Pages

Saturday, February 15, 2014

RAIS KIKWETE:KUNA MAJANGILI PAPA 40 NCHINI

Wakati kuna joto la vyombo vya habari vya kimataifa kuituhumu Tanzania kuwa haipambani na ujangili, Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali imeubaini mtandao unaojumuisha watu 40, akiwemo tajiri maarufu mkoani Arusha.Akihojiwa juzi jioni na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Rais Kikwete alikanusha taarifa zilizotolewa na gazeti la Sunday Mail la Uingereza zilizodai Tanzania haijafanya juhudi za kupambana na ujangili wa meno ya tembo, akisema taarifa hizo ni uzushi na upuuzi mtupu.“Gazeti hilo limezungumza na nani, ndiyo maana sitaki kupoteza muda kujadili upuuzi, achana na mambo hayo. Ndiyo maana tunasema, akutukanaye hakuchagulii tusi,” alisema Rais Kikwete.Alisema inashangaza kuona watu wanaozusha taarifa hizo hawaoni jinsi tulivyofanya jitihada za kutokomeza ujangili, kama operesheni za tokomeza ujangili na operesheni kipepeo.Kuhusu majangili 40 ambao wametambuliwa, Rais Kikwete alisema wameutambua mtandao mkubwa wa majangili unaoongozwa na mfanyabiashara mkubwa wa Arusha Mjini.“Kuna majangili 40 waliotambuliwa na tumetambua mtandao mzima, pale Arusha kuna mtu mkubwa alikuwa anaendesha biashara. Kazi ilikuwa ni kutambua mtandano wote, ule mtandao ni mpana sana,” alisema Rais Kikwete.

Katika mahojiano hayo, Rais Kikwete alisema, Tanzania ilikuwa ni nchi yenye tembo wengi zaidi duniani, lakini ujangili ulipokithiri, tembo walipungua na kufikia 57,000 tu mwaka 1987.
“Mwaka 1989, Taasisi ya Kimataifa ya Cites, walipiga marufuku biashara ya meno ya tembo duniani na ujangili ulipungua kwa kiasi kikubwa hivyo tembo waliongezeka na kufikia, 110,000 mwaka 2009,” alisema.
Kikwete ahojiwa CNN
Rais Jakaya Kikwete amekiri kuwa vita dhidi ya ujangili ni tatizo sugu linaloielemea Tanzania.
Wakati idadi ya tembo ikiendelea kupukutika kila siku, vita dhidi ya ujangili ilichukua sura mpya mwishoni mwa mwaka jana baada ya operesheni iliyofahamika kwa jila la Tokomeza Ujangili, kukumbwa na kashfa ya ukiukwaji wa haki za binadamu na kusababisha mawaziri wanne kujiuzulu.
Mawaziri waliojiuzulu ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo.
Akizungumza katika kipindi cha Televisheni ya CNN ya Marekani kinachoendeshwa na mtangazaji, Christiane Amanpour, Rais Kikwete alisema vita dhidi ya ujangili ina changamoto kubwa.
“Hizo ni changamoto tunazokumbana nazo. Baada ya kuona wahifadhi wanaelemewa na mzigo, niliagiza Jeshi la Polisi lisaidie na walifanya. Baada ya kuona polisi wenyewe wanashindwa, tukaweka wanajeshi na hiyo ilikuwa operesheni tokomeza ili kupambana na majangili,” alisema na kuongeza:
“Wao walikamata hadi wafugaji na ng’ombe wao. Hapo ndipo kulikuwa na ripoti za uvunjifu wa haki za binadamu, tukasema hilo halikubaliki. Ndiyo maana mawaziri wanne waliwajibika na kusimamisha operesheni ili kuangalia upya.”
Hata hivyo, alisema kuwa operesheni hiyo itaendelea siku za usoni.
Akifafanua zaidi jinsi Serikali ilivyochukua hatua, Rais Kikwete alisema:
“Wakati wa uhuru Tanzania ilikuwa na tembo 350,000… Mwaka 1987 walibaki 55,000…Juhudi za kupambana na ujangili zimeanza muda mrefu. Tangu mwaka 1989 kulikuwa na Operesheni Uhai na tulifanikiwa, kwani mwaka 2009 idadi ya tembo ilifikia 110,000,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mwaka 2010 kulizuka aina nyingine ya ujangili na hii ni ya upuuzi kabisa. Kwa mfano katika pori moja kulikuwa na tembo 30,000 na wote walikwisha… Ni jambo gumu sana.”
Ili kuendeleza mapambano hayo, Rais Kikwete pia amezitaka nchi zilizoendelea kutoa misaada kwa nchi za Afrika ili ziweze kupambana.
“Wito wangu na viongozi wengine wa Afrika ni kwamba, kwanza ili kupambana katika vita hii, lazima kuwe na rasilimali watu, kuajiri askari wa wanyamapori na wapewe mafunzo,” alisema na kuongeza:
“Nchi zilizoendelea kama Uingereza na Marekani watatusaidia katika mafunzo na vifaa, silaha, uangalizi na vyovyote vile watakavyojitolea.”
Alipoulizwa kuhusu upigaji marufuku kama ilivyofanywa na Marekani, Rais Kikwete alisema ipo dhamira ya kufanya hivyo.
“Tunazo zaidi ya tani 112 za meno ya tembo na tunafikiria hilo. Tulikuwa na wazo la kuomba kibali cha kuyauza, lakini tumeghairi huu siyo wakati wake. Kwa sababu ingekuwa ni kufungua mlango wa biashara hiyo,”
“Wito wangu ni kupiga marufuku biashara hiyo. Kama hakutakuwa na mahitaji ya meno ya tembo hakutakuwa na sababu ya kuua tembo. Hivyo wataishi salama.”
Alipoulizwa kuhusu utajiri wa rasilimali wakiwemo wanyamapori, gesi na madini, Rais Kikwete alikiri kuwa haziwanufaini Watanzania licha ya takwimu za uchumi kuongezaka.
“Uchumi wa Tanzania unakuwa kwa asilimia saba kwa mwaka, lakini ukuaji huo ni kwenye sekta za mawasiliano, uchukuzi na viwanda. Kwa hiyo mtu mtaani anajiuliza, au sijasikia vizuri, anafikiria mbona bado ni maskini, hakuna umeme, maji huduma za afya.
“Wakati uchumi unakua hivyo, uondoaji wa umaskini unakua kwa asilimia mbili na tathmini yetu kwa hii asilimia saba inachangiwa na sekta za mawasiliano, usafirishaji na viwanda.”
Awali mtangazaji Amanpour alinukuu baruapepe ya Mtanzania aliyejitambulisha kwa jina la ‘Car washer’ (muosha magari) akisema:
“Watu pekee wanaofaidika na ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa gesi ni viongozi wa Serikali huku wananchi wengi wakiogelea kwenye umaskini.”
Hata hivyo, Rais Kikwete alikanusha:
“Kusema kwamba tunapata zaidi ya Dola 100,000 ni upotoshaji. Hata hivyo, nasema wazo hilo ni zuri..,” alisema na kuongeza:
“Sekta inayoajiri watu wengi ni kilimo na inakua kwa asilimia nne. Sasa kama kilimo kitakua haraka kama sekta nyingine basi tutaendelea. Jinsi ya kufikia hapo ndiyo tunafanyia kazi, ndiyo mchango wangu,” alisisitiza.
Kuhusu haki za mashoga, Rais Kikwete alionyesha kusita kukubaliana na hoja hiyo kwa Tanzania:
“Itachukua muda kwa watu wetu kukubali mila za Magharibi. Siwezi kusema sasa kwamba niko tayari… haiwezi kutokea kwa sasa.
“Haiwezi kutokea Tanzania … Nakumbuka wakati fulani Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron aliwahi kuibua jambo hilo na lilileta malumbano mengi. Wakati huo pia kulikuwa na ziara ya Mwanamfalme, Prince Charles. Kwa hiyo hilo bado,” alisema Rais Kikwete.
Nyalandu
Serikali imeacha nia yake ya awali ya kuwasilisha ombi la kukubaliwa kuuza akiba ya pembe za ndovu katika chombo cha kimataifa kinachosimamia biashara ya wanyapori (CITES), ikiwa ni hatua ya kuunga mkono vita dhidi ya biashara haramu ya meno ya tembo.
Msimamo huo ulitolewa juzi jijini London, Uingereza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu wakati wa mkutano wa kimataifa unaojadili namna ya kukabiliana na biashara haramu ya wanyamapori duniani (Conference on Illegal Wildlife Trade).
Akiwasiliana na Mwananchi kwa njia ya mtandao jana, Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete alimkariri Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kutia saini makubaliano ya kushiriki harakati za taasisi ya Hillary Clinton ya Clinton Global Initiative inayopigania kupiga marufuku kwa biashara ya meno ya tembo.
Waziri Nyalandu alitumia mkutano huo kuelezea juhudi na mafanikio ya Tanzania katika vita dhidi ya ujangali ambapo alisema hadi mwishoni mwa mwaka jana zaidi ya watuhumiwa 320 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo za Jumuiya ya Ulaya (EU), Bara la Asia (China) na Afrika walitiwa mbaroni kwa kujihusisha na biashara ya meno ya tembo.
“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, tani 19.7 za meno ya tembo zilikamatwa katika maeneo mbalimbali duniani kati ya hizo, tani 15.2 zilikamatwa na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na vyombo mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya Kimataifa,” Shelutete alimkariri Waziri Nyalandu akiueleza mkutano huo.
Alisema Serikali itafanya sensa kubwa katika hifadhi na mapori ya akiba nchini kubaini idadi kamili ya tembo waliopo huku akibainisha kuwa hadi sasa, utafiti unaonyesha kuwa tembo walioko ndani ya maeneo ya hifadhi wako salama zaidi kulinganisha na walioko nje ya hifadhi.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imetajwa kama moja ya hifadhi salama kwa tembo barani Afrika baada ya kufanikiwa kudhibiti idadi ya tembo wanaouawa kutoka watatu kwa mwezi hadi sifuri katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.Mwaka jana, Serikali ilifanya sensa ya tembo katika mifumo wa ya kiikolojia ya Selou-Mikumi na Ruaha-Rungwa na kubaini kuwa katika ikolojia ya Selou-Mikumi, idadi ya tembo katika mfumo wa ikolojia ya Selou-Mikumi imepungua kutoka 38,975 mwaka 2009 hadi 13, 084 mwaka jana, huku katika mfumo wa kiikolojia wa Rwaha-Rungwa wakipungua kutoka 31,625 hadi 20,000.Rais Jakaya Kikwete anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ulioitishwa na Serikali ya Uingereza na kuhudhuriwa na washiriki kutoka zaidi ya nchi 47 duniani pamoja na mashirika 13 ya kimataifa.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo unajadili jinsi ya kuimarisha usimamizi wa sheria, mchango wa mfumo mzima wa sheria za jinai katika kukabiliana na biashara haramu ya Wanyamapori.
Mengine ni jinsi ya kupunguza mahitaji ya bidhaa zitokanazo na wananyamapori, maendeleo endelevu kwa jamii zilizoathiriwa na biashara haramu ya wanyamapori na mikakati ya kuwanusuru wanyama kama tembo, faru, tiger na makundi mengine ya wanyama wanaolengwa na wawindaji haramu kutokana na thamani ya pembe na ngozi zao.
-MWANANCHI–

No comments:

Post a Comment