Pages

Wednesday, February 26, 2014

UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA UTALII WA UTAMADUNI NA KUMBUKIZI YA VITA YA MAJIMAJI MJINI SONGEA-RUVUMA

-Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bi M.K Tarishi akibadilishana mawazo na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu, kulia ni Kaimu Katibu Tawala wa Ruvuma Bw. Severin Tossi
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bi M.K Tarishi akihutubia wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Utamaduni na Kumbukizi ya Vita ya Majimaji katika ukumbi wa Songea Club,kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Bw Joseph.J. Mkirikiti  na kulia ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Bw Severin Tossi.
Philip Maligisu, Mhifadhi Kiongozi Makumbusho ya Majimaji akitoa maelezo kwa wajumbe katika eneo ambalo lilikuwepo kanisa katoliki la kwanza nchini.

HOTUBA YA KATIBU MKUU,  WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, BI. TARISHI M.K WAKATI WA UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA  UTALII WA UTAMADUNI NA KUMBUKIZI YA VITA YA MAJIMAJI TAREHE 25 FEBRUARI 2014, UKUMBI WA MALIASILI, MJINI SONGEA-RUVUMA
 ==========  ========  ========




Awali ya yote, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuifikia siku ya leo. Ninayo furaha kubwa kupewa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi   wa maadhimisho  haya muhimu kwa historia ya nchi yetu.  Nimefurahi kwa sababu hii imekuwa ni  fursa kubwa na ya pekee kwangu kukutana  na kufahamiana na  wadau  wa urithi  wa utamaduni kutoka Kanda ya Kusini hususan mkoa wa Ruvuma.  Kupitia  fursa hii, nitapata nafasi ya  kubadilishana uzoefu  nanyi  wadau wetu  muhimu mnaotusaidia katika jukumu la kuhifadhi, kulinda, kuendeleza rasilimali za urithi wa utamaduni na utalii katika ukanda huu wa Kusini.  

Ndugu wageni waalikwa na wadau wetu,
 Nimefurahishwa pia na utaratibu huu wa  wadau kukutana na kujadili namna ya kuendeleza utalii wa utamaduni   na kuenzi mchango wa Mashujaa wetu wa Vita ya Majimaji. Utaratibu huu ni  mzuri  kwa sababu   unatekeleza Sera na Sheria zetu ambazo zinaelekeza  ushirikishwaji wa wadau  katika kuhifadhi na kuendeleza kumbukumbu za kihistoria na kutunza maeneo ya urithi wa utamaduni.  Aidha, napenda kuwakumbusha kuwa  sote kwa ujumla wetu tunawajibika kuuenzi kwa kutambua na kutumia kiundelevu  urithi wa utamaduni  uliopo katika maeneo yetu.   Kila mdau  anayo  nafasi  katika  kuendeleza na kuimarisha rasilimali  hizi  kwa manufaa ya Taifa letu.

Ndugu wadau wenzangu,
Nimefahamishwa kuwa katika maadhimisho haya tutapata fursa ya kutembelea baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo katika Mkoa wa Ruvuma. Aidha, nimefahamishwa kuwa baada ya kutembelea vivutio hivyo, kutakuwa na warsha ya wadau  ambapo  jumla ya  mada  nne  zinazolenga katika matumizi endelevu ya urithi wa utamaduni na uendelezaji  wa utalii katika Ukanda huu zitawasilishwa na kujadiliwa.  Nimefahamishwa pia kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwawezesha mfanye ulinganifu baina ya hali mtakayokuwa mmeiona wakati mkitembelea vivutio vya utalii na mada zitakazowasilishwa ili muweze kutushauri kulingana na hali halisi ya vivutio husika.

Ndugu Wadau,
Napenda niwakumbushe kuwa wakati mtakapokuwa mnatembelea vivutio vya utalii na  kujadili  mada zitazowasilishwa,  zingatieni  kuwa lengo kuu la Serikali  ni kushirikisha wadau wote katika kutunza, kuhifadhi, kuendeleza urithi wa utamaduni na utalii  ili kuchangia katika kujenga uchumi imara, endelevu na unaolenga katika kuboresha maisha ya Watanzania wote. 

Wadau  mnayo nafasi kubwa ya kuchangia katika  majadiliano   haya  kwani mawazo na michango yenu ndio itasaidia kufikia lengo linalokusudiwa. Ninaamini kuwa  kupitia uzoefu wenu,  mtaweza kutushauri sisi watendaji tunaohusika na usimamizi wa shughuli za kuendeleza urithi wa utamaduni na utalii.  Nami nawaahidi kuwa Ofisi  yangu itashirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Ruvuma    kushughulikia  ushauri  wote mtakautoa. 



Ndugu wadau,
Naomba nichukue fursa hii kumkaribisha rasmi Profesa Audax  Z.P Mabulla,  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Makumbusho  ya Taifa la Tanzania   katika Wizara ya Maliasili na Utalii  na kumwaahidi kuwa Wizara iko tayari kumwezesha ili aweze kutekeleza majukumu ya utunzaji wa urithi wa utamaduni  na kuwawezesha  Watanzania kufurahia na kuuenzi urithi  wetu ikiwa ni  pamoja na kuendeleza kusimamia na kuratibu hili tamasha la Utalii wa Utamaduni na Kumbukizi ya Vita ya Majimaji.   

Ndugu wadau,
Mwisho nimalizie kwa kuwashukuru tena nyote kwa kukubali kushiriki katika maadhimisho  haya.  Baada ya kusema hayo machache, ninawatakie  maadhimisho  mema na kutamka kwamba  maadhimisho ya Utalii wa Utamaduni na Kumbukizi ya Vita ya Majimaji kwa mwaka 2014 yamefunguliwa rasmi.
CHANZO JIACHIE BLOG

No comments:

Post a Comment