MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia (DP), Mchungaji Christopher Mtikila
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amesema atajiuzulu ujumbe katika Bunge Maalumu la Katiba na kwenda mahakamani kama wajumbe wenzake watakataa kuirejesha Tanganyika.
Mchungaji
Mtikila aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwamo katika Bunge hilo,
alisema kwa sasa anajiandaa kufungua kesi Mahakama Kuu kutaka kuvunjwa
kwa Muungano na kudai katiba ya Watanganyika ambayo haipo.
“Nitawaeleza
wajumbe wenzangu mambo ya msingi, ikiwemo Katiba ya Tanganyika kwanza,
wakikataa najiuzulu ili niendelee na kesi yangu nitakayokuwa
nimeifungua,” alisema.
Alisema jambo la
muhimu ambalo lingefanyika kabla ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ni uundwaji wa Katiba ya Tanganyika.
Mtikila
alisema atashiriki kikamilifu katika Bunge hilo na atawaeleza wajumbe
wengine jambo la kufanya kabla ya kupitisha rasimu ya katiba
inayotarajiwa kujadiliwa kwenye vikao vitakavyoanza Februari 18 mkoani
Dodoma.
Mbali
ya Mtikila, baadhi ya wajumbe wengine waliochaguliwa kuunda Bunge hilo
maalumu, wamesema watakwenda kutetea maslahi ya nchi kwa ajili ya
Watanzania wote.
Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Florence Turuka, kwa niaba ya Rais
Jakaya Kikwete, juzi alitangaza majina 201 ya wajumbe watakaowakilisha
Bunge Maalumu la Katiba wanaotoka katika makundi 10 nchini.
Makundi hayo ni taasisi zisizokuwa za kiserikali (NGOs), taasisi za
kidini Tanzania Bara, vyama vya siasa, taasisi za elimu, watu wenye
ulemavu, vyama vya wafanyakazi, vyama vinavyowakilisha wafugaji, vyama
vya wavuvi, vyama vya wakulima na watu wenye malengo yanayofanana.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima Jumapili, baadhi ya wateule hao
waliwashauri wajumbe wenzao kuwa makini kwa kuwa katiba ndiyo sheria
mama inayowaongoza wote, hivyo hawatakiwi kupeleka matakwa ya vyama
vyao.
Naibu
Katibu Mkuu (bara) wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema
msimamo wa chama chao ni kuwakilisha wananchi huku akisisitiza kwamba
wajumbe wa Bunge hilo wanapaswa kuachana na maoni ya vyama vyao kwa kuwa
katiba ni mali ya taifa.
Wasomi wanena
Kwa upande wa wasomi na wanaharakati katika masuala ya kisiasa
wamejitokeza kupongeza na wengine kupinga uteuzi wa majina 201 ya
wajumbe watakaongia katika Bunge la Katiba litakaloanza wiki ijayo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Mwesiga Baregu, alisema ingependeza kama majina hayo yaliyoteuliwa na Rais Kikwete yangerejeshwa kwa wananchi ili wachague wenyewe.
Aliongeza kuwa wananchi walipaswa wachague wajumbe wa kuwawakilisha kama
ilivyo katika chaguzi za udiwani, ubunge na rais kwa kuwa hilo ni Bunge
linaloenda kujadili maswala yao.
“Naweza kusema kwamba, uteuzi wa rais si mbaya sana kwa kuwa umechukua
wawakilishi katika makundi yote… lakini ingependeza kama wananchi
wangejichagulia wawakilishi wao kwa kuwa lile ni Bunge lao na si
vinginevyo,” alisema msomi huyo.
Profesa Baregu ambaye alikuwa mjumbe katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakayomaliza muda wake wakati
wa kupiga kura ya maoni, alisema anatarajia wajumbe hao watawawakilisha
vema wananchi kwa kuwa waliomo ni wanaharakati, wanasiasa kutoka katika
vyama vya siasa vyote vyenye usajili wa kudumu.
Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk.
Benson Bana, alisema uteuzi huo umezingatia sheria na kuangalia makundi
yote ambayo yalitakiwa kuwa na wawakilishi.
“Nampongeza
Rais Kikwete kwa kuzingatia sheria katika uteuzi wake, lakini pia
amenifurahisha zaidi kuwachukua viongozi wote wa siasa ambao vyama vyao
vina usajili wa kudumu kwenda kuifanya kazi ya wananchi waliowaamini,”
alisema Dk. Bana.
Alisema anatarajia vongozi wa siasa ambao wamepata nafasi hiyo, wakiwa
katika Bunge hilo watajifunza kujenga hoja, kuheshimiana na kuvumiliana
ili watakapotoka hapo, waweze kuwa viongozi bora.
“Ni matumani yangu kuwa Bunge hilo litakapomaliza na rasimu hiyo
kurejeshwa kwa wananchi, viongozi hao watatumia uzoefu walionao
kuwaelimisha wananchi na wafuasi wao hoja zilizojadiliwa na kupitishwa
ili kurahisisha upigaji kura ya maoni,” alisema.
Kabla
ya kutangaza majina hayo, Dk. Turuka alisema kazi ya kuwapata wajumbe wa
Bunge hilo ilikuwa ngumu kwani walioomba walikuwa 3,754 na waliotoswa
ni 3,553.
Alisema wapo waombaji 118 waliojiteua wenyewe na kwamba kulikuwa na vimemo vya waliokuwa wakiomba uteuzi kinyume cha sheria.
Alisema uteuzi huo umezingatia ushiriki wa rika na
jinsi zote na kwa kuzingatia uwiano wa theluthi moja ya wajumbe kutoka
Zanzibar na theluthi mbili kutoka Tanganyika kwenye kila kundi.
Kwa
mujibu wa Dk. Turuka, wajumbe vijana wenye umri kati ya miaka 22 hadi 35
wapo 35; wenye umri wa kati ya miaka 36 hadi 64 wapo 145 na wenye umri
wa miaka 65 na kuendelea wapo 21.
“Hapa
kwenye umri yupo mjumbe mwenye miaka 81, tulizingatia hilo kwa sababu
uzee dawa… kati ya wote hao wapo wanawake 100 na wanaume 101 ili kuweka
uwiano wa jinsia, japo kidogo kwa wanaume imezidi kwa sababu hakuna mtu
nusu,” alisema. Chanzo Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment