Pages

Sunday, February 16, 2014

Profesa Kaisi: Daktari wa kwanza kuzalisha kwa njia ya upandikizaji upandikizaji

Ni Daktari alieonyesha moyo wa kuendelea na kazi licha ya kupata maradhi ya kiharusi yaliyomsababishia kupooza mkono na mguu. Hapana shaka kuwa maelfu ya wanawake nchini waliowahi kupata huduma zake wanamkumbuka bado kwa msaada mkubwa aliowapa na kuwasaidia kushika mimba, kuwapa ushauri wa kitaalamu au hata kuwazalisha. Licha ya kustaafu, atabakia  kukumbukwa kwa mengi hapa nchini, hasa kwa mchango wake kwenye sekta ya afya ya mama na mtoto.
Huyu si mwingine, bali ni  Profesa Malise Kaisi (pichani), Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi  ya Tiba (Muhas). Nafika nyumbani kwake maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam na ninamkuta akiwa amejipumzisha. Anaanza kwa kunipa historia  yake fupi ya  kikazi.
Atoa damu kuokoa wagonjwa - Nia ya daktari yeyote duniani, ni kuokoa maisha ya mgonjwa. Hiyo ndiyo faraja ya wataalamu wa afya walio wengi. 
Akiwa ni daktari ambaye anaipenda kazi yake, Profesa Kaisi amewahi kujitolea damu kuwaokoa wagonjwa wake katika dakika ambazo pengine walikuwa kwenye bonde la uvuli wa mauti.
“Unajua wakati ule, damu ilikuwa ni tatizo kubwa. Hakukuwa na benki ya damu kama ilivyo sasa, hivyo unapopata mgonjwa anayehitaji damu na yupo mikononi mwako, lazima ujitoe mhanga” anasema
Anakumbuka mwaka 1970 ambapo alimpokea mgonjwa aliyepata ajali mbaya na alihitaji damu. Ilibidi ajitolee damu yake ili kumwokoa mgonjwa yule.
“Nikiwa Newala mwaka 1970 huo huo, mgonjwa wangu aliyekuwa anajifungua aliishiwa damu sana na ikabidi nitoe damu yangu haraka sana na kumuwekea na alipona,” anasema
 Mara nyingine akiwa ndiyo kwanza ameripoti kwenye kituo kipya cha kazi huko Mtwara, alifika na kumkuta mgonjwa akiwa kwenye hali mbaya na hakuwa na mtu wa kumpa damu hivyo alikuwa akisubiriwa kufa, yeye alitoa damu yake na mgonjwa akapona.
“Cha muhimu ni kufahamu  kama una maambukizi au la. Ukishajijua, unatakiwa utoe damu kama wewe ni daktari,” anasisitiza Profesa Kaisi.
Azalisha kwa kutumia IVF - Profesa Kaisi, ni daktari wa kwanza Mtanzania kuzalisha kwa njia ya IVF  hapa nchini na kufanikiwa   kusababisha mimba zaidi ya 11 kutungwa kwa njia hiyo.
 IVF ni mchakato wa utungishwaji wa mimba kwa upandikizaji wa mbegu za mwanamke na mwanaume kwenye nyumba ya uzazi ya mwanamke.
Anasema akiwa na daktari kutoka Korea , Otman Bauer, walifungua Kliniki  ya majaribio mwaka 1989  ambayo ilikuwa ikiwasaidia wanawake walioshindwa kushika ujauzito.
 Wanawake waliozalishwa kwa njia ya  IVF ni wale ambao walikuwa hawawezi kushika ujauzito kwa sababu kama vile mirija ya kupitisha mayai kukatika, mayai kushindwa kupevushwa au kuwa na maradhi mengine yanayozuia utungishwaji wa mimba.
IVF hufanyikaje? - Profesa Kaisi anasema, yai la mama hupevushwa  kwa kutumia dawa maalumu na hufuatiliwa  kwa kutumia mashine ya uchunguzi wa ndani ya mwili (ultrasound).
“Baada ya yai kukomaa, sindano maalum yenye wembamba mithili ya unywele huingizwa ukeni hadi kwenye mirija na yai lililopevuka huchukuliwa na kutolewa nje” anasema
 Yai  au mayai hayo  huwekwa kwenye chombo maalumu (test tube) kabla ya kuhamishwa  kwenye beseni maalumu ambalo litalifanya liendelee kuwa hai licha ya kutoka nje ya mwili wa binadamu.
“Beseni hilo halina budi kuwa na mazingira kama ya mwilini, kwa mfano joto, mwanga na kusiwepo na sauti, kwani yai huweza kuharibika kwa kasoro ndogo ndogo sana,” anasema
Anaongeza kuwa wakati huo  mbegu za mwanaume hupimwa kama hazina walakini na  hutolewa kwa mwanaume kujichua au kama hawezi kujichua basi hutakiwa kufanya tendo la ndoa na mke wake na kisha mbegu kukingwa na kuwekwa kwenye chombo maalumu.
Mbegu za baba, hutakiwa kutolewa saa mbili mara baada ya  yai la mama kutolewa ili visipishane.  “Baada ya yai na mbegu kutolewa,  hatua inayofuata ni kuichoma mbegu kwenye yai kwa kutumia sindano maalum. Mchakato huu unaitwa kwa kitaalamu, Intra Cytoplasmic Sperm Injection au ICSI), ” anasema.
Anaeleza kuwa, baada ya mbegu na yai kuchanganywa, huwekwa kwenye chombo maalum cha  joto kitaalamu ‘Incubator” kwa saa 40 kabla ya kuwekwa  au kupandikizwa kwenye kizazi cha mama.
 “Hali kadhalika, ‘incubator’ inatakiwa kuiga hali ya tumboni mwa mama wakati yai la mama na mbegu za baba vinapowekwa kabla ya kuwekwa kwenye kizazi cha mama, kwa mfano joto, mwanga na sauti” anasema Profesa Kaisi.
Hata hivyo,  Profesa Kaisi anasema IVF ina mafanikio makubwa kwa mtu yeyote isipokuwa wanawake wenye umri wa miaka 40 na kuendelea .
Anaeleza zaidi kuwa, wanawake walio wengi hudhani kuwa ni wagumba, lakini kumbe hawajafahamu matatizo yao.
Umuhimu wa madaktari - Profesa Kaisi anasema, bado madaktari nchini hawapewi umuhimu unaolingana na kazi yao, bado hawathaminiwi   kwa mchango wao.
 Kwa mfano, anasema, hakuna mtu anayejali kuwa madaktari hufanya kazi kwa saa 24 na wakati mwingine kukosa wakati wa kupumzika hata na familia zao.
“Wakati mwingine mimi nilikuwa nakosa hata muda wa kuonana na watoto wangu. Zinapita hata siku tano, sijawaona watoto” anasema
Anasema, viongozi wengi hawafahamu umuhimu wa madaktari ndiyo maana wanakwenda kutibiwa nje.
 Historia yake - “Kabla ya kuingia chuo kikuu, nilibahatika kusoma Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, ambako nilisoma na Samwel Sitta (Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Joseph Mungai na Muhidin Ndolanga, ” anasema
Anasema alianza kazi Hospitali ya Muhimbili (sasa Hospitali ya Taifa), mwezi Aprili mwaka 1969 baada ya kumaliza Shahada ya Udaktari.
Profesa Kaisi, alishika nafasi hiyo hapo Muhimbili kwa muda mfupi kabla ya kuhamishwa Hospitali ya Mawenzi iliyoko Moshi Mkoani Kilimanjaro mwaka 1970.  Mwaka 1971 alichaguliwa kuwa Daktari Mkuu wa Mkoa wa Mtwara (RMO).
Anasema alipata nafasi ya kujiendeleza kielimu ambapo mwaka 1973 alikwenda Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba cha Muhimbili (Muhas) ambako alibobea kwenye masuala ya tiba ya magonjwa ya wanawake hasa ugumba.
Kwa elimu hiyo, alikuwa ni daktari bingwa wa kwanza nchini wa magonjwa ya wanawake.
Aliendelea na kazi hadi mwaka 1976 ambapo alitakiwa kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba (Muhas) kazi aliyoifanya hadi mkwaka 1998 alipostaafu.
Hata hivyo, kutokana na unyeti wa taaluma yake, Profesa Kaisi hakustaafu moja kwa mojabali alipata mkataba wa kuendelea kufundisha hadi  serikali ilipotengua mikataba yao Novemba mwaka jana.
Profesa Kaisi anasema, kutokana na kubobea kwenye masuala ya uzazi kwa wanawake, aliamua kuanzisha huduma ya  mama na mtoto ili kuwasaidia wanawake vijijini.
“Niliomba fedha kwa wafadhili kwa ajili ya mafunzo kwa wakunga ambao walikwenda mkoani Mtwara kuwasaidia wanawake walioathiriwa baada ya vita iliyokuwa ikiendelea Msumbiji wakati huo” anasema
Anasema huduma hiyo ilisaidia sana wanawake wengi kupata huduma ambayo ilipunguza vifo vya mama na mtoto maeneo ya vijijini.

Anamaliza kwa kusema: “Madaktari si mashetani wala malaika, wanapogoma wasilaaniwe,  bali maslahi yao yaangaliwe upya kwani kazi yao ni ngumu.”
Chanzo - Mwananchi

No comments:

Post a Comment