Pages

Saturday, February 22, 2014

LIBYA KWATOKOTA

libya_4303c.jpg
Makundi mawili ya wanamgambo yenye usemi mkubwa ambayo awali yalitangaza kulitaka bunge la mpito kujiuzulu au wabunge wakamatwe, sasa yanasema makundi ya kisiasa nchini humo yana muda wa masaa 72 kuitatuwa migogoro yao.
makundi ya al-Qaaqaa na al-Sawaaq yalilitaka bunge la mpito kujiuzulu hadi kufikia leo saa tatu usiku, la sivyo wabunge wote wangelikamatwa na kuchukuliwa kama wanya'nganyi, lakini baadaye makundi hayo yalibadili msimamo wake na kutangaza kwamba yametowa muda wa hadi siku ya Ijumaa makundi yote ya kisiasa yafikie ufumbuzi wa mwisho katika mgogoro uliopo.
Msimamo huu mpya unakuja baada ya viongozi wa makundi hayo kukutana na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Tarek Mitri, ambaye alisema aliwatolea mwito viongozi hao kutowa nafasi ya kufanyika mdahalo wa kisiasa juu ya suala la kufanyika uchaguzi mkuu wa mapema. Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa aliwaonya pia viongozi hao kwamba matumizi ya nguvu yanaweza kutishia usalama wa Libya na mchakato mzima wa kisiasa katika taifa hilo.
Kinachoshuhudiwa sasa nchini Libya ni mpasuko mkubwa katika bunge kati ya wafuasi wa itikadi kali na makundi yenye misimamo ya wastani. Muda wa bunge hilo la mpito ulitarajiwa kumalizika mwezi huu, lakini upande unaoegemea itikadi kali ukawasilisha muswaada kurefusha muda wa bunge hilo kwa mwaka mmoja.
Kwa upande mwingine, kutokana na shinikizo la wananchi, bunge lilipiga kura kuitisha uchaguzi wa mapema katikati ya mwaka huu, lakini wananchi wengi wa Libya wamekasirishwa na bunge hilo ambalo wanalitazama kama taasisi iliyoshindwa na isiyopaswa kuendelea kuwepo hadi wakati huo.
Waziri Mkuu Ali Zidan alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kwamba alikuwa na vikao na makundi ya wanamgambo yanayohasimiana pamoja na mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika hatua ya kujaribu kufikia mapatano na kuumaliza mzozo uliopo.
Waziri mkuu huyo alisema mapinduzi ya kijeshi na matumizi ya nguvu ili kuwashinikiza Walibya kuchukuwa hatua yoyote ni mambo yasiyokubalika. Zidan alipendekeza pia kufanyika kwa uchaguzi na kuwepo kipindi cha amani cha mpito cha kugawana madaraka.
Bunge hili la mpito lilichaguliwa mwaka 2012, likipewa jukumu la kutoa muongozo wa kipindi cha mpito ambacho kingeliandika katiba na baadaye kufanyika uchaguzi mpya kabla ya Februari 7. Inatarajiwa kwamba wajumbe 60 wa jopo la katiba watachaguliwa hapo kesho kushiriki katika mchakato wa kuandika katiba hiyo.
Mgogoro unaoendelea katika taifa hilo unashuhudiwa wakati ikiwa ni miaka mitatu tangu kuanza kwa vuguvugu lililomuondowa madarakani mtawala wa kiimla, Muammar Gadhafi, aliyeitalawa Libya kwa miaka 42.
Chanzo, dw.de.com/swahili

No comments:

Post a Comment