Sangoma Ramadhani Issa (20) akiwa chini ya ulinzi baada ya kunaswa.MGANGA wa kienyeji ‘Sangoma’aitwaye Ramadhani Issa (20) amedaiwa kuwatorosha watoto wawili, Salim Swalehe(13) na Laurent Oscar (13) wanaosoma katika Shule ya Msingi ya Pamba jijini hapa.
Tukio hilo limetokea Januari 20, mwaka huu
katika kitongoji cha Ujaluoni, Igogo jijini hapa baada ya watoto hao
kutoonekana kwa mwezi mzima tangu Desemba 27, mwaka jana.
Inadaiwa kwamba watoto hao walirudi
makwao kwa njia za ajabu na kusema walikuwa wamewekwa ndani kama
misukule nyumbani kwa mganga huyo.
Wazazi wa watoto hao wanaoishi Mabatini,
waliomba msaada kwa Kitengo cha Oparesheni cha Fichua Maovu (OFM) cha
Global Publishers kumnasa mganga huyo.
OFM wakiwa na mtandao wa kijamii wa
Farijika, waliambiwa na watoto hao kwamba walichukuliwa na mganga huyo
Desemba 27, mwaka jana wakiwa katika matembezi ya sikukuu.
“Mganga alitugusa na shanga vichwani na kutufanya tupoteze kumbukumbu na kumfuata kila alipokuwa akienda,” alisema Laurent.
Watoto hao walidai kufikishwa kwenye
kilinge cha mganga huyo na kufungiwa ndani huku wakilishwa karanga
mbichi na ulezi kwa mwezi mzima.
Kama haitoshi walidai mganga alikuwa
akiwalimisha na kuwachotesha michanga usiku kucha huku Salim akionesha
chale alizochanjwa sehemu za magotini na kichwani.
Mtoto Salim alisema kuwa alimuona mwenzake
Laurent akiruka kimiujiza jambo lililomshtua na kumfanya atoroke baada
ya kumuona mganga huyo kauacha mlango wazi.
“Ndani ya nyumba kuna mauzauza mengi sana, wakati mwingine tulikuwa tunasikia sauti za watoto lakini hatukuwaona.
“Hata chakula (karanga na ulezi) tulikuwa
tukipewa kingi, lakini tukila kidogo tu kinaisha kama vile tulikuwa
tunakula na watu wengine,” alisema Salim.
Mmoja wa wazazi wa watoto hao ambaye ni
Makamu wa Rais wa Chama cha Waganga wa Tiba za Jadi Tanzania (Tameto),
Swalehe Issa Bukuku, alisema kuwa watoto hao walifika nyumbani wakiwa
katika hali ya kuweweseka huku wakisisitiza walikuwa kwa mganga Igogo na
wangeweza kuwapeleka kwa kuwa wanaikumbuka njia waliyopita siku ya
kwanza.
OFM na wazazi wa watoto hao pamoja na
wanaharakati walifika kwa mganga huyo wakiwa na mwenyekiti wa serikali
ya mtaa wa Ujaluoni.
Bahati mbaya mganga huyo alikuwa ametoka
hadi ndugu yake alipompigia simu na kumtaka afike kilingeni baada ya
kuambiwa kulikuwa na wateja.
Mganga huyo alifika kilingeni kwake ndipo
OFM ikiwa pamoja na mwenyikiti wa mtaa na wazazi wa watoto hao na Polisi
Jamii, walimnasa na kumfikisha Kituo Kikuu cha Polisi cha Nyamagana na
kufunguliwa jalada la uchunguzi MW/RB/07/2014 JALADA LA UCHUNGUZI.
No comments:
Post a Comment