JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
TAARIFA KWA UMMA
RATIBA YA UZIMAJI WA MITAMBO YA UTANGAZAJI YA ANALOJIA AWAMU YA PILI
Ndugu wananchi,
napenda kuchukua nafasi hii kuwataarifu kuwa Awamu ya Pili ya
Uzimaji wa Mitambo ya Utangazaji ya Analojia itaanza rasmi mwezi Machi
mwaka huu. Awamu hii ya Uzimaji inaanza baada ya Serikali kujiridhisha
na matokeo ya tathmini ya uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya
analojia awamu ya kwanza kwenye miji saba ya Dar Es salaam, Tanga,
Mwanza, Dodoma, Mbeya, Moshi na Arusha. Tathmini hiyo imeonyesha kuwa
asilimia 89% ya watanzania kwenye miji hiyo wamehamia kwenye mfumo mpya
wa utangazaji wa dijitali.
Ninaamini kuwa
asilimia kumi na moja ya watanzania waliobaki kwenye miji hiyo watakuwa
wameingia katika mfumo wa dijitali hadi hivi sasa.
Ndugu wananchi, Awamu ya Pili ya Uzimaji wa Mitambo ya Utangazaji ya Analojia itaanza mwezi Machi mwaka huu katika miji tisa na kukamilika mwezi Oktoba 2014. Miji hiyo ni Singida, Tabora, Musoma, Bukoba, Kigoma, Morogoro, Kahama, Iringa na Songea.
Natoa wito
kwa wadau na wananchi wote kushirikiana na Serikali katika kutekeleza
vema zoezi hili la uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya analojia kwa
manufaa ya Taifa letu na wananchi wote kwa ujumla.
Asanteni sana.
Imetolewa na:
Prof. Makame M. Mbarawa (MB.)
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia
DAR ES SALAAM
21/02/2014
No comments:
Post a Comment