Makundi
mawili ya wanamgambo yenye usemi mkubwa ambayo awali yalitangaza
kulitaka bunge la mpito kujiuzulu au wabunge wakamatwe, sasa yanasema
makundi ya kisiasa nchini humo yana muda wa masaa 72 kuitatuwa migogoro
yao.
makundi
ya al-Qaaqaa na al-Sawaaq yalilitaka bunge la mpito kujiuzulu hadi
kufikia leo saa tatu usiku, la sivyo wabunge wote wangelikamatwa na
kuchukuliwa kama wanya'nganyi, lakini baadaye makundi hayo yalibadili
msimamo wake na kutangaza kwamba yametowa muda wa hadi siku ya Ijumaa
makundi yote ya kisiasa yafikie ufumbuzi wa mwisho katika mgogoro
uliopo.
Msimamo huu
mpya unakuja baada ya viongozi wa makundi hayo kukutana na mwakilishi
maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Tarek Mitri, ambaye alisema
aliwatolea mwito viongozi hao kutowa nafasi ya kufanyika mdahalo wa
kisiasa juu ya suala la kufanyika uchaguzi mkuu wa mapema. Mjumbe huyo
wa Umoja wa Mataifa aliwaonya pia viongozi hao kwamba matumizi ya nguvu
yanaweza kutishia usalama wa Libya na mchakato mzima wa kisiasa katika
taifa hilo.
Kinachoshuhudiwa
sasa nchini Libya ni mpasuko mkubwa katika bunge kati ya wafuasi wa
itikadi kali na makundi yenye misimamo ya wastani. Muda wa bunge hilo la
mpito ulitarajiwa kumalizika mwezi huu, lakini upande unaoegemea
itikadi kali ukawasilisha muswaada kurefusha muda wa bunge hilo kwa
mwaka mmoja.
Kwa
upande mwingine, kutokana na shinikizo la wananchi, bunge lilipiga kura
kuitisha uchaguzi wa mapema katikati ya mwaka huu, lakini wananchi wengi
wa Libya wamekasirishwa na bunge hilo ambalo wanalitazama kama taasisi
iliyoshindwa na isiyopaswa kuendelea kuwepo hadi wakati huo.
Waziri
Mkuu Ali Zidan alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kwamba
alikuwa na vikao na makundi ya wanamgambo yanayohasimiana pamoja na
mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika hatua ya kujaribu kufikia mapatano na
kuumaliza mzozo uliopo.
Waziri
mkuu huyo alisema mapinduzi ya kijeshi na matumizi ya nguvu ili
kuwashinikiza Walibya kuchukuwa hatua yoyote ni mambo yasiyokubalika.
Zidan alipendekeza pia kufanyika kwa uchaguzi na kuwepo kipindi cha
amani cha mpito cha kugawana madaraka.
Bunge
hili la mpito lilichaguliwa mwaka 2012, likipewa jukumu la kutoa
muongozo wa kipindi cha mpito ambacho kingeliandika katiba na baadaye
kufanyika uchaguzi mpya kabla ya Februari 7. Inatarajiwa kwamba wajumbe
60 wa jopo la katiba watachaguliwa hapo kesho kushiriki katika mchakato
wa kuandika katiba hiyo.
Mgogoro
unaoendelea katika taifa hilo unashuhudiwa wakati ikiwa ni miaka mitatu
tangu kuanza kwa vuguvugu lililomuondowa madarakani mtawala wa kiimla,
Muammar Gadhafi, aliyeitalawa Libya kwa miaka 42.
Chanzo, dw.de.com/swahili
No comments:
Post a Comment