Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), tawi la Dar esSalaam, kimemfukuza kazi mhadhiri wa chuo hicho anayedaiwa kuhusika na vitendo vya ukiukaji wa maadili ikiwamo kufanya ngono. Mhadhiri huyo ambaye jina halikutajwa alinaswa nakamera za
kisasa za kurekodi matukio za CCTV zilizofungwa kwenye vyumba vya
madarasa ili kudhibiti nidhamu, miongoni mwa wanafunzi na wahadhiri.Kamera
hizo zimefungwa kwenye vyumba vya madarasa 20 ili kudhibiti vitendo vya
ngono baina ya walimu na wanafunzi, wizi wa mitihani na matendo mengine
yanayovunja sheria.
Hayo
yalibainishwa jana jijini na mkuu wa chuo hicho, Profesa Emanuel Mjema
(pichani), alipokuwa akizungumza na wanahabari wakati wa ziara ya Naibu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene.
Profesa Mjema, alisema, walifikia maamuzi ya
kuweka kamera hizo za kisasa ndani ya madarasa Aprili mwaka jana baada
ya kujiridhisha na taarifa za kuwapo matukio ya ukosefu wa maadili
miongoni mwa wahadhiri ikiwa ni pamoja na kutoa alama za juu kwa baadhi
ya wanafunzi wa kike baada ya vitendo vya ngono.
“Nilipoingia chuoni hapa Januari mwaka jana, nilisikia kuwa kuna baadhi
ya wahadhiri wamekosa maadili, wanatoa alama za juu kwa wanafunzi wa
kike kwa masharti hata kama hawajafaulu kwa kiwango hicho. Nikaona vyema
tuweke vifaa hivyo ili kudhibiti vitendo hivyo,” alifafanua Profesa
Mjema.
Alieleza kuwa baada ya kuweka kamera hizo 20 kwa kila darasa kuwa na
kamera moja, walifanikiwa kumnasa mwalimu mmoja kwa kitendo cha kukiuka
maadili yake ya kazi na kumfukuza kazi.
Alisema kuwa, kamera hizo pia, zinasaidia kuwadhibiti wanafunzi wenye
tabia ya kuiba mitihani, kwani mikakati iliyopo hata wakufunzi na
wanafunzi hawajui anayetunga mitihani ili mradi ipo ndani ya silabasi ya
chuo.
Kamera hizo zinadaiwa kuwa na uwezo wa kumvuta karibu mwanafunzi aliyeko
darasani na kujua anachokiandika, pia mhadhiri iwapo anachokifundisha
ni cha ukweli au anadanganya kwa hiyo zinatumiwa wakati wote kwenye
vipindi na mitihani.
Alisema, chuo kimeajiri walinzi kwa ajili ya kuwadhibiti wanafunzi ambao
wanavaa nguo ambazo hazina maadili mazuri na pia hukagua vitambulisho
wanapofika getini, lengo likiwa ni kukifanya chuo hicho kubakia katika
heshima yake.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Mbene, alipongeza jitihada hizo
zilizofanywa na chuo hicho, huku akikemea vikali tabia inayofanywa na
baadhi ya wahadhiri hao, akiongeza kuwa, ni lazima mwanafunzi apewe
madaraja ya matokeo ya mitihani kutokana na ufaulu na uwezo wake.
Pia, aliahidi kushughulikia suala la uvamizi wa eneo la chuo hicho
pamoja na maombi ya kuongezewa madarasa ikiwa ni pamoja na kupewa
majengo ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula cha Taifa (NFRA).
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment