Moja kati ya nyumba 14 katika
Kijiji cha Shumba Mjini Wilaya ya Micheweni zilizotoathirika kwa moto
mkubwa ulitokea majira ya saa 5.00 asubuhi Jumapili hii huku wakaazi
wake wakichanganyikiwa kutokana na maafa hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini
Pemba Afande Shehani Mohamed Shehani akitoa tathmini ya awali ya
uchunguzi wa moto uliotokea Shumba Mjini mbele ya Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif aliyefika kijijini hapo kuwapa pole wananchi
walioathirika na maafa hayo.Kulia ya Balozi Seif ni Mwakilishi wa Jimbo
la Micheweni Mh. Subeit Juma Khamis na kushotoni kwake ni Mkuu wa Mkoa
wa Kaskazini pemba Mh. Dadi Faki Dadi na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba
Kanal Mstaafu Juma Kassim Tindwa.
Baadhi ya wananchi 100 ambao nyumba
zao 14 zimeathirika na vibaya na moto katika Kijiji cha Shumba Mjini
wakipata hifadhi kwenye madrasa moja Kijijini hapo.
Moja kati ya nyumba 14
zilizoathirika na moto katika kijiji cha Shumba Mjini ambapo wakaazi
wake wakiwa wamechanganyikiwa kutokana na janga hilo. Picha na Hassan
Issa wa –OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi ameiagiza Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Pemba
kufanya tathmini mara moja nyumba zote zilizoathirika kutokana na moto
mkubwa uliokikumba Kijiji cha Shumba Mjini leo majira ya saa 5.00 za
asubuhi.
Nyumba zipatazo 14 zikiwa na wakaazi
100 zimeathirika vibaya kutokana na moto huo na nyengine 24 kuezuliwa
mapaa yake kwa hofu ya kuathirika na moto huo ambao hadi sasa kwa mujibu
wa taarifa za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Shehani Mohamed
Shehani kwamba chanzo chake bado hakijafahamika. Uchunguzi wa jeshi la
polisi pamoja na vikosi vyengine vya ulinzi ukiendelea.
Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Taifa ya Maafa Zanzibar akiwa kisiwani Pemba kwa shughuli
mbali mbali za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar alitoa
agizo hilo muda mfupi baada ya kuwafariji wananchi wa Kijiji cha Shumba
Mjini kutokana na maafa waliyoyapata ya janga la moto.
Akiwapa pole wananchi hao 100
waliohifadhiwa kwenye madrasa mmoja Kijijini humo na baadaye kupelekwa
Skuli ya Kijiji hicho Balozi Seif aliwataka kuwa na subra katika kipindi
hichi cha mitihani na Serikali inajipanga kuangalia namna ya kuwasaidia
wananchi hao.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itaandaa kikao maalum cha dharura keshokutwa jumatatu ili
kulijadili suala hili na kuona jinsi itakavyoweza kukusanya nguvu za
kuwasaidia wananchi walioathirika na janga hili.
“ Wakati nimeshamuagiza Mkuu wenu wa
Mkoa kufanya tathmini ya janga hili mimi kama mtendaji Mkuu wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na vile vile nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Taifa ya Maafa Zanzibar nitawajibika kuitisha kikao cha dharuura
Jumatatu kulitafakari suala hilo “. Alisema Balozi Seif.
Alisisitiza kwamba ni wajibu wa
Serikali Kuu kutafuta mbinu na utaratibu utakaoweza kutoa fursa nzuri ya
kujaribu kusaidiana Wananchi walioathirika na Maafa hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliwashukuru wananachi na baadhi ya Taasisi zilizojitokeza kwa njia
mbali mbali kusaidia wananchi hao ikiwemo vyakula, vifaa na baadhi ya
huduma muhimu kama nguo kwa wale wananchi 100 waliokuwa wakiishi kwenye
zile nyumba 14 zilizounguwa na kuteketeza vitu mbali mbali.
Aidha Balozi Seif aliupongeza
Uongozi wa Wilaya ya Micheweni pamoja na Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa
hatua iliyochukuwa ya kuandaa mazingira ya kuwahifadhi wale wananachi
watakaokosa hifadhi na kuwapeleka katika Skuli ya Kijiji hicho cha
Shumba Mjini.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wananci
wa Kijiji cha Shumba Mjini Mwakilishi wa Jimbo la Micheweni Mh. Subeit
Juma Khamis amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
kwa hatua aliyochukuwa ya kuwafariji wananchi hao katika muda mfupi
baada ya kutokea tukio hilo, Mh. Subeit alimuelezea Balozi Seif kuwa ni
kiongozi mwenye moyo unaomuelekeza kujali wananchi wake.
Moto huo mkubwa uliokuwa ukivuma
kutokana na upepo mkali licha ya taarifa za awali za kutotambulikana
chanzo chake ulianzia kwenye Nyumba ya Bwana Masoud Ali Khamis na naadhi
ya wananchi walisikika wakisema chanzo chake kimesababishwa na watoto
waliokuwa wakijiandaa kupika mlo wa mchana.
No comments:
Post a Comment