Endapo mapendekezo hayo yatapitishwa, hoja ya
Katiba Mpya itakayowasilishwa na Kamati ya Bunge Maalumu la Katiba,
itaamuliwa kwa kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa Tanzania
Bara na idadi kama hiyo ya wajumbe kutoka Tanzania Zanzibar.
Upigaji kura huo kwa siri, umepongezwa na baadhi
ya wabunge kwa maelezo kuwa utatoa fursa kwa wajumbe kupiga kura hizo
kwa uhuru na bila kushinikizwa na misimamo ya vyama au taasisi
zilizowapendekeza.
Kanuni hizo zimekuja wakati CCM, kikiwa
kimewaagiza wajumbe wake ambao ndiyo wengi bungeni, kutetea muundo wa
Serikali mbili badala ya ule wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Pamoja na CCM kuweka msimamo wa kuwataka wajumbe
wake kuutetea mfumo huo, kumeibuka mgawanyiko mkubwa huku baadhi yao
wakitarajiwa kukitosa na kuunga mkono mfumo wa Serikali tatu.
Kanuni ya 82(1) ya rasimu hiyo, imeweka bayana
kuwa utaratibu utakaotumika kupata uamuzi baada ya mwenyekiti kulihoji
Bunge ni wa ama kura ya siri au ya kielektroniki.
“Wakati wa kupiga kura ya siri, kila mjumbe
atapiga kura ya Ndiyo au Hapana kwa kutumia karatasi za kupigia kura
zitakazokuwa zimeandaliwa na Katibu wa Bunge,” inasomeka kanuni ya
83(1).
Kanuni hiyo imeweka wazi kuwa kupiga kura kwa
mujibu wa masharti ya kanuni hiyo, itakuwa ni wajibu na haki ya msingi
ya kila mjumbe na kwamba kila mjumbe atapiga kura kwa binafsi yake.
Hatua ya wajumbe kupiga kura hiyo, itatanguliwa na
kazi ya kila Kamati ya Bunge Maalumu, kujadili rasimu ya katiba hiyo
kulingana na mgawanyo wa majukumu. Kamati 17 zitashughulikia ibara za
rasimu.
Baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ataagiza taarifa ya kamati iwekwe kwenye orodha ya
shughuli kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni kwa mjadala.
Kanuni hizo zimeeleza kuwa wakati wa mjadala huo,
mjumbe yeyote anaweza kushauri na kutoa mapendekezo ya marekebisho au
mabadiliko kwa ajili ya kuboresha sura ya rasimu inayohusika.
Hata hivyo, Kanuni za 78 (11) na 78 (12) za rasimu
hiyo, zinapendekeza mwenyekiti asiruhusu hoja yoyote inayokiuka sheria
au pendekezo la kamati linalohusu jambo lililo nje ya mamlaka ya Bunge.CHANZO MWANAINCHI
No comments:
Post a Comment