Pages

Wednesday, January 8, 2014

MITIHANI INAYOWAKABILI WANAWAKE WANAPOPENDA PALE WASIPOPENDWA


 Linapokuja suala la kupenda kwa upande wa wanawake, kila mmoja anakuwa na vigezo vyake katika kumchagua mwenza hususan kwa sifa za nje. Inaweza kuwa ni maumbile ya mwili kwa maana ya unene, wembembe, urefu, ufupi au yaweza kuwa ni mtindo wa nywele kwa maana ya rasta, afro, nywele fupi zilizokatwa vizuri au yaweza kuwa mtindo wa kunyoa ndevu kwa maana ya kunyoa “O”, kufuga mustachi au mzuzu kama beberu.
Kwa kifupi ni kwamba kila mwanamke anakuwa na uchaguzi wake mwenyewe anaouzingatia linapokuja suala la kuvutiwa na mwanaume anayempenda ambapo kama akikutana naye au akimuona… “Damn!” Moyo wake unamlipuka na anajikuta akitamani mwanaume huyo japo amsemeshe.


Lakini kwa bahati mbaya ni kwamba, mapenzi ni kizungumkuti (Complex) hasa kwa wanawake kwa sababu hawana ujasiri wa kumtongoza mwanaume na kama akithubutu kufanya hivyo kibao kitamgeukia. Nani asiyejua kwamba mwanamke kujitongozesha kwa mwanaume ni kujitafutia muhali? Kwa mwanamke kujitongozesha au kujirahisisha kwa mwanaume ni kutaka kuwekwa katika kundi la malaya au kupewa thamani ya chini, labda tu kama mwanaume huyo atakuwa ana utambuzi wa hali ya juu na anajua thamani ya kupendwa.

Lakini kama mwanaume ni hayawani basi atamfanyia mwanamke huyo vibweka kwa jinsi atakavyo na kama mwanamke akilalamika atamwambia… “Si ulijipendekeza mwenyewe, huna budi kuishi nitakavyo na kama hupendi au hutaki chapa lapa!”

Naam, hebu angalia sasa jinsi mambo yanavyokuwa ndivyo sivyo. Wakati mwanamke akiwa amejiwekea vigezo vyake katika kuchagua mwenza, haimaanishi kwamba, wanaume wanaokidhi vigezo hivyo wanavutiwa nao kama wanavyodhani, hususan wale wanaume wenye sifa za nje, ma handsome boy, wenye muonekano mzuri kwa nje (Good Personality) au masharobaro ambao kila mwanamke huvutiwa nao pale wawaonapo. Tatizo ni kwamba wanaume hawa wanajua kwamba wanawake wanawababaikia, hivyo nao wanakuwa hawajatulia, ni wanaume wachache sana, narudia tena wachache sana wenye sifa hizo za nje wanaojitambua na wanaojua thamani ya kupendwa.

Binafsi nimeshawahi kukutana na hali kama hii, miaka ya nyuma sana wakati nikiwa nimedhamiria kutafuta mwenza baada ya mbilinge zangu za ujanani. Niliwahi kukutana na mwanamke mwenye sifa nizitakazo. Huyu kwangu alikuwa ni mwanamke wa ndoto zangu, nilimpenda kwa dhati na nilitumia mbinu mbalimbali ikiwemo fedha ili kumnasa, hakuonekana kunipenda na nilijikuta mimi nikiwa mtumwa wake. Mwishowe nilikubali matokeo nikachapa lapa ili kumpa nafasi au kuepusha msongamano.

Naamini wanawake wengi hukumbana na mtihani huu, ambapo mwanamke anakutana na mwanaume ambaye humtendea wema na kumuonyesha mapenzi ya dhati huku akimhudumia na kumchukulia kama malkia lakini kwa bahati mbaya mwanaume huyu masikini hakidhi viwango vyake, hana sifa (za nje) azitakazo na hata akimuona moyo wake haushtuki kabisa. 

Lakini hata hivyo wapo baadhi ya wanawake pamoja na kwamba hawawapendi wanaume hawa huwatumia kuwachuna watakavyo bila hata ya chembe ya huruma, au kama mwanamke amefunzwa kwao, atamchukulia mwanaume huyu kama wa kupita tu kwa ajili ya mitoko na kula bata na sio wa kudumu naye.

Labda sasa niwaulize wanawake, je unafanyaje unapokutana na hali kama hii? Je unaweza kumpa nafasi mwanaume huyu mwenye muafaka, yaani mwanaume anayeonekana kukujali na kukuthamini ingawa hujavutiwa naye? Je unaweza kubadili msimamo wako uliojiwekea? Au unaweza kujipa muda kusubiri mpaka pale atakapotokea mwanaume wa ndoto zako? Mwanaume ambaye ukimuona tu moyo wako unalipuka kwa mapenzi? (Lakini naamini wote mnajua jinsi jambo hilo lilivyogumu)

No comments:

Post a Comment