-Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bi M.K Tarishi akibadilishana
mawazo na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu, kulia ni Kaimu
Katibu Tawala wa Ruvuma Bw. Severin Tossi
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bi M.K Tarishi akihutubia wakati
wa ufunguzi wa Tamasha la Utamaduni na Kumbukizi ya Vita ya Majimaji
katika ukumbi wa Songea Club,kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Bw
Joseph.J. Mkirikiti na kulia ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma
Bw Severin Tossi.
Philip
Maligisu, Mhifadhi Kiongozi Makumbusho ya Majimaji akitoa maelezo kwa
wajumbe katika eneo ambalo lilikuwepo kanisa katoliki la kwanza nchini.
HOTUBA
YA KATIBU MKUU, WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, BI. TARISHI M.K WAKATI
WA UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA UTALII WA UTAMADUNI NA KUMBUKIZI YA VITA
YA MAJIMAJI TAREHE 25 FEBRUARI 2014, UKUMBI WA MALIASILI, MJINI SONGEA-RUVUMA
========== ======== ========
Awali
ya yote, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha
kuifikia siku ya leo. Ninayo furaha kubwa kupewa heshima ya kuwa Mgeni
Rasmi katika ufunguzi wa maadhimisho haya muhimu kwa historia ya nchi
yetu. Nimefurahi kwa sababu hii imekuwa ni fursa kubwa na ya pekee
kwangu kukutana na kufahamiana na wadau wa urithi wa utamaduni
kutoka Kanda ya Kusini hususan mkoa wa Ruvuma. Kupitia fursa hii,
nitapata nafasi ya kubadilishana uzoefu nanyi wadau wetu muhimu
mnaotusaidia katika jukumu la kuhifadhi, kulinda, kuendeleza rasilimali
za urithi wa utamaduni na utalii katika ukanda huu wa Kusini.
Ndugu wageni waalikwa na wadau wetu,
Nimefurahishwa
pia na utaratibu huu wa wadau kukutana na kujadili namna ya kuendeleza
utalii wa utamaduni na kuenzi mchango wa Mashujaa wetu wa Vita ya
Majimaji. Utaratibu huu ni mzuri kwa sababu unatekeleza Sera na
Sheria zetu ambazo zinaelekeza ushirikishwaji wa wadau katika
kuhifadhi na kuendeleza kumbukumbu za kihistoria na kutunza maeneo ya
urithi wa utamaduni. Aidha, napenda kuwakumbusha kuwa sote kwa ujumla
wetu tunawajibika kuuenzi kwa kutambua na kutumia kiundelevu urithi wa
utamaduni uliopo katika maeneo yetu. Kila mdau anayo nafasi katika
kuendeleza na kuimarisha rasilimali hizi kwa manufaa ya Taifa letu.
Ndugu wadau wenzangu,
Nimefahamishwa
kuwa katika maadhimisho haya tutapata fursa ya kutembelea baadhi ya
vivutio vya utalii vilivyopo katika Mkoa wa Ruvuma. Aidha,
nimefahamishwa kuwa baada ya kutembelea vivutio hivyo, kutakuwa na
warsha ya wadau ambapo jumla ya mada nne zinazolenga katika
matumizi endelevu ya urithi wa utamaduni na uendelezaji wa utalii
katika Ukanda huu zitawasilishwa na kujadiliwa. Nimefahamishwa pia kuwa
lengo la kufanya hivyo ni kuwawezesha mfanye ulinganifu baina ya hali
mtakayokuwa mmeiona wakati mkitembelea vivutio vya utalii na mada
zitakazowasilishwa ili muweze kutushauri kulingana na hali halisi ya
vivutio husika.
Ndugu Wadau,
Napenda
niwakumbushe kuwa wakati mtakapokuwa mnatembelea vivutio vya utalii na
kujadili mada zitazowasilishwa, zingatieni kuwa lengo kuu la
Serikali ni kushirikisha wadau wote katika kutunza, kuhifadhi,
kuendeleza urithi wa utamaduni na utalii ili kuchangia katika kujenga
uchumi imara, endelevu na unaolenga katika kuboresha maisha ya
Watanzania wote.
Wadau
mnayo nafasi kubwa ya kuchangia katika majadiliano haya kwani
mawazo na michango yenu ndio itasaidia kufikia lengo linalokusudiwa.
Ninaamini kuwa kupitia uzoefu wenu, mtaweza kutushauri sisi watendaji
tunaohusika na usimamizi wa shughuli za kuendeleza urithi wa utamaduni
na utalii. Nami nawaahidi kuwa Ofisi yangu itashirikiana na Ofisi ya
Mkuu wa Ruvuma kushughulikia ushauri wote mtakautoa.
Ndugu wadau,
Naomba
nichukue fursa hii kumkaribisha rasmi Profesa Audax Z.P Mabulla,
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika
Wizara ya Maliasili na Utalii na kumwaahidi kuwa Wizara iko tayari
kumwezesha ili aweze kutekeleza majukumu ya utunzaji wa urithi wa
utamaduni na kuwawezesha Watanzania kufurahia na kuuenzi urithi wetu
ikiwa ni pamoja na kuendeleza kusimamia na kuratibu hili tamasha la
Utalii wa Utamaduni na Kumbukizi ya Vita ya Majimaji.
Ndugu wadau,
Mwisho
nimalizie kwa kuwashukuru tena nyote kwa kukubali kushiriki katika
maadhimisho haya. Baada ya kusema hayo machache, ninawatakie
maadhimisho mema na kutamka kwamba maadhimisho ya Utalii wa Utamaduni
na Kumbukizi ya Vita ya Majimaji kwa mwaka 2014 yamefunguliwa rasmi.
CHANZO JIACHIE BLOG
No comments:
Post a Comment