Pages

Monday, January 27, 2014

Mapro Azam wabanana katika chumba kimoja




AZAM FC ina utaratibu wa kuwaweka wachezaji wawili wawili katika vyumba vya kambi yake iliyopo Chamazi Mbagala jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo hali ni tofauti kwa wachezaji Kone Muhamad, Balou na Kipre Tchetche ambao wanaishi chumba kimoja kutokana na tatizo la lugha.
Kocha wa Azam, Joseph Omog amependekeza timu yake iweke kambi Azam Complex, katika eneo ambalo uwanja wa mazoezi upo mita chache kutoka vilipo vyumba vya wachezaji.
Kone, Balou na Tchetche wenyewe wanaishi chumba kimoja kwa kuwa wote wanazungumza Kifaransa kwa kuwa kwao Ivory Coast ndiyo lugha ya taifa.
Awali chumba hicho kilikuwa kinatumiwa na pacha Balou na Tchetche ambao wanamudu pia kuzungumza Kingereza, lakini aliposajiliwa Kone, Novemba mwaka jana wanalazimika kuishi naye chumbani humo.
“Kone hawezi kuzungumza lugha nyingine zaidi ya Kifaransa, anashindwa kuwasiliana na wachezaji wengine katika mazingira ya nje ya uwanja. Tupo naye hapa chumbani ili angalau tumfundishe Kingereza ili akimudu naye aweze kuishi na wachezaji wengine,” Tchetche aliliambia Mwanaspoti chumbani humo.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa msaada wa Tchetche, Kone alisema anafurahia maisha ya Tanzania, lakini changamoto ya lugha inampa wakati mgumu.
“Nazungumza Kifaransa tu, na ninaoweza kuzungumza nao hapa ni Balou na Tchetche labda na kocha, lakini wachezaji wengine ni tatizo, nikiweza kuzungumza Kingereza nitaenda chumba kingine,” alisema Kone.
Akizungumzia hali hiyo, meneja wa Azam, Jemedari Said alisema wamemkubali Kone kuishi chumba kimoja na raia wenzake wa Ivory Coast ili kupata muda wa kujua Kingereza ili aweze kujichanganya wachezaji wengine.
“Hata Tchetche alipofika hapa alikuwa anakaa na Ibrahim Shikanda, alipojua Kingereza akajichanganya na wengine. Alipokuja Balou akaishi na Tchetche na hadi sasa wapo pamoja,” alisema Jemedari.CHANZO MWANASPOTI

No comments:

Post a Comment