Rais
Jakaya Kikwete amesema uteuzi wa majina 201 ya wajumbe wa Bunge Maalumu
la Katiba umekamilika na kati ya leo na kesho, atayatangaza pamoja na
tarehe ya kuanza kwa Bunge hilo. Bunge la Katiba litakalokuwa na wajumbe
640, litakutana kwa siku 90 kujadili Rasimu ya Katiba iliyotolewa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Desemba 30, mwaka jana.
"Bunge la
Katiba litakutana katika wiki ya tatu ya mwezi huu. Mambo
yanayosubiriwa ni mawili tu, uteuzi wa wajumbe 201 na siku ya kuanza kwa
Bunge hili. Mambo haya yote ninayesubiriwa kuyakamilisha ni mimi tu,"
alisema Rais Kikwete alipokuwa akihutubia katika kilele cha maadhimisho
ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM.
Alisema
kazi ya uteuzi wa wajumbe hao ilikamilika tangu juzi na kinachofanyika
sasa ni kuhariri majina hayo na kurekebisha mambo kadhaa.
"Jumatatu
(leo) tutayapitia majina haya ili tuone kama tunaweza kurekebisha. Baada
ya hapo tutaweza kutangaza na inaweza kuwa siku hiyohiyo au kesho yake
(Jumanne), hazitazidi siku hizi mbili," alisema.
Alisema
hivi sasa ukarabati katika Ukumbi wa Bunge, Dodoma bado unaendelea na
mkandarasi ameeleza kwamba hadi Februari 10, mwaka huu atakuwa amemaliza
kazi.
"Nimewapa
siku tano hadi saba za kujaribu spika na vipaza sauti ili kuhakikisha
kila kitu kinakuwa sawa, lakini pia nitakwenda kupata ushauri wa
wanasheria ili kuweza kutangaza siku ya Bunge hili kukutana," alisema.
Amshangaa Mbowe
Katika
hotuba yake Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alimshangaa
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa kauli yake kwamba mfumo wa
Serikali tatu ukikataliwa katika Bunge hilo, nchi haitatawalika.
"Huku ni
kuwadanganya wananchi, pale hakuna ngumi wala vurugu yoyote, kila ibara
iliyopo katika rasimu itajadiliwa ili upatikane mwafaka. Huku ni kukosa
ukomavu wa kisiasa," alisema.
Alisema
si kweli kwamba kila mwanaChadema anataka mfumo wa Serikali tatu na kila
mwanaCCM anapendelea mfumo wa Serikali mbili akisema kinachohitajika ni
ushawishi wa kujenga hoja ili wanaopinga wakubaliane. Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment