Kiongozi wa
Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amenusurika
kifo na mtu mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Mikidadi, ambaye
yupo mahututi katika Hospitali ya Temeke, baada ya kushambuliwa na watu
wanaodaiwa kuwa na mzozo wa ardhi eneo la Kurasini, jijini Dar es
Salaam.
Mchungaji
Mtikila alikumbwa na mkasa huo Ijumaa wiki iliyopita baada ya kufika
katika eneo hilo kwa nia ya kutaka kuwaondoa watu hao wa familia tatu
tofauti ambao wanaishi katika eneo hilo.
Kipigo
hicho ambacho kimemsababishia majeraha ya kisogoni na hata kushonwa
nyuzi tatu kichwani, kuvimba usoni na maumivu makali mwilini yalitokana
na kipigo kutoka kwa familia mbili tofauti zinazoishi katika eneo hilo
ambao wanapinga kuhama.
Pia
katika sakata hilo, Mtikila anadai kupoteza simu mbili, pesa taslimu
Sh400,000 na Dola za Marekani 2,000 na siku ya tukio na alifika hapo
akiwa ameongozana na watendaji wa Dawati la Msaada wa Kisheria katika
taasisi yake ya Liberty Fund International.
Kamanda
wa Polisi Temeke, Engbert Kiondo alikiri kutokea kwa tukio hilo na
kusema kuwa wanalifanyia uchunguzi na taarifa kamili itatolewa kesho
Jumanne.
"Ni kweli
suala hilo limeripotiwa hapa na tunalifanyia uchunguzi na kesho Jumanne
nitatoa taarifa rasmi kwa waandishi wa habari," alisema Kiondo.
Mtikila
alisema, mara baada ya kufika eneo hilo, alikwenda katika nyumba ya
kwanza na kuwakuta walinzi ambao walikubali na kuondoka katika eneo hilo
kwani tayari notisi walikuwa nayo na walikuwa wanatambua kuwa
wanatakiwa kuondoka.Alisema baadaye walikwenda katika nyumba ya pili
ambayo anaishi mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Rubein Sanga ambaye hata
hivyo vitu vyake vingi akuwa amekwisha vihamisha.
Alisema
wakiwa mbele ya nyumba hiyo gari la polisi lilifika na wakiwa hawana
hili wala lile vijana ambao anawataja kuwa ni wa Sanga walianza
kuwashambulia kwa kutumia nondo na kila aina ya silaha za jadi.
"Walinipiga
sana hadi nikapoteza fahamu na wakawa wanasema huyo Mtikila bebeni na
mumchome moto, walitaka kuniua kwani walinikwida tai hadi ikakatika,"
alisema.
Na
kuitaja pia familia ya Evelyne Mboya kuwa ilishiriki kuwashambulia.
Alisema wakati vurugu zinaendelea, ndipo akatokea mmoja wa jirani
wanaoishi katika eneo hilo aliyemtaja kwa jina la Mikidaki: "Yule bwana
alipojaribu kunitetea kuwa nisiendelee kupigwa alipigwa nondo kichwani
na akaanguka na alishambuliwa hadi kuzirai na hajapata fahamu hadi leo,"
alisema.
Mchungaji
Mtikila alisema alikuwa ameambatana pia na walinzi wawili (mabaunsa),
wafanyakazi wa dawati lake la msaada wa kisheria lililopo chini ya
taasisi yake ya Liberty Fund International na mmiliki halali wa eneo
hilo, Omar Salum Muhsin ambaye pia alijeruhiwa mkononi kwa nondo.
Mtikila
aliwataja wafanyakazi wake waliojeruhiwa kuwa ni Hemed Wendo na Gray
Mhando na akiwa amezirai alibebwa na kupandishwa katika gari hadi Kituo
cha Polisi Chang'ombe ambako yeye na wenzake walifunguliwa jalada kwa
shtaka la kuingia isivyo halali katika eneo la watu wengine. Chanzo:
mwananchi
No comments:
Post a Comment