Vyama vya siasa vimekubaliana kutafuta mwafaka wa agenda za Katiba Mpya kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba.
Kutokana
na makubaliano hayo, vimekubaliana kuwasilisha mapendekezo yao kwenye
Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ili kuratibiwa kabla ya kuanza kwa
Bunge hilo.
Vyama
hivyo vimetakiwa kuwasilisha maoni ili yachambuliwe na kutolewa maoni ya
pamoja yatakayotumika kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Baadhi ya
vyama vimeonyesha wazi kutofautiana na Rasimu ya Katiba iliyotolewa
hivi karibuni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Chama tawala, CCM
kinatofautiana na vingine juu ya mfumo wa Muungano kikitaka Serikali
mbili wakati vingine vikikubaliana na maoni ya Tume ya Serikali tatu.
Bunge la
Katiba limepangwa kuanza Februari, mwaka huu na litakuwa na wajumbe 640,
huku 42 wakitokea katika vyama hivyo vya siasa, kila chama kikitoa
wajumbe wawili.
Akizungumza
baada ya kumalizika kwa majadiliano ya viongozi wa vyama hivyo,
Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia alisema: “Tumekubaliana kuwa mpaka
Januari 31, mwaka huu kila chama kiwe kimewasilisha maoni yake kuhusu
rasimu ya Katiba.
“Kuanzia
Februari 8 hadi 14, mwaka huu Kamati ya mashauriano itayapitia maoni
yote ya vyama ili kama kuna tofauti ziweze kujadiliwa. Tunataka tuwe na
mawazo yanayofanana ndani ya Bunge la Katiba kwa sababu Katiba Mpya ni
muhimu kuliko itikadi za vyama vyetu, nchi kwanza vyama baadaye.”
Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman
Kinana ambao walikuwapo katika mkutano huo, walikataa kutolea ufafanuzi
msimamo wa chama hicho kuhusu mapendekezo yaliyomo katika rasimu hiyo.
“Kila
kitu amezungumza msemaji wetu Mbatia, sasa mimi mnataka niseme nini
siwezi kuzungumza tofauti na makubaliano ya kikao chetu cha leo (jana),”
alisema Mangula.
Katika
ufafanuzi wake, Mbatia alisema kama vyama hivyo vitaingia katika Bunge
hilo na kuanza kupingana ni wazi kuwa vitawachanganya wananchi: “Kuna
vyama vinataka Serikali mbili vingine tatu na vingine moja, nadhani
tutakubaliana na hata ikishindikana basi tuwe na aina ya uwasilishaji
ambayo haitaleta mvutano bungeni.”
Mbatia
pia aligusia suala la maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapigakura…
“Tumeiomba Serikali kuipatia fedha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili
iweze kuliboresha daftari hilo, tunataka liwe limefanyiwa maboresho
katika upigaji wa kura ya maoni Mei mwaka huu.”
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema lengo la kukutana ni kutaka kuweka msimamo wa pamoja kwa maslahi ya taifa.
No comments:
Post a Comment