufundi wa
kampuni hiyo ni Sokonoi, lakini walipobanwa zaidi wakadai ni Kissima
ambaye inadaiwa amehamishwa makao makuu Tanroads na kupelekwa kuwa
meneja wa Mkoa wa Simiyu.
“Mimi
ninamfahamu Kissima kama ‘technical director’ wa Visual Storm wala si
Sokonoi,” alisema Muhegi lakini alipoelezwa kuwa Kissima ni mwajiriwa na
Tanroads akafichua siri kuwa kampuni hiyo vielelezo vyake vyote
vilikuwa vya kughushi.
“Tumekwenda
huko TRA (Mamlaka ya Mapato) tumekuta kadi za vifaa walizowasilisha
huko sio vya kwao, kinachofuata sasa ni kuifuta na kuanza utaratibu wa
kuwasiliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na
vyombo vingine vya kisheria,” alisema.
Hata
hivyo, Muhegi alipobanwa alionyesha kuhamaki mara kadhaa na kuhusisha
suala hilo na fitna za kisiasa, akisema; “najua aliyekutuma ni
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha.”
Alipoulizwa
ilikuwaje hawakujiridhisha na umiliki wa vifaa hivyo kabla ya usajili,
alitoa majibu yasiyoridhisha akisingizia kuwa bodi yao haina mtandao wa
kuweza kufuatilia makandarasi wote.
Alipotafutwa
Sokonoi kuthibitisha kama ndiye bado mkurugenzi wa ufundi wa kampuni
hiyo, alijibu kwa msisitizo kuwa; “Huyo jamaa tulifanya naye kazi,
lakini wakati tukiwa kwenye mchakato huo wa usajili alionekana kunizika
fedha zangu nikajiondoa.
“Mimi
kwa sasa niko Shinyanga nimeajiriwa serikalini na nilikwishawaandikia
CRB kuwaarifu kuwa vyeti vyangu visitumike popote kwenye taasisi yao kwa
namna yoyote, maana sifanyi kazi huko tena.”
Hata
hivyo, katika kile kinachoonyesha udhaifu wa CRB, gazeti hili linayo
nakala ya makubaliano kati ya Visual Storm na Kampuni ya Fabec/Home base
(T) Ltd.
Makubaliano
hayo yanaonyesha kuwa wakati wa kukaguliwa vifaa vya ujenzi, Visual
walionyesha kwa CRB mkataba huo wakidai vifaa vyao wameikodishia Fabec
iliyokuwa na kazi ya ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Mpanda wakati huo.
Msemaji wa Fabec, Ziota, alipotafutwa alilieleza gazeti hili kuwa kampuni yao haijawahi kuwa na mkataba wa aina hiyo na Visual.
“Kampuni
hiyo wala sijawahi kuisikia, inamilikiwa na nani?” alihoji Ziota na
kufafanua kuwa hata kama wangekuwa wamekodishwa vifaa hivyo, CRB
walitakiwa kutembelea mradi wao kujiridhisha kama vipo kweli.
Hata
baada ya kusajiliwa CRB, Kampuni ya Visual Storm imeendelea kutekeleza
miradi yake mikubwa ikiwemo ile ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii
(NSSF) bila kuisajili kwenye Bodi ya Makandarasi kama sheria inavyosema
wala kufuata taratibu za kuwa na vibali vya ujenzi.
Severe ajitetea
Alipotafutwa
kujibu tuhuma hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Visual Storm, Severe alikiri na
kuonyesha mshangao akihoji nani alivujisha suala hilo kwenye vyombo vya
habari.
Alidai
kuwa ameshangaa kuona nyaraka sahihi alizompatia mshirika wake kwa
ajili ya kushugulikia usajili, zilibadilishwa na kupachikwa zile za
kughushi.
“Kaka
yaani nashangaa kwanini jambo hili linakuwa hivi, mimi hivi vifaa
unavyonionyesha hapa kampuni yetu haina na sijui hawa walivitoa wapi,”
alisema.
Alipoulizwa
kuhusu utata wa mkurugenzi wao wa ufundi, Severe alimtaja Sokonoi kuwa
ndiye waliyewasilisha jina lake CRB. Lakini alipobanwa aeleze inakuwaje
mhusika anafanya kazi serikalini, alisema walikuwa kwenye mkakati wa
kumbadilisha.
Alipoelezwa
kuwa CRB wamedai wanamtambua Kissima kama mkugenzi wa ufundi wa kampuni
hiyo, Severe alidai kutomtambua mtu huyo huku akionyesha kushangaa
alichomekwaje na kuwa mmoja wa wanahisa.
Severe
katika kujitetea alimtwisha lawama mtu aliyemtaja kwa jina la Ruben
ambaye alidai kuwa alikuwa mshirika wake kuwa ndiye alivujisha siri hiyo
kwa sababu wakati wa usajili CRB alihusishwa kwa ukaribu.
Tanzania
Daima lilimtafuta Emmanuel Ruben, ambaye alikiri kushirikiana na Severe
katika usajili wa kampuni hiyo CRB, lakini akasema kuwa baadaye
walihitilafiana katika mgawanyo wa rasilimali na hivyo akajitoa na
kuanzisha kampuni yake.
“Mimi
pale CRB nina power of attorney (nguvu ya kisheria) kwa kampuni ya
Visual Storm kwa vile tulikuwa pamoja, lakini kwa sasa niko kivyangu,
sasa hayo ya kwamba nimeleta siri hiyo kwenu ndiyo nasikia
kwako,” alisema Ruben.
chanzo:Tanzania daima
No comments:
Post a Comment