Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limefafanua kuwa askari wake aliyedaiwa
kuua raia alilazimika kufyatua risasi kujihami na watu waliodaiwa kuwa
ni vibaka waliomvamia na kumlazimisha kufungua milango ya gari lake.
Ofisa huyo, Meja Abdallah Mzee, alidaiwa kuua watoto wawili kwa
risasi siku ya mkesha wa mwaka mpya katika mkasa uliotokea Pugu
Kinyamwezi jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya ufafanuzi ya JWTZ iliyotolewa Dar es Salaam jana ilisema
kuwa Meja Mzee wakati anarudi nyumbani kwake saa 6.00 usiku akiwa
anaendesha gari aina ya RAV4, alivamiwa na vibaka waliomzingira na
kumlazimisha kufungua milango ya gari hilo.
Kitendo kilichoelezwa kwenye taarifa hiyo kuwa hakikuwa cha kawaida
hali iliyomfanya ofisa huyo kujihami kwa kurusha risasi akihofia
kudhuriwa na kuporwa gari.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Habari
Makao Makuu ya JWTZ , Meja Joseph Masanja, ilisema ofisa huyo alikuwa
anarejea nyumbani kwake akitokea katika hospitali ya Amana na kwamba
alivamiwa na vibaka hao eneo la Pugu Kinyamwezi na kwamba Meja Mzee
alikuwa na bastola anayoimiliki kihalali.
“Alianza kufyatua risasi hewani kwa lengo la kujihami na
kuwatawanya watu hao .Katika tukio hilo ofisa huyo alifanikiwa
kujinasua na kuondoka kwenye kusanyiko hilo huku akiamini kuwa watu hao
wametawanyika,” ilisema taarifa hiyo ya jeshi kwa umma.
Katika tukio hilo inadaiwa kuwa watu wawili walipoteza maisha na wengine wawili kujeruhiwa.
Awali Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala Marieta Minangi, alisema
mwanajeshi huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kuwaua kwa kuwapiga risasi
watoto wawili na kujeruhi wengine wawili baada ya kundi la vijana
waliokuwa wanasherehekea mwaka mpya kuzingira gari lake.
Minangi aliwataja marehemu hao kuwa ni Ibrahimu Mohamed (16) na
Abubakar Hassan (14) wakati majeruhi ni Rupano Wanga (17) na Kassimu
Abdul (16)
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment