WATOTO
wawili wakazi wa Kijiji cha Ngombanya, Kata ya Kimbiji wilayani Temeke
jijini Dar es Salaam, Alhamisi ya wiki iliyopita saa 9 alasiri
walilipuliwa na bomu na kupoteza maisha. Licha ya bomu hilo kuua watoto hao, mwenzao mmoja Shaban Hassan,5, aliponea chupuchupu. Waliopoteza
maisha ni Yohana Vicent,10, na William Jeremia,8, na inadaiwa kuwa
watoto hao walilipukiwa na bomu hilo wakati wanatoka kufukuza nyani
shambani.
Katika mahojiano na gazeti hili kaka wa marehemu Yohana
aliyejitambulisha kwa jina la Venance Silungwe alikuwa na haya ya
kueleza kuhusina na tukio:
“Maeneo hayo lilipotokea tukio kuna mashamba ya mihogo ambapo watoto hao walikuwa wakiwafukuza nyani.
“Wakiwa wanarudi waliona hilo bomu ambapo walifikiria kuwa ni kitu cha
kuchezea, hivyo kuamua kulichukua na kulichezea ndipo likawalipukia.
“William alifariki hapohapo wakati Yohana alikutwa hai lakini akiwa
amejeruhiwa kichwa upande wa kulia na vidole vitatu vya mkono wa kulia
vilikatika na shingoni kulikuwa na jeraha kama vile alichomwa na kitu
chenye ncha kali, alifia njiani akiwa anapelekwa hospitali.
“Baada ya tukio hilo kutokea mtoto Shabani ambaye hakujeruhiwa alijaribu
kuwaita wenzake kwa majina, alipoona wamenyamaza aliamua kwenda kwa
wazazi wa marehemu na kuwaeleza.
“Wazazi walifuatana naye hadi eneo la tukio ambapo waliwakuta
wamejeruhiwa vibaya, William alikuwa amekwishafariki dunia na Yohana
alitapakaa damu.
“Maiti za watoto hao zimehifadhiwa katika Zahanati ya Kimbiji na tunatarajia kuzika Jumatatu (jana).”
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, SACP Engelbert Kiondo alikiri
kutokea kwa tukio hilo. “Tukio hilo limetokea na tunaendelea kufanya
uchunguzi,” alisema kamanda huyo.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameliomba Jeshi la Wananchi, kulifanyia ukaguzi eneo hilo walilokuwa wakilitumia kwa mazoezi.
-GPL
No comments:
Post a Comment