Pages

Sunday, January 5, 2014

Schumacher : Milionea anayepigania uhai wake

schumacherclip1 a5c13
ALIZALIWA katika Mji wa Hurth, kaskazini mwa Rhine-Westphalia, Ujerumani Magharibi. Wazazi wake ni Rolf Schumacher na Elisabeth.

Alipokuwa na umri wa miaka minne, baba yake alinunua injini ndogo na kisha akaifunga kwenye gari dogo alilokuwa akichezea mwanaye huyo.
Akawa anapanda na kuendesha. Siku moja aligonga nguzo ya kuwekea taa nyumbani kwao na wazazi wake wakaamua kumpeleka kwenye shule ya kuendesha magari hayo madogo maarufu kwa jina la 'Kert' na uamuzi huo ukamfanya kuwa mtu mwenye umri mdogo zaidi kuliko wote waliokuwa kwenye shule hiyo, Kerpen-Horrem.


TUNAOMBA BOFYA HAPA NA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGI ZA KILA SIKU,(USIPITWEEEEEEEE)

Alipofikisha umri wa miaka sita akashinda ubingwa wa mbio za magari kwa upande wa klabu kabla ya kuendelea kutamba na Dunia nzima kumfahamu kwa uhodari wake kwenye usukani. Tangu hapo akafahamika kuwa dereva mashuhuri zaidi duniani baada ya kuingia kwenye mashindano ya Formula One na kutamba.
Michael Schumacher ni Mjerumani aliyeweka rekodi za aina yake kwenye ulimwengu wa mashindano ya Formula One. Mataji saba ya ubingwa wa Dunia yamemfanya kuwa dereva hodari zaidi na kuwa mwanamichezo tajiri zaidi kutokana na kulipwa pesa za maana.
Kutamba kwenye mbio hizo za magari kumempa utajiri mkubwa dereva huyo aliyezaliwa Januari 3, 1969 na sasa anatajwa kuwa na pato linalokadiriwa
kuwa Dola 800 milioni.

Habari mbaya kuhusu yeye ni kwamba kwa sasa anapigania uhai wake hospitalini, Grenoble, alikolazwa akiwa mahututi baada ya Jumapili iliyopita kupata ajali ya kugonga kichwa kwenye jiwe alipoanguka akiwa kwenye michezo ya kuteleza katika barafu.
Jinsi alivyopiga pesa
Kutwaa mataji saba ya Dunia ya mashindano ya Formula One, kumechangia sehemu kubwa ya kipato chake. Schumacher amebahatika kuwa mmoja wa wanamichezo wanaolipwa vizuri zaidi duniani.
Umashuhuri wake umemfanya awe anapata pesa hata asiposhiriki kwenye mbio. Kuvuna Dola 50 milioni kwa mwaka si kitu kigumu kwa Mjerumani huyo kutokana na mikataba ya kibiashara ya udhamini anayoimiliki.
Kwenye miaka ya ubora wake, Schumacher alikuwa akilipwa Dola 10 milioni kwa mwaka na Kampuni ya Shell kwa ajili ya kuvaa kofia tu yenye nembo yao anapokuwa mitaani.
Schumacher alitingisha zaidi kati ya mwaka 1991 na 2006 alipokuwa na kampuni za Jordan Benetton na Ferrari. Kuna kipindi alitangaza kustaafu kabla ya kurudi mchezoni mwaka 2010 na kujiunga na Kampuni ya Mercedes GP.
Mara yake ya kwanza Schumacher kushiriki kwenye Formula One ilikuwa kwenye mashindano ya Ubelgiji mwaka 1991. Miaka mitatu baadaye akaanza kuweka alama zake baada ya kuibuka mshindi kwenye mbio sita kati ya saba. Mwaka 1996 alijiunga na timu ya Ferrari.
Schumacher aliendelea kutesa kwenye mchezo huo hadi hapo alipostaafu. Staa huyo ana kipaji pia cha mchezo wa soka, anacheza kwa kiwango cha juu na kama isingekuwa kupenda mchezo wa mashindano ya magari, basi huenda angesajiliwa na moja ya klabu kubwa za soka kutokana na kipaji chake.
Familia na mambo binafsi
Agosti 1995, Schumacher alimwoa mrembo Corinna Betsch na kufanikiwa kuzaa naye watoto wawili; Gina-Maria na Mick.
Tofauti na mastaa wengine, Schumacher si mtu anayependa kuyaanika maisha yake binafsi. Kwa sasa anaishi Uswisi alikohamia tangu mwaka 2007 na anamiliki jumba la kifahari lenye ukubwa wa mita za mraba 650. Jumba hilo lina gereji chini ya ardhi na kituo cha kujaza mafuta na lipo kwenye ufukwe binafsi wa Ziwa Geneva.
Familia yake inamiliki mbwa wawili, mmoja walimpata Brazil, ambaye Corinna anampenda sana na mwingine ni wa kutoka Australia anaitwa Ed.
Wakati wanatoka kuwachukua mbwa hao, Schumacher aliendesha teksi mwenyewe kutoka Mji wa Coburg kuwahi ndege ya kwenda Uswisi na familia yake.
Alieendesha kwa kasi kubwa na kuiwahisha familia yake kupanda ndege, lakini yeye mwenyewe na dereva anayemiliki teksi hiyo walishikiliwa na polisi ili kutoa maelezo kutokana na mwendo wao.
Moja ya mambo anayoyapenda ni kupanda farasi na kucheza soka, ni mchezaji wa klabu ya mtaani kwao ya FC Echichens. Amecheza soka kwenye mechi nyingi za hisani na mara kadhaa amekuwa akiandaa mechi na madereva wenzake wa Formula One. Schumacher ni shabiki mkubwa wa klabu ya Koln ya Ujerumani na Newcastle United ya Ligi Kuu England.
Misaada
Schumacher ni Balozi Maalumu wa UNESCO na ameichangia taasisi hiyo Euro 1.5 milioni. Alilipia pia ujenzi wa shule kwa ajili ya watoto maskini na wanaoishi mitaani kwenye Jiji la Dakar, Senegal.
Ametoa misaada pia ya pesa kwenye hospitali inayohudumia watoto walioathirika na vita ya Sarajevo na huko Lima, Peru. Ana mradi wake unaoitwa 'Palace For The Poor' unaojishughulisha kuwahudumia watoto wa mitaani kupata elimu bora, mavazi, chakula, huduma za afya na makazi.
Mwaka 2008 alichangia kati ya Dola 5 milioni hadi 10 milioni kwenye kituo cha Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton. Hakika Schumacher ni mtu wa watu. Chanzo: mwananspoti

No comments:

Post a Comment