Maisha uliyoishi zamani hayawezi kukukwamisha kufikia malengo uliyojiwekea. Hakuna mtu ambaye alifikiri leo hii Muhando
angeweza kuwa mwanamuziki mkubwa wa nyimbo za Injili anayelipwa fedha
nyingi kutokana na muziki wake, hasa kwa wale waliomjua tangu utoto
wake. (HM)
Lakini mwanamuziki huyo aliyesaini mkataba wa miaka mitano na Kampuni ya Sony Music Africa ya
Afrika Kusini alioanza kuutumikia mwaka huu 2014, anasema kuwa maisha
yake yalianzia katika hali duni kwani alikuwa akiombaomba baada ya
kufukuzwa katika familia yake huko Dumila mkoani Morogoro kwa kosa la
kubadili dini.
"Nilikuwa
mwimbaji mzuri sana wa kaswida, nilihudhuria kila siku madrasa nikiwa
Dumila. Baadaye maisha yangu yalikuwa magumu sana, chanzo cha haya yote
ilikuwa ni ugonjwa uliosababisha afya yangu kudhoofu. Kwa wakati huo
nilipimwa kila ugonjwa sikukutwa na tatizo, ndipo siku nilipoamua kwenda
katika maombi," anasema Rose Muhando ambaye sasa anatamba na wimbo
Wololo alioutoa chini ya Sony Music Africa.
"Nikiwa na mtoto wa miezi sita niliwahi kufukuzwa na mchungaji mmoja jijini Arusha kwa
kuwa tu nilikwenda kumwomba msaada wa fedha kidogo za kurekodi studio.
Kitu hicho kiliniuma sana na sitakisahau katika maisha yangu. Kila
nikikaa hukumbuka na kuumia sana."
Anasimulia kuwa alianza safari ya
kurejea nyumbani, lakini kwa bahati nzuri njiani alikutana na watu
wenye asili ya Somalia na kujitambulisha kwao kuwa aliwahi kuwa muumini
wa dini ya Kiislamu, nao walimsaidia na kumsafirisha hadi mkoani
Morogoro.
"Nashukuru
Mungu mpaka nilipofika sasa nina albamu nne, sanjari na tuzo sita, tatu
kutoka albamu ya Mteule Uwe Macho nilizopata mwaka 2005, Tuzo ya
Mwimbaji Bora wa
nyimbo za Injili mwaka 2009 na Tuzo ya Tanzania Broadcasting
Corporation ( TBC), kupitia wimbo wangu Nibebe, huku mwaka 2008 nikipata
tuzo kutoka Kenya Groove Awards kama Mwimbaji Bora wa nyimbo za Injili
Afrika," Rose anajinasibu.
Macho (2004), Kitimutimu (2005), Jipange Sawa Sawa (2008) na Yesu Kung'uta albamu iliyotengenezwa chini ya Sony mwaka huu 2014.
Anaweka
wazi kuwa Februari 2011, ndipo alisaini mkataba na Kampuni ya Sony
uliojulikana kama (Multi Album Recording Deal with Sony Music) na kuwa
msanii wa kwanza kusaini mkataba huo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
Maisha yake chini ya Sony Music Africa
Rose
anatanabaisha kwamba licha ya kusaini mkataba huo mwaka 2011, lakini
Januari mwaka huu ndipo alipoanza kuutumikia na utadumu kwa miaka mitano
hadi mwaka 2018.
"Nilisaini
mkataba miaka miwili iliyopita, lakini wakati huo nilikuwa bado
ninamalizia baadhi ya mikataba mingine, hivyo tumeanza rasmi mwaka huu.
Nashukuru Mungu kwani ni mkataba mnono wenye kila aina ya neema.
Nagharimiwa kila kitu, kazi yangu mimi ni kuimba tu, hicho ndicho
natakiwa kukiwasilisha kwa Sony Music Africa," Rose anaweka wazi.
Anadokeza kwamba kuna tofauti kubwa kati ya mkataba huo na ile ya nje ya nchi kama wa Sony.
"Mimi
Rose Muhando sina vitu vinavyonisonga, kila kitu nafanyiwa na Sony,
kuanzia mavazi, chakula, malazi, yaani kila kitu. Lakini mikataba ya
hapa nchini ni tofauti kwani meneja ndiyo anakuwa bosi wako, sasa mimi
ni bosi wa Sony Music Africa," anasema.
Anafafanua
kwamba kwa mkataba huo mpya sasa wanaotaka kumwalika katika matamasha
na mialiko mingine nje na ndani ya nchi, wanapaswa kuwasiliana na Sony,
lakini mialiko ya mikutano ya Injili, hiyo kwake ni ibada.
"Mikutano
ya Injili yote kwangu ni ibada hii haipo chini ya Sony, naweza kufika
na kuhudhuria wakati wowote. Lakini inategemea ni mahala gani kwani
mapatano ni kitu cha msingi," Rose anaweka wazi.
Albamu ya Yesu Kung'uta (Wololo)
Akizungumzia
albamu yake mpya aliyoiandaa chini ya Kampuni ya Sony Rose anabainisha:
"Katika albamu ya Wololo iliyotengenezwa chini ya Sony kuna kazi
nimefanya nikiwa Afrika Kusini, lakini nyingi nimefanyia hapa Tanzania
baada ya wao (Sony) kuridhia kwamba studio hizo zina ubora wa kutosha, nimekuwa nikisafiri kwenda Afrika Kusini na kurudi mara kwa mara."
Muhando
anasema kuwa albamu hiyo ina jumla ya nyimbo nane akitaja baadhi kuwa
ni wimbo Yesu Kung'uta maarufu kwa jina la Wololo uliobeba jina la
albamu na Uko Juu Sana.
"Mpaka
sasa nimeshaachia nyimbo hizo mbili; Uko Juu Sana na Wololo, neno
lililotumika kama kibwagizo katika wimbo wa Yesu Kung'uta. Video ya
wimbo huu ilitengenezewa Afrika Kusini na wote walioshiriki katika video
hiyo ni kutoka Afrika Kusini," anasema.
Nyota
huyo wa muziki wa Injili aliamua kutoa ya moyoni mwake kuhusu hali ya
sintofahamu miongoni mwa wasanii nchini, akisema inachafua tasnia ya
sanaa Tanzania kwenye anga za kimataifa. "Nachukizwa sana na baadhi ya
wasanii wa muziki wa kizazi kipya, Injili, waigizaji na mastaa wengine
kutumia mwanya wa sanaa, kufanya mambo mengine yasiyo haki mbele za
Mungu. Kwa nini usiishi maisha yako? Kwa nini uwe na tamaa ya kufanikiwa
haraka bila jasho? Inaniumiza, ninapowaona wasanii wanakamatwa na dawa
za kulevya nje ya nchi," anasema na kuongeza:
"Tunadhalilishwa
sana, imefika hatua hatuaminiki tena. Ni lazima sasa tutambue kwamba
anasa siyo maisha yanayofaa, wengi wetu tukishapata umaarufu tu
tunajisahau,. Sasa wewe unavyobeba dawa za kulevya na kuingiza nchini,
si unaua taifa la kesho?"
Anasema
kuwa kinachomuumiza zaidi ni kwamba wanaoshiriki katika masuala hayo ni
wanawake, akionya : "Biblia inasema 'usinie (usitake) makubwa kupita
uwezo wako." Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment