MWENYEKITI
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James
Lembeli, amesema kuwa kiasi cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya
Operesheni Tokomeza Ujangili hazijulikani zilipo.
Alisema
kuwa hatua hiyo imesababisha askari zaidi ya 2,000 waliounda kikosi
maalumu kwa ajili ya operesheni hiyo ambayo imesitishwa kwa muda kuanza
kudai posho zao.
Lembeli
aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati kamati hiyo ilipotembelea
Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) kwa ajili ya kujionea
namna hifadhi hiyo ilivyofanikiwa kudhibiti uharibifu wa mazingira na
kutunza bioanuai ya eneo la ukanda wa hifadhi ya nusu maili.
Alisema kuwa hadi sasa kiasi cha sh bilioni 1.5 za posho hizo hakijalipwa kwa askari hao.
Lembeli
alisema katika operesheni hiyo iliyoanza mwanzoni mwa mwaka 2013 na
baadaye kusitishwa Novemba mosi, serikali ilikuwa imetenga zaidi ya sh
bilioni 3.5, lakini inashangaza kuambiwa kuwa askari bado wanadai posho
zao.
Alisema
baada ya operesheni hiyo kusitishwa kutokana na ripoti ya kamati yake
iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana bungeni, askari hao bado walikuwa
wakiendelea na kazi huku wakisubiri kuanza kwa awamu ya pili ya
operesheni hiyo.
"Serikali
ilitenga zaidi ya sh bilioni 3.5 zitumike katika Operesheni Tokomeza,
inashangaza sana kuambiwa kuwa askari wale wanaendelea kusotea posho zao
hadi sasa," alisema.
Kwa
mujibu wa Lembeli, kusitishwa kwa operesheni hakukumaanisha kwamba ndiyo
ukomo wake, kwani askari waliendelea kulinda usalama wa maeneo yale, na
kwamba katika kazi hiyo ambayo wameifanya kwa moyo mmoja hadi sasa,
walitakiwa kulipwa stahili zao.
Askari
walioshiriki operesheni hiyo ni wanajeshi 480 kutoka Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ), polisi 440, wamo pia askari 440 kutoka Kikosi dhidi
ya Ujangili (KDU), askari wa wanyamapori kutoka Shirika la Hifadhi za
Taifa (Tanapa) na Usalama wa Taifa.
Wengine
ni askari 99 kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na askari
wanyamapori 51 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Alisema
ili kuondoa sintofahamu hiyo, kamati inashauri kufanyika kwa ukaguzi wa
fedha hizo pamoja na serikali kutoa ufafanuzi wa kiasi kilichobaki kwa
kueleza sababu za ucheleweshaji wa malipo ya askari hao wakati bajeti
hiyo tayari ilikwishapitishwa.
Wakati
huo huo, kamati hiyo imekutana na kushauriana na Menejimenti ya Hifadhi
za Taifa (Tanapa) na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa)
kuhusu viwango vya tozo za utalii kwenye mlima huo.
Waliitaka
serikali kulipa fursa shirika hilo kupanga viwango vya tozo za
viingilio vya utalii nchini ili kuvifanya viendane na hali halisi ya
utalii duniani badala ya utaratibu wa sasa ambao hauipi nafasi Tanapa
kupanga viwango hivyo.
"Haya
mambo tatizo hapa ni siasa, serikali inatakiwa kuangalia tozo zake na
kuacha hadithi ya kunufaisha wafanyabiashara ambao hata hivyo hawalipi
kodi.
"Hifadhi
ikipewa mamlaka kamili ya kujiendesha lazima nchi ipate faida, lakini
kwa staili hii tusipowatetea hawa Tanapa, shirika hili litakufa kama
lilivyokufa Shirika la Ndege nchini (ATCL)," alisema.
Ushauri
wa Kamati ya Lembeli, unafananishwa na taarifa za serikali ambazo
zinaonyesha kwamba kwa sasa mlima Kilimanjaro unaonekana kuzidiwa na
idadi ya watalii.
Takwimu
zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, mlima
Kilimanjaro kwa mwaka ulikuwa ukipokea wageni 13,000, lakini hivi sasa
watalii wanaopanda mlima huo ni zaidi ya 50,000 huku wapagazi wakidaiwa
kuwa zaidi ya 200,000 kwa mwaka.
Akizungumzia
changamoto hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi, alisema
shirika hilo limeweka mikakati ya kuona njia mbadala ya kupunguza idadi
ya watu wanaopanda mlima ambapo tayari wameshaanza kuwasiliana na vyama
vya wafanyabiashara ya uongozaji wa utalii kuhusu mpango huo.
Kuhusu
eneo la hifadhi ya nusu maili, Kijazi alisema Tanapa imeandaa mpango
utakaohakikisha ukanda huo unasimamiwa na kupunguza uharibifu wa
mazingira kikamilifu ambapo rasimu ya muongozo huo imeshaandikwa.
CHANZO:TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment