Pages

Tuesday, January 7, 2014

WAFUASI WA CHADEMA WATWANGANA TENA DAR

  Mfuasi wa Chadema akiwa chini baada ya ‘kukatwa mtama’ na mfuasi mwingine wa chama hicho baada ya kutokea vurugu baina ya wafuasi wanaounga mkono uongozi na wale wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe jana baada ya kuahirishwa kwa hukumu ya kesi ya mbunge huyo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam jana. Picha na Silvan Kiwale 

Dar es Salaam.Wafuasi wa Chadema wanaomuunga mkono aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe na wanaounga mkono uongozi wa juu, jana walitwangana tena muda mfupi baada ya kuondoka eneo la Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea huku Mahakama hiyo ikiahirisha hadi leo, kutoa uamuzi wa maombi ya Zitto kuzuia kujadiliwa na Kamati Kuu ya Chadema.
Katika maombi hayo namba 1 ya mwaka 2014, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, anaiomba Mahakama iizuie Kamati Kuu ya Chadema kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake hadi kesi yake ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Uamuzi wa maombi hayo ulipangwa kutolewa jana na Jaji John Utamwa ambaye hata hivyo, alisema alikuwa hajamaliza kuandika uamuzi huo na kuahirisha shauri hilo hadi leo mchana.
Maombi hayo ya Zitto ya zuio la muda la kujadiliwa na kuchukuliwa uamuzi wowote kuhusu uanachama wake yametokana na kesi ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.


Katika kesi hiyo, Zitto pia anaiomba Mahakama Kuu imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za kikao cha Kamati Kuu za kumvua nyadhifa zake zote alizokuwa nazo ndani ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake ya ubunge wa Kigoma Kaskazini.
Mapigano
Baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, wanachama wa makundi yote waliondoka eneo la Mahakama wakiendelea kuimba na kushangilia lakini walipofika eneo la Mahakama ya Rufani ghafla walianza kupigana ngumi na mawe. Baadhi yao walikamatwa na askari kutokana na vurugu hizo.
Awali, wafuasi hao walifika mapema asubuhi katika viwanja vya Mahakama tayari kusikiliza uamuzi huo.
Ulinzi ulikuwa umeimarishwa na askari polisi wakiwamo wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliokuwa na silaha pamoja na mabomu ya machozi walikuwa wametanda.
Pia kulikuwa na askari wa Kikosi cha Mbwa pamoja na gari la maji ya kuwasha.
Licha ya kuwahi, ni wafuasi wachache walioruhusiwa kuingia ndani ya u`kumbi wa Mahakama tena baada ya kuandikisha majina yao huku wakitambuliwa na viongozi wao waliokuwapo.
Baada ya idadi iliyokuwa ikihitajika kutimia, wafuasi wengine waliambiwa wasubiri kutapata taarifa za uamuzi huo baadaye.
Wakiwa wanasubiri, walikuwa wakitambiana kwa maneno na nyimbo.
Kundi la Zitto lilikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kumsifu na bendera za chama hicho pamoja na ngoma huku likikejeli kundi linalounga mkono uongozi wa chama hicho.
Baadhi ya mabango yalisomeka ‘Zitto kama Mandela’, ‘Zitto Mkombozi.’
Baadhi ya maneno waliyokuwa wakiyatamka katika nyimbo zao ni pamoja na `Zitto Kwanza’, chama (Chadema) baadaye.
Wafuasi wa uongozi nao walikuwa na mabango yaliyosomeka: ‘Hongera Mbowe kwa ujasiri,’ ‘Kunguru hafugiki’ na ‘Zitto rudisha kadi yetu’.
Awali, kundi linalounga mkono uongozi lilidai kwamba wanaomuunga mkono Zitto si wanachama halali wa chama hicho, bali wamenunuliwa kwa lengo la kwenda mahakamani.
Tofauti na siku ya kwanza ya kusikilizwa kwa maombi ya Zitto, ambayo kundi linalounga mkono uongozi lilidai kuwa wafuasi wa Zitto wameandaliwa na CCM, jana liliwatuhumu kuwa wameandaliwa na CUF.
Baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), walisikika wakilalamika kwa askari kuwa wafuasi hao wametoka mitaani na wengine ni wa CUF.
CUF wakana tuhuma
Hata hivyo, CUF jana kimekana kuhusika na mgogoro huo unaoendelea Chadema. Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Julius Mtatiro alisema jana kuwa kuna taarifa zimesambaa kuwa CUF kilikuwa kimeandaa vijana wa kwenda mahakamani jana kwa ajili ya kufanya vurugu.
“Wadau, waandishi wengi wa habari walinipigia nithibitishe ikiwa CUF iliandaa makundi ya wanachama wakamshabikie ZZK (Zitto) mahakamani leo (jana) hii. Taarifa ya namna hii pia imeenea mitandaoni.
“Pia viongozi kadhaa wa Chadema wamenipigia kunijulisha kuwa intelijensia yao imegundua kuwa vijana wa CUF wamepenyezwa na kwamba wamevishwa T-shirt (fulana za M4C na mapanga,” alisema Mtatiro na kusisitiza kuwa CUF hakijapanga wala kutuma makundi ya vijana kwenda kumshabikia Zitto.
Alisema ikiwa wanachama wa CUF wameonekana mahakamani itakuwa ni kwa utashi na matakwa yao.
“Hatujawahi kukutana, kupanga wala kutuma vijana wa CUF wakasimamie upande wowote katika mgogoro huu.
Wakati wa fukuto la Hamad Rashid na CUF watu wengi tu raia walifika mahakamani, hatukuhoji na kutafuta vyama vyao, tuliamini ni Watanzania tu,” alisema Mtatiro na kuongeza:
“Ni vigumu kwa CUF kukataza wanachama wake wasihudhurie kesi maarufu kama ile ya Babu Seya, Sheikh Ponda, Zitto Kabwe, Samaki wa Magufuli na nyinginezo.”


MWANANCHI

No comments:

Post a Comment